Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-01-04 20:27:53    
Wakulima wanaofanya kazi za vibarua mijini waelimishwa zaidi kuhusu ujuzi wa ugonjwa wa Ukimwi nchini China

cri

Tangu virusi vya ugonjwa wa Ukimwi vigunduliwe mwaka 1981 mpaka sasa, kwa miaka zaidi ya 20, ugonjwa huo umekuwa tishio kubwa kwa afya ya binadamu, ili kutafuta njia za kutibu ugonjwa huo, wanasayansi wa nchi mbalimbali wamefanya utafiti bila kulegea. Lakini mpaka sasa, bado haijapatikana njia mwafaka ya kutibu ugonjwa huo, na katika mwaka 2005, watu milioni 3.1 wamekufa kutokana na ugonjwa huo.

Kutokana na hali hiyo, kueneza ujuzi kuhusu kinga dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi na kuinua tahadhari ya umma kuhusu ugonjwa huo kumekuwa njia muhimu ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo. China pia inatilia maanani kazi hiyo.

Katika siku za karibuni, shughuli moja ya kueneza ujuzi kuhusu ugonjwa wa Ukimwi kwa wakulima wanaofanya kazi za vibarua mijini ilifanyika kwenye uwanja wa kituo cha garimoshi cha Beijing ya Magharibi na kuwavutia watu wengi. Wataalamu zaidi ya 20 wa Ukimwi walikuwa wanajibu maswali ya papo hapo, na watu wanaojitolea walikuwa wakisambaza hojaji na vijitabu vinavyohusu kujikinga dhidi ya maambukizi ya Ukimwi. Aidha, vibao zaidi ya mia moja vya maonesho ya kinga na tiba ya Ukimwi vimeweka huko.

Mkulima mmoja aliyekuwa ameshuka kwenye garimoshi muda mfupi uliopita aliweka chini mizigo yake na kujaza kwa makini hojaji aliyopewa. Mwandishi wetu wa habari alizumgumza naye,

"unatoka wapi?"

"Natoka mji wa Shangqiu mkoani Henan."

"Umekuja hapa kwa sababu gani?"

"nimekuja kufanya kazi za kibarua."

"Unajua nini kuhusu kinga na tiba ya ugonjwa wa Ukimwi?"

"Najua kidogo tu kutokana na matangazo ya radio na televisheni. Nina bahati sana kuona maonesho haya."

Hali ya mkulima huyo ni ya kawaida nchini China. Hivi sasa, wakulima milioni 120 wanaingia mijini kufanya kazi za vibarua, viwango vyao vya elimu ni vya chini na hawajui namna ya kujikinga na ugonjwa wa Ukimwi. Asilimia 65 ya watu hao ni vijiana wenye umri wa miaka 20 hadi 40, na wengi wao hawajafunga ndoa. Baada ya kuingia mijini kutoka vijijini, kutokana na kukabiliwa na mazingira tofauti na mahitaji ya kihisia na ya mwili, mtizamo wao juu ya mapenzi umebadilika sana. Aidha kutokana na kuwa watu hao wanahama mara kwa mara, hivyo kama wakiambukizwa virusi vya Ukimwi, wanaweza kueneza virusi vya Ukimwi.

Kutokana na hali hiyo, China imeweka mkazo katika kueneza ujuzi kuhusu kinga na tiba ya ugonjwa wa Ukimwi kwa wakulima wanaofanya kazi za vibarua mijini, na idara husika za serikali na jumuiya mbalimbali za kiraia zote zinafanya shughuli nyingi kwa nyakati tofauti. Mbali na kufanya maonesho kwenye kituo cha garimoshi, China pia imeanza kufanya shughuli kama hizo kwenye vyombo vya mawasiliano.

Kati ya vyombo mbalimbali vya mawasiliano, garimoshi ni chaguo la kwanza kwa wakulima wanaoingia mijini kufanya kazi ya kibarua. Hivyo, imetiliwa maanani kueneza ujuzi kuhusu Ukimