Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-01-03 17:38:39    
Barua 0101

cri

Leo ni tarehe mosi Januari mwaka 2006, kwanza tunawatakia wasikilizaji wetu heri na baraka ya Mwaka mpya. Tunawashukuru wasikilizaji wetu kwa juhudi mlizofanya mwaka 2005 kwa kutuunga mkono, ni matumaini yetu kuwa katika mwaka mpya 2006, mtaendelea kutusaidia ili tuweze kuandaa vipindi vizuri zaidi kwa wasikilizaji wetu.

Sasa tunawaletea barua tulizopokea kutoka kwa wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu Mbarouk Msabah wa sanduku la posta 52483 Dubai- Falme za Kiarabu anasema katika barua yake kuwa, alihuzunishwa sana na kitendo cha waziri mkuu wa Japan Bw. Junichiro Koizumi hivi karibuni kwenda kwenye hekalu lijulikanalo kama "yasukuni" mjini Tokyo, kutoa heshima kwa mizimu ya wahalifu wa vita kuu ya pili ya dunia.

Kwa kweli hatua kama hiyo inaweza kuashiria kwamba Japan haina majuto yoyote kutokana na uvamizi wake wa kijeshi ilioufanya dhidi ya nchi jirani mbili za China na Korea katika vita ya pili ya dunia, na kusababisha vifo na mateso makubwa kwa maelfu ya raia wasiokuwa na hatia wa nchi hizo, pamoja na kufanya uharibifu mkubwa wa mali na miundo mbinu.

Hekalu la "Yasukuni" limewekwa vibao vya mizimu ya wahalifu wa kivita wa Japan milioni 2.5 waliokufa katika vita hivyo wakiwemo viongozi wa juu kabisa wa kijeshi na kiserikali, waliohusika moja kwa moja katika kuandaa uvamizi huo, kama vile aliyekuwa waziri mkuu wa Japan wa kifashisti Bw. Hideki Tojo ambaye hatimaye alihukumiwa kifo na mahakama ya kimataifa ya wahalifu wa kivita ya mataifa yaliyoshinda vita dhidi ya Japan na kuwaua mwaka 1948. Bila shaka hekalu la Yasukuni halipaswi kuwa ni eneo lililostahiki heshima na utukufu alioupa waziri mkuu wa Japan Bw. Koizumi. Kwani huko ni kuchochea hisia za mirengo ya "kifashisti" miongoni mwa Wajapan pamoja na kukejeli "utu" wa maelfu na mamia ya Wachina na Wakorea ambao waliuawa kinyama chini ya mikono ya wavamizi hao wa kijapan.

Hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa waziri mkuu huyo wa Japan Bw Koizumi kwenda kwenye hekalu hilo la "yasukuni" kutoa heshima, jambo ambalo Bw Msabaha anasema kwa maoni yake anadhani halikupaswa kurejewa tena, ili kurejesha hali nzuri ya maelewano katika ya nchi hiyo na majirani zote.

Msikilizaji wetu Gulam Haji Karim wa sanduku la posta 504 Lindi Tanzania ametuletea barua akisema, anapenda kwa mara nyingine tena kutoa shukrani zake za dhati kabisa kwa mama Chen. Anasema kwa sasa tayari zawadi aliyowekewa Zanzibar kwa mkuu wa Radio Tanzania Zanzibar, imeshafika mikononi mwake pamoja na fulana na radio ya bandi 10. Anasema radio hiyo ni nzuri na itamsaidia katika safari zake za vijijini.

Msikilizaji wetu Ludovick S. Mathias Lunguya wa sanduku la posta 90 Mkwajuni Mbeya-Tanzania anasema katika barua yake kuwa anapenda kutoa shukrani zake kwa uongozi wote wa Radio China Kimataifa kwa mawasiliano mazuri. Pili anashukuru kwa kumtumia jarida la Daraja la Urafiki, kwani ni jarida hilo ni zuri na linajulisha mambo mengi na litasaidia sana wasikilizaji kuifahamu zaidi China, ndiyo maana anatoa pongezi nyingi kwa uongozi wa Radio China Kimataifa na kwa wasikilizaji walioshiriki kikamilifu katika kulipamba jarida hilo. Na tatu anatoa shukrani nyingi kwa bahasha ambazo tumekuwa tukimtumia, kwani anasema zimemrahisishia sana katika kutuma barua na kuwa na uhakika wa kupata majibu kwa urahisi na kwa haraka sana.

Pia ana maoni, anasema anauomba uongozi wa Radio China kimataifa uboreshe zaidi matangazo, kwani huko aliko Mkwajuni Mbeya hapati matangazo vizuri. Anamaliza kwa kusema anapenda kumshukuru mkuu mpya wa Radio China Kimataifa kwa risala yake ya mwaka mpya wa 2005, na kwa maelezo yake mazuri.

