Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-01-02 17:59:59    
Lugha na maandishi ya makabila madogo madogo nchini China yahifadhiwa na kuendelezwa

cri

Katika kipindi hiki tutawaeleza jinsi China inavyohifadhi na kuendeleza lugha na maandishi ya makabila madogo madogo.

Wasikilizaji wapendwa, mliosikia ni wimbo wa kabila la Wamongolia. Wimbo huo unajulikana kote nchini China kutokana na mtandao wa internet na wengi kuufanya wimbo huo kuwa ni mlio wa simu za mkononi. Ingawa wengi hawafahamu nini kinachoimbwa lakini kutokana na sauti yake na mtindo wake mzito wa kikabila, wimbo huo unawavutia sana.

China ni nchi yenye makabila mengi, licha ya kabila la Wahan ambalo ni kabila kubwa na lenye watu wengi, pia kuna makabila madogo madogo 55. Kati ya makabila hayo, mengi yana lugha na maandishi yao, na baadhi yanatumia zaidi ya lugha na maandishi ya aina mbili. Hivi sasa nchini China kuna lugha zaidi ya 80, na maandishi zaidi ya aina 20 ya makabila madogo madogo. Kwa mfano, kabila la Wamongolia, licha ya kuwa na lugha na maandishi yake, lugha hiyo inakwenda sambamba na wakati kwa kutohoa maneno mapya na istilahi.

Lakini kwenye baadhi ya makabila hali ni tofauti kabisa. Wasikilizaji wapendwa, mliosikia ni wimbo wa kabila la Waman lililoko katika sehemu ya kaskazini mashariki ya China unaoimbwa wakati wa kufanya tambiko. Ingawa kabila hilo lina watu zaidi ya milioni kumi, lakini wanaofahamu lugha ya Kiman hawafikii 100.

Lugha ya Kiman ilitumika sana kabla ya miaka 200?kwani ilikuwa ni moja ya lugha za kiserikali katika Enzi ya Qing iliyotawaliwa na kabila la Waman nchini China. Lakini pamoja na kumalizika kwa utawala wa enzi hiyo, lugha ya kabila hilo iliachwa kutumika, na zimeachwa nyaraka nyingi zilizoandikwa kwa lugha hiyo. Ili kufahamu vilivyo historia, China imeweka mpango kamili wa kuhifadhi na kuendeleza lugha kama ya Kiman zilizokuwa hatarini kutoweka, ikishirikisha wataalamu wa lugha kurekodi, kuratibu na kuchapicha kamusi na kutengeneza picha za video. Kutokana na kuthamini lugha hizo, baadhi ya watu wa makabila madogo madogo walijitokeza kujifunza ili kurithisha lugha zao.

Lugha ni chombo cha kusheheni utamaduni, bila ya lugha utamaduni hauwezi kurithishwa. Mkurugenzi wa kitengo cha lugha za makabila madogo madogo katika Kamati ya Mambo ya Makabila Madogo Madogo ya China Bi. An Qingping alieleza,

"Katiba ya taifa na Sheria ya Kujitawala ya Makabila Madogo Madogo nchini China inaeleza wazi kwamba makabila madogo madogo yana uhuru wa kutumia lugha na maandishi yao, na uhuru huo lazima uheshimiwe bila kupuuzwa au kugeuzwa kwa kulazimishwa."

Kwa mujibu wa takwimu, nchini China kuna watu milioni 50 wanaotumia lugha na maandishi yao ya kikabila, seikali ya China imechukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha uhuru wao. Mfano ni kwamba waraka wa mkutano wa serikali kuu unaofanyika kila mwaka unatolewa kwa lugha za makabila ya Mongolia, Uygur, Kazak, Korea, Zhuang na Yi, na wakati hotuba inapotolewa inaambatana na tafsiri ya lugha hizo.

Ili kuhakikisha lugha na maandishi ya makabila madogo madogo yanaendelea na kukamilishwa, kuanzia miaka ya 50 serikali ya China inawashirikisha wataalamu kuchunguza, kutafiti na kuratibu lugha na maandishi ya makabila madogo madogo, na imeanzisha idara za kila ngazi toka serikali kuu hadi serikali za mitaa kushughulikia kazi hiyo. Na katika sehemu zote za makabila madogo madogo lugha za kikabila zinaweza kuwa lugha za kufundishia katika shule za msingi na sekondari, na baadhi ya makabila yameanzisha masomo ya shahada ya juu yanayofundishwa kwa lugha za kikabila. Bw. Zhoujia Cairang ni mwalimu wa Chuo Kikuu cha Makabila Madogo Madogo cha China, alisema,

"Nafundisha historia ya Tibet, utamaduni wa dini na tafsiri kati ya Kichina na Kitibet. Wanafunzi wangu watashughulika na kazi ya utamaduni wa Kitibet baada ya kuhitimu."

Hivi sasa vituo vya redio vya ngazi mbalimbali nchini China vinatangaza habari kwa lugha za aina 21 za makabila madogo madogo, na kuna mashirika zaidi ya 80 ya uchapishaji yanayochapisha magazeti, vitabu na video kwa lugha 15 za makabila madogo madogo.

Katika zama hizi ambapo kompyuta zinatumika sana, lugha za makabila madogo madogo nchini China pia zimeanza kutumika kwenye kompyuta.

Mkurugenzi wa ofisi ya kazi ya lugha na maandishi ya makabila madogo madogo katika Kamati ya Mambo ya Kikabila ya China Bi. An Qingping alieleza,

"Karibu maandishi yote ya makabila madogo madogo yanaweza kutumika katika kompyuta kwenye mfumo wa Windows, watu wa makabila madogo madogo wanaweza kusoma na hata kuwasiliana kwa lugha zao."

Idhaa ya Kiswahili 2006-01-02