Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-01-03 18:40:55    
Wananchi wanufaike kutokana na ongezeko la uchumi

cri

   

Katika mwaka huu, wananchi walinufaika zaidi kutokana na ongezeko la uchumi, wawe wakazi wa mijini au wa sehemu ya vijiji, watu wanaona kuwa pato lao limeongezeka na kiwango cha maisha yao kimeinuka kuliko miaka michache iliyopita.

Kwa mkulima wa Anqing mkoani Anhui Bw. Hong Tiangan eneo la shamba lake lililopandwa mazao ya chakula ni sawa na la mwaka uliopita, lakini pato lake liliongezeka kwa kiasi kikubwa.

"Mwaka 2005, kodi za kilimo zilifutwa katika mkoa wa Anhui, pato letu la kila hekta liliongezeka Yuan karibu 700, mwaka 2005 nilipanda mazao ya chakula katika hekta zaidi ya 80, hivyo pato langu liliongezeka kwa Yuan karibu elfu 50 kutokana na kufutwa kodi za kilimo."

Idadi ya wakulima wa China walionufaika katika mwaka 2005 kama Bw. Hong Tiangan ilifikia milioni 800, na kodi zilizosamehewa zilifikia Yuan bilioni 23.3. Kutokana na maendeleo ya viwanda na sekta ya huduma, fedha zilizokusanywa kutokana na kodi za kilimo zilikuwa chache sana ikilinganishwa na jumla ya fedha zilizokusanywa kutokana na kodi za aina nyingine nchini China, na umuhimu wake kwa pato la taifa ni mdogo sana. Hivyo kuondolewa kodi za kilimo hakutaleta athari kwa pato la taifa, bali kutaweza kuongeza pato la wakulima na kuhimiza matumizi ya sehemu ya vijiji.

Kuondolewa kwa kodi za kilimo kumeongeza juhudi za wakulima, kuhimiza uzalishaji nafaka nchini China na kuongeza pato la wakulima. Inakadiriwa kwamba uzalishaji wa nafaka nchini China kwa mwaka 2005 ungeongezeka kwa kilo bilioni 14 kuliko mwaka uliotangulia, na pato la wakulima pia lingeongezeka kwa udhahiri.

Jambo lililowafurahisha wakazi wa mijini wenye pato la wastani na la chini ni kuinua kiwango cha kutoza kodi ya mapato kuanzia Yuan 1,600 badala kile cha zamani cha mshahara wa Yuan 800 kwa mwezi. Ingawa sera hizo zitatekelezwa rasmi kuanzia mwaka 2006, lakini watu wanaotarajia kupata mshahara wamefurahi sana.

Bibi Chen Yuexiu, ambaye anaishi mkoani Sanxi, sehemu ya kaskazini ya China, anapata mshahara Yuan 1,700 kwa mwezi, anaunga mkono marekebisho ya kodi ya mapato. Alisema kuinuka kwa kiwango cha kodi ni nafuu kwa watu kama yeye anayepata pato dogo. Alimwambia mwandishi wetu wa habari,

"Zaidi ya nusu ya mshahara wangu wa kila mwezi inatumika kulipa mkopo wa nyumba, na fedha zinazobaki ni kidogo sana baada ya kukatwa fedha za matumizi ya simu na mawasiliano. Kuinua kiwango cha kutoza kodi kuanzia Yuan 1,600, baadaye kodi yake ya mapato itakatwa kwa pungufu ya Yuan zaidi ya 80. Ingawa hesabu hiyo ni ndogo, lakini ni nafuu kwake."

Baada ya kuinuka kwa kiwango cha kodi ya mapato, idadi ya watu walionufaika zaidi ni wale wenye pato la wastani na wenye pato dogo. Ofisa husika wa idara kuu ya kodi ya taifa alisema, pato la serikali litapungua kwa Yuan bilioni 28 kwa mwaka, hatua ambayo itapunguza malalamiko ya mzigo mkubwa wa kodi ya watu wenye pato dogo, kuchangia kupunguza tofauti kati ya matajiri na watu maskini na kulinda haki na utulivu wa jamii.

Pamoja na kuongezeka kwa mapato ya wakulima na wakazi wa mijini, maisha yao yataendelea kuboreshwa. Habari zinasema kuwa katika miezi 9 ya mwanzo ya mwaka 2005, ongezeko la fedha za matumizi kwa wakazi wa mijini pamoja na ongezeko la wastani wa pato la mkulima yalikuwa kubwa zaidi kuliko ongezeko la uchumi. Ongezeko la kasi la pato la wakazi wa mijini na sehemu ya vijiji limehamasisha zaidi masoko ya nchini.

