Wakati ambapo watu wa nchi mbalimbali walipokuwa wakisherehekea sikukuu ya mwaka mpya maafa mengi yalitokea mfululizo katika nchi za Ujerumani, Indonesia, Marekani na Australi, na kusababisha vifo vya watu wengi na hasara kubwa. Maafa hayo yanawatahadharisha na kuwakumbusha wanadamu kuwa wakitaka kuishi katika dunia hii, lazima wahifadhi mazingira na kuishi kwa kupatana na maumbile, vinginevyo matokeo yatakuwa mabaya.
Jumba la mchezo wa kuteleza kwenye barafu nchini Ujerumani tarehe pili liliporomoka na kusababisha watu kumi na wawili kupoteza maisha, watu wengi walisema, chanzo cha mporomoko huo ni uzito wa theluji nyingi. Mafuriko makubwa yalitokea tarehe pili nchini Indonesia na kusababisha vifo vya watu 60 na wengine kumi kadhaa kujeruhiwa. Serikali ya Indonesia ilitangaza kuwa kutokana na kukatwa miti mingi ovyo, vijiji vinne kwenye mteremko wa mlima viliathirika vibaya. Baada ya ukame uliodumu kwa muda mrefu, moto ulitokea katika majimbo kadhaa ya kusini ya Marekani, na mafuriko makubwa yalitokea kutokana na mvua nyingi katika baadhi ya sehemu jimboni Califonia. Kadhalika, katika siku za Krismasi na mwaka mpya, moto mkubwa ulitokea katika majimbo mengi nchini Australia, baadhi ya majumba yaliteketea na watu wa familia elfu kadhaa waliathirika.
Ingawa maafa hayo yalitokea kwa bahati mbaya tu kwa kiasi fulani, lakini pia yanaonesha kuwa uharibifu wa mazingira uliofanywa na binadamu umekuwa mkubwa, kwa hiyo hifadhi ya mazingira imekuwa kazi ya haraka na ya lazima kwa binadamu. Taarifa iliyotolewa na Shirika la Maumbile Duniani mwishoni mwa mwaka jana ilisema kwamba mwaka 2005 ulikuwa ni mwaka wenye joto zaidi, ukame na kimbunga vilikuwa juu katika historia ya rekodi ya hali ya hewa. Kwa makadirio ya mwanzo, hasara zilizosababishwa na maafa ya kimaumbile kwa mwaka jana zilifikia dola za Marekani bilioni 200, na hasara ya bima zilikuwa zaidi ya dola za Marekani bilioni 70, na kiasi cha hasara hizo mbili hakijawahi kutokea katika miaka yote iliyopita.
Uharibifu wa mzingira unawaletea madhara gani makubwa binadamu?
Kwanza, ongezeko la joto duniani na maafa ya kimaumbile yatakuwa mengi na makubwa zaidi, licha ya tsunami iliyotokea mwishoni mwa mwaka jana nchini Indonesia, watu walikumbwa na maafa makubwa yaliyosababishwa na kimbunga cha bahari ya Atlantiki na matetemeko ya ardhi yaliyotokea Asia ya Kusini.
Pili, mabadiliko ya mazingira kwenye ardhi ya dunia, mabadiliko hayo yamebadilisha mazingira yanayofaa kuishi kwa wanyama na mimea. Kutokana na ongezeko la joto sehemu ya kaskazini ya eneo ya barafu limebadilika kuwa ndogo, na ukame mkubwa ulitokea katika historia kwenye Msitu wa Mvua wa Amazon, mazingira ya kuishi kwa wanyamapori na mimea yaliharibika vibaya, na uharibifu huo wa mazingira mwishowe utahatarisha maisha ya binadamu.
Tatu, magonjwa mengi yametokea na kuhatarisha afya ya binadamu. Wanasayansi wamesema kwamba UKIMWI, homa ya Ebola na Dengue, yote ni magonjwa yaliyotokea tu katika kipindi cha miaka 30 iliyopita na kutokana na ongezeko la joto duniani, uharibifu wa mazingira na shughuli mbaya za binadamu, magonjwa yasiyopungua aina 30 yatatokea katika kipindi cha miaka 30 ijayo. Isitoshe, kutokana na uharibifu wa mazingira, magonjwa ya zamani ambayo yaliyodhibitiwa yatafufuka na kuenea tena. Katika miaka ya karibuni, magonjwa yaliyofufuka ya malaria, homa ya Dengue, uvimbe wa ubongo na kichocho ni onyo kutokana na uharibifu wa mazingira.
Wanasayansi wanaonya kuwa binadamu wakitaka kuishi katika dunia hii, wanapaswa kubadilisha shughuli zao, kwa mfano, kupunguza matumizi ya makaa ya mawe, mafuta na gesi na kuongeza matumizi ya nishati ya upepo, maji na joto la ardhini, kupunguza ukataji wa miti na hasa kuhifadhi misitu ya tropiki na uenezi wa miji utilie mkazo mazingira ya kuishi. Hivi sasa watu wametambua kwamba mabadiliko ya hali ya hewa duniani ni changamoto kubwa na ya muda mrefu kwa binadamu, na lazima wabadilishe njia yao ya kuishi na nchi zilizoendelea ambazo zimefurahia maisha ya starehe kwa kuharibu mazingira, lazima ziwajibike kwa vitendo halisi.
Idhaa ya kiswahili 2006-01-04
|