Msikilizaji wetu Mashauri Missana ambaye barua zake huhifadhiwa na Maijo Missana wa sanduku la posta 346, Magu Mwanza-Tanzania, anasema katika barua yake anatumai kuwa sisi Beijing ni wazima tukiendelea na kazi za kusukuma gurudumu la maendeleo. Yeye anapenda kutupongeza kwa kuwezesha kuchapishwa kwa jarida dogo la "Daraja la Urafiki". Pia anapenda kutoa pongezi na shukrani kwa mkuu mpya wa Radio China Kimataifa Bwana Wang Gengnian, watangazaji na uongozi wote kwa ujumla, kwani ni furaha kwa wasikilizaji kuona barua na maoni yao yakichapishwa ndani ya jarida na kusambazwa pande zote duniani.

Anasema furaha yake itaongezeka iwapo mpango wa kujenga kituo cha kurusha matangazo barani Afrika utakamilika, anatumai kuwa hiyo itakuwa ndio mwisho wa usikivu mbaya unaotokana na mabadiliko ya hali ya hewa. Itakuwa ndio mwisho wa ukiwa wa baadhi ya watu wasio na uwezo wa kwenda kwenye internet mara kwa mara, maana kwa nyakati fulani huwa wanapitwa na vipindi kadha wa kadha kutokana na sababu mbalimbali. Anatumai kuwa maoni yake tutayafanyia kazi akiwa kama mmoja wa wasikilizaji wetu wa miaka mingi.

Msikilizaji wetu Happyanus Pilula wa sanduku la posta 47 Dodoma Tanzania anasema katika barua yake kuwa, ni matumaini yake kuwa sote hapa Beijing tu wazima tukiendelea kuchapa kazi vilivyo, kama wanavyoshuhudia katika matangazo yetu ya kila siku. Anasema yeye bado anaendelea na kazi zangu, ikiwemo kubwa ya kueneza sifa na kazi nzuri za Radio China Kimataifa. Anasema anafahamu kuwa kutokana na kazi zetu ipo siku moja tutatembelea sehemu mbalimbali, na mitaani katika Afrika Mashariki tutawakuta watu wakisikiliza Radio China Kimataifa. Anasema hayo yote yatafanikiwa mapema, endapo tutaunganisha mawazo yetu na nia zetu katika kuieneza na kuijenga Radio China Kimataifa, kwani wahenga walisema Penye nia pana njia, umoja ni nguvu utengano ni udhaifu na panapofuka moshi, moto lazima uwake.

Hivyo anasema anapenda kuwaomba tena wasikilizaji wenzake wa Radio China Kimataifa waungane na kuanzisha klabu za wasikilizaji wa Radio China Kimataifa, kwani kwa kufanya hivyo kazi ya uenezaji wa sifa hizi za Radio China Kimataifa itakuwa rahisi zaidi tofauti na ilivyo sasa, ambapo karibu kila msikilizaji anafanya kazi hii pasipo ushirikiano na wenzake. Kwa kufanya hivyo pia wataweza kuunganisha mawazo mbalimbali ya wasikilizaji na hivyo klabu itaweza kuwasilisha maoni yenye nguvu na yenye kusaidia katika kuijenga na kuiimarisha Radio China Kimataifa.

Anasema vilevile muungano huo utaweza kusaidia kuongeza idadi ya wasikilizaji na sio kupungua tena kama inavyotokea sasa kwa baadhi ya klabu. Kwani anasema yeye amefuatilia na kugundua kwamba wasikilizaji wengi wanawasiliana na Radio China Kimataifa mara moja moja tu. Punde wanapomwagiwa sifa za Radio China Kimataifa wanapotea. Kama hawa watakuwa tayari wamejiunga na klabu hizo wataweza kushauriwa na kuendelea kuitegea sikio Radio China Kimataifa.

Pia anasema anapenda kutuarifu kuwa amepokea kitabu cha kuwa nami jifunze Kichina pamoja na bahasha zilizolipiwa gharama za stempu za kutosha. Anasema anatumai kuwa, kwa kuwa na hicho kitabu ataweza kupiga hatua katika harakati za kujifunza Kichina. Kwani anasema kimemuongoza vizuri sana katika matamshi na kusoma.

Pia anasema katika uchunguzi wake amegundua kuwa vijana ndio nguzo na wasikilizaji wakubwa wa Radio China Kimataifa. Hivyo ili vijana waweze kuvutika zaidi angependa hapo baadaye vipindi vitakavyoanzishwa, kiwepo na kipindi ambacho kitaweza kujadili mambo ya jamii hasa yale yanayowakumba vijana kama vile ugonjwa wa Ukimwi na jinsi gani waweze kuuepuka.

Mwisho Anamaliza kwa kusema anapenda kututakia kazi njema, kwani anasema matunda ya kazi zetu wanayaona, kama uongozi wa radio china Kimataifa ulipokwenda kutembelea Afrika ya Mashariki siku za karibuni.

Idhaa ya Kiswahili 2006-01-03