Mkulima wa Xuzhou, mkoani Jiangsu, sehemu ya mashariki ya China Bw. Qie Jijun ingawa anaishi kijijini, umbali wa kilomita makumi kadhaa kutoka mjini, lakini kwenda kununua bidhaa supamaketi kumekuwa mazoea yake na wanakijiji wenzake katika mwaka 2005. Hivi karibuni alinunua kiyoyozi kwenye supamaketi moja ya karibu, akitaka kuongeza ujoto nyumbani katika majira ya baridi.

"Hapa kuna bidhaa za aina mbalimbali, tunapenda kununua vitu kutoka supamaketi, mazingira ya hapa ni mazuri, tunataka kununua bidhaa zenye chapa nzuri na zinazotangazwa sana katika matango ya biashara."

Kutokana na kukuzwa kwa uwezo wa wakulima wa kununua bidhaa mbalimbali, supamaketi ya aina hiyo haijajengwa katika miji peke yake. Hivi sasa sehemu za vijiji nchini China zimekuwa na supamaketi zaidi ya elfu 70, na wakulima wamekuwa na chaguo kubwa zaidi wakati wa kununua bidhaa.

Takwimu zinaonesha kuwa katika miezi kumi ya mwanzo ya mwaka 2005, jumla ya thamani ya biashara ya rejareja nchini China ilifikia Yuan bilioni 5,100, ikiwa ni ongezeko la 13% kuliko mwaka uliotangulia, na ni ongezeko la karibu 4% ikilinganishwa na kasi ya ongezeko la uchumi. Aidha, pato la sekta ya huduma ukiwemo utalii na migahawa limeongezeka kwa kiwango kikubwa kuliko mwaka uliotangulia.

Ni dhahiri kuwa ongezeko la pato la watu wa China katika mwaka 2005 na kuinuka kwa kiwango cha maisha kulitokana na maendeleo mwafaka wa uchumi wa China. Mtaalamu wa idara ya utafiti wa uchumi ya chuo cha sayansi ya jamii ya China Bw. Yuan Gangming alipotathmini hali ya uchumi ya Chika ya mwaka 2005, alisema, "Hali ya uchumi ya mwaka 2005 ni nzuri, uwiano kati ya kasi ya ongezeko la pato la taifa na bei za vitu ni mzuri, kasi ya ongezeko la pato la taifa ni 9.5%, lakini mfumuko wa bei bado ni 2% hivi, uwiano wa namna hiyo ni nadra kutokea, katika mwaka 2004 pato la taifa liliongezeka kwa kasi, lakini bei za vitu pia zilipanda kwa kiwango cha juu. Hivi sasa bei za vitu zimepungua, lakini ongezeko la pato la taifa bado ni kubwa, hivyo ninasema, hali ya uchumi ya mwaka 2005 ni nzuri zaidi katika miaka mitatu iliyopita."

Bw. Yuan Gangmin alichambua kuwa kwa kawaida ongezeko kubwa la uchumi linaleta mfumuko wa bei za vitu, ongezeko la uchumi lililotokea katika kipindi cha kati cha miaka ya 90 lilileta mfumuko wa bei za vitu, ambao ulizidi 10%. Katika raundi nyingine ya maongezeko ya uchumi lililoanza mwaka 2003, bei za vitu zilipanda kwa kiwango kidogo. China ilijifunza kutokana na mafunzo yaliyotokea hapo nyuma, ilichukua hatua kwa wakati ya kudhibiti kwa mpango mkuu wa taifa, hivyo kupanda kwa bei za vitu nchini China mwaka 2005 ulikuwa kiasi cha 2% tu. Ikilinganishwa na ongezeko la uchumi la zaidi ya 9%, watu wa China wamenufaika kutokana na ongezeko la uchumi, wakati upandaji bei za vitu wa kiwango cha chini unafanya fedha za mfukoni mwa watu wa China kuwa na thamani zaidi.

Hata hivyo maofisa na wataalamu wa uchumi wa China wanaona matatizo mengi yaliyoko katika maendeleo ya uchumi wa China mwaka 2005, ambayo hususan ni upungufu wa raslimali na uchafuzi mkubwa kwa mazingira ya asili. Serikali ya China imesema, licha ya kudumisha maendeleo ya uchumi na kufanya watu wa China wanufaike kutokana na ongezeko la uchumi, itajitahidi kupunguza hatari inayoletwa na maendeleo ya uchumi kwa shughuli zao za uzalishaji mali na maisha yao.

Idhaa ya Kiswahili 2006-01-03