Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-01-02 19:43:02    
Mgogoro wa gesi kati ya Russia na Ukraine waongezeka

cri

Kutokana na nchi mbili za Russia na Ukraine kushindwa kuafikiana kuhusu bei ya gesi ya asilia kwa mwaka 2006 itakayotolewa na Russia kwa Ukraine, kampuni ya gesi ya Russia Gazprom tarehe moja Januari mwaka huu kupunguza msukumo kwenye bomba la usafirishaji wa gesi kwa Ukraine. Jambo hilo si kama tu limeongeza mgogoro wa bei ya gesi kati ya Russia na Ukraine, bali pia limevutia uangalifu mkubwa wa Ujerumani na Poland nchi zinazoagiza gesi kutoka Russia kupitia bomba linalopita nchini Ukraine. Wachambuzi wamechukulia kuwa, kuongezeka kwa mgogoro wa gesi kati ya Russia na Ukraine si kama tu kunahusu suala la kiuchumi, bali pia kumeonesha kuongezeka kwa tofauti za kisiasa kati ya nchi hizo mbili.

Kwa kipindi kirefu Russia inatoa mafuta na gesi kwa Ukraine na nchi nyingine za Jumuiya ya madola huru kwa bei ya chini iliyowekwa na Urusi ya zamani. Lakini baada ya kuingia mwaka 2005, Russia ilianza kurekebisha sera ya kutoa nishati kwa nchi za jumuiya ya madola huru, na kuanza kutoa nishati kwa nchi hizo kwa bei ya kimataifa hatua kwa hatua. Russia na Ukraine zilianza kufanya mazungumzo kuhusu bei ya gesi tokea mwezi Mei mwaka jana, lakini hadi leo pande hizo mbili bado hazijaafikiana kuhusu bei ya gesi. Russia inashikilia kuongeza bei ya gesi kwa dola za kimarekani 220 hadi 230 kwa mita za ujazo 1000 kutoka 50, lakini Ukraine inatumai kuwa bei hiyo itaongezwa katika vipindi tofauti ili kupunguza hasara zitakazoletwa na jambo hilo kwa sekta husika nchini Ukraine. Kutokana na tofauti kubwa za msimamo wa nchi hizo mbili, mazungumzo kati ya nchi hizo mbili yamekwama. Tarehe 31 Desemba mwaka jana, rais Vladimir Putin wa Russia aliitaka serikali ya Russia na kampuni ya gesi ya nchi hiyo ziendelee kutoa gesi kwa Ukraine kwa bei ya mwaka 2005 katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka 2006, lakini Ukraine inapaswa kusaini mkataba wa kununua gesi kutoka Russia kwa bei ya sokoni kuanzia miezi mitatu ya pili ya mwaka 2006 kabla ya tarehe 31 Desemba mwaka 2005. Kutokana na Ukraine kushindwa kujibu pendekezo hilo la rais Putin, Russia imeamua kusimamisha utoaji gesi kwa Ukraine kuanzia tarehe moja Januari mwaka 2006.

Ukraine inahitaji gesi asilia kiasi cha mita za ujazo bilioni 80 kwa mwaka, na mita bilioni 25 za ujazo zinaagizwa kutoka Russia. Baada ya Russia kusimamisha utoaji gesi kwa Ukraine, Ukraine ilisema hivi sasa utoaji wa gesi wa nchini humo unaweza kukidhi mahitaji ya kimaisha ya wananchi wake. Hata hivyo wizara inayoshughulikia mambo ya dharura ya Ukraine imeunda idara ya uongozi ya kukabiliana na matukio dharura, ili kufuatilia kwa makini hali ya dharura itakayoweza kutokea. Isitoshe, kwa upande mmoja rais Yushchenko alisema kuwa nchi yake inakubali kununua gesi kutoka Russia kwa bei ya sokoni, lakini haitakubali bei ya dola za kimarekani 230 kwa mita za ujazo 1000, kwa upande mwingine Ukraine pia inatafuta njia nyingine ya kununua gesi. Imefahamika kuwa, Ukraine imekubaliana na Turkmenistan, ambayo imekubali kutoa gesi yenye mita bilioni 40 za ujazo kwa Ukraine kwa bei ya dola za kimarekani 50 kwa mita za ujazo 1000 katika mwaka mmoja kuanzia tarehe moja Januari, hivyo Ukraine haitakabiliwa na upungufu wa gesi.

Wachambuzi wameainisha kuwa, mgogoro wa bei ya gesi kati ya Russia na Ukraine pia una msingi wa kisiasa. Baada ya Bw. Yushchenko kushika madaraka ya urais mwaka 2004, alianza kufuata sera ya kuzingatia uhusiano na nchi za magharibi, kujitahidi kujiunga na NATO kabla ya mwaka 2008, na kuikosoa jumuiya ya madola huru inayoongozwa na Russia. Isitoshe Ukraine imedai bei kubwa kuhusu suala la kuwepo kwa kikosi cha manowari cha Bahari nyeusi cha Russia nchini Ukraine. Mambo hayo yameathiri maendeleo ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Inasemekana kuwa mgogoro wa bei ya gesi kati ya Russia na Ukraine kwa kweli kunaonesha kuongeza kwa tofauti za kisiasa kati ya pande hizo mbili.

Idhaa ya Kiswahili 2006-01-02