
Kutokana na nchi mbili za Russia na Ukraine kushindwa kuafikiana kuhusu bei ya gesi ya asili kwa mwaka 2006 itakayotolewa na Russia kwa Ukraine, kampuni ya gesi ya Russia Gazprom tarehe 1 Januari mwaka huu ilisimamisha usafirishaji wa gesi kwa Ukraine. Jambo hilo limeathiri mara moja usafirishaji wa gesi ya asili wa Russia kwa nchi za Ulaya, na kuleta wasiwasi kwa watu wa nchi za Ulaya kuhusu usalama wa nishati.
Nchi za Ulaya mashariki na kati zinazotegemea kwa kipindi kirefu gesi kutoka Russia zimeathirika zaidi na usimamishaji wa gesi wa Russia. Takwimu zilizotolewa tarehe 2 na nchi mbalimbali zinasema kuwa, siku hiyo utoaji wa gesi nchini Romania ulipungua kwa asilimia 25, kiasi hicho cha nchini Poland ni asilimia 35, asilimia 40 nchini Slovak na Hungary, na asilimia 50 nchini Serbia. Mhusika wa kampuni ya gesi ya Serbia alisema, nchi hiyo inapaswa kutekeleza utaratibu wa kutoa gesi kwa mgao, na kukidhi kwanza mahitaji ya gesi ya idara muhimu zikiwemo hospitali na shule.
Nchi kadhaa za Ulaya magharibi pia zimekumbwa na upungufu wa gesi. Tarehe 2 Kiasi cha utoaji gesi nchini Austria kilipungua kwa theluthi moja, japokuwa Ujerumani na Italia zina akiba kubwa ya gesi, lakini hali mbaya ya hewa iliyotokea barani Ulaya hivi karibuni imeongeza matumizi ya nishati, hivyo nchi za Ulaya zinapaswa kuyahimiza mashirika yanayotumia nishati kwa wingi yatumie mafuta badala ya gesi, na kuzitaka Russia na Ukraine zichukue hatua mwafaka kupunguza tofauti zao, ili kuhakikisha utulivu wa utoaji wa gesi ya asili, na kuziwezesha nchi za Ulaya ziwe na nishati ya kutosha katika kupambana na baridi.
Mgogoro kati ya Russia na Ukraine kuhusu bei ya gesi umevutia uangalifu mkubwa na tahadhari kubwa za nchi za Ulaya. Asilimia 25 ya gesi ya asili ya nchi za Ulaya magharibi inaagizwa kutoka Russia, na asilimia kubwa ya gesi iliyoagizwa kutoka Russia inasafirishwa kwa kupitia bomba linalopita nchini Ukraine. Ili kukabiliana na athari zitakazoletwa na mgogoro wa gesi kati ya Russia na Ukraine kwa usalama wa nishati wa nchi za Ulaya, kamati ya Umoja wa Ulaya tarehe 4 huko Brussels itafanya mkutano wa kikundi cha kazi cha uratibu wa gesi ya asili, kujadiliana hali itakayoweza kutokea, na kuthibitisha mfumo wa utoaji nishati kwa kipindi kirefu katika soko la Umoja huo. Kamati ya Umoja wa Ulaya ilisema kuwa, hata kama usafirishaji wa gesi kutoka Russia ukisimamishwa, kutokana na kuwepo kwa akiba nyingi na vyanzo vingi vya gesi ya asili, utoaji wa gesi wa nchi za Ulaya katika muda mfupi ujao hautaathirika kwa kiwango kikubwa.
Japokuwa kampuni ya gesi ya Russia imeahidi kuchukua hatua za aina mbalimbali kuhakikisha usafirishaji wa gesi kwa nchi za Ulaya kutokana na mkataba, lakini wasiwasi uliosababishwa na kusimamishwa kwa utoaji wa gesi bado unawasumbua watu wa nchi za Ulaya.
Vyombo vya habari vya nchi za Ulaya vimeona kuwa, kitendo cha Russia cha kusimamisha gesi si kama tu ni mgogoro wa kiuchumi, bali pia ni karata ya kisiasa. Ukraine kufuata sera ya kuzingatia uhusiano na nchi za magharibi, na kuikosoa jumuiya ya madola huru inayoongozwa na Russia, kumeathiri vibaya uhusiano kati yake na Russia. Mwaka huu Russia ni nchi mwenyekiti wa kundi na nchi nane, ikiwa mshirika muhimu wa nishati wa nchi za magharibi, Russia huenda itachukua fursa hiyo kugeuza sifa yake ya nishati kuwa athari ya kisiasa, ili kuimarisha nguvu yake katika mchakato wa kukuza uhusiano kati yake na nchi za magharibi.
Wachambuzi wanaona kuwa, japokuwa kitendo cha kusimamisha gesi cha Russia kimeleta wasiwasi kwa nchi za Ulaya, lakini nchi za Umoja wa Ulaya hazina la kufanya kwa sababu zinaitegemea sana Russia katika sekta ya nishati.
Idhaa ya Kiswahili 2006-01-03
|