Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-01-03 18:37:23    
Mabadiliko ya aina tano yametokea nchini China katika juhudi za kustawisha kilimo

cri

Fedha zilizotengwa katika bajeti ya mwaka 2005 nchini China kwa ajili ya kustawisha kilimo zimeongezeka hadi kufikia yuan bilioni 300, fedha hizo zimehakikisha usalama wa chakula, ongezeko la mapato ya wakulima, na zimeharakisha maendeleo ya vijiji. Wakulima wameridhika kwa kiasi kikubwa kutoka na manufaa waliyoyapata, na hali hiyo ya kuridhika kwa wakulima ni nadra kutokea katika miaka mingi iliyopita. Hayo yamesemwa na waziri wa fedha wa China Bw. Jin Renqing kwenye mkutano wa taifa wa mambo ya fedha uliofanyika tarehe 19 Beijing.

Bw. Jin Renqing alisema, katika juhudi za kustawisha kilimo yametokea mabadiliko ya aina tano kama yafuatayo:

Moja ni kuwa fikra za namna ya kustawisha kilimo zimebadilika. Sera za "kuwanufaisha wakulima kwa wingi, kuwatoza kidogo na kukiacha kilimo kiwe huria" na sera za "viwanda kusaidia kilimo, miji isaidie vijiji" zimekuwa zikitekelezwa.

Pili ni kuwa uwekezaji kwa ajili ya ustawi wa kilimo umebadilika. Uwekezaji wa kilimo umeongezeka kwa kiasi kikubwa zaidi toka serikali kuu hadi serikali za mitaa. Mwaka 2005, serikali kuu imeongeza uwekezaji huo kwa asilimia 50 kuliko mwaka jana.

Tatu, namna za kusaidia maendeleo ya kilimo zimebadilika. Sera za "kupunguza au kusamehe kodi za aina tatu na kutoa ruzuku za aina tatu" zimetungwa na kutekelezwa, kiwango cha kunufaika kwa wakulima kimekuwa kikubwa. Mwaka 2005 mikoa 30 imetoa ruzuku ya kilimo yenye thamani ya yuan bilioni 13.2 na wakulima walionufaika moja kwa moja na ruzuku hiyo wamefikia milioni 642. Zaidi ya hayo, serikali kuu imetenga fedha kwa ajili ya wilaya muhimu zinazozalisha nafaka, kutokana na sera hizo serikali za mitaa zimehamasishwa katika juhudi za kustawisha kilimo.

Nne ni kuwa hatua za kukipiga jeki kilimo zimebadilika. Licha ya hatua za kueneza kilimo cha kitaalamu, kilimo kiwe uzalishaji mkubwa wa kiwanda, kustawisha vijiji kwa viwanda na kujenga misitu ya kuleta mazingira bora, pia zimeanzisha uwekezaji wa hisa, na kwa kutumia sera za ushuru wa forodha kuhamasisha kuingiza njia za uzalishaji wa kilimo kutoka nje, kuunga mkono maendeleo ya mashirika ya wakulima, na ujenzi wa hifadhi ya maji unaoendeshwa na wakulima unasaidiwa na serikali na kupima udongo na kutia mbolea kwa mujibu wa hali ya udongo. Hatua hizo zimesaidia kwa pande zote maendeleo ya kilimo.

Tano ni kuwa, usimamizi wa matumizi ya fedha za kusaidia kilimo umepata mabadiliko. Fedha zilizotumika kwa ajili ya kustawisha kilimo zimeratibiwa na kusimamiwa zaidi, hivyo fedha hizo zimetumika kwa tija kubwa.

Pamoja na yote hayo, mageuzi ya kodi yamewanufaisha zaidi wakulima. Mwaka 2005, mazao ya kilimo yote yamesamehewa ushuru isipokuwa tu ufugaji na tumbaku. Mikoa 28 imesamehe kodi za kilimo, na katika mikoa mingine mitatu iliyobaki wilaya 210 pia zimesamehe kodi za kilimo. Kwa ajili ya kufanikisha kusamehe kodi za kilimo serikali kuu imetoa fedha yuan bilioni 66.4, hili ni ongezeko la asilimia 271 kuliko mwaka 2003, na kimsingi lengo la "kupunguza mzigo, kusawazisha kanuni na kufanya mageuzi kwa hatua ya uthabiti" limepatikana, na wakulima wamenufaika.

Idhaa ya Kiswahili 2006-01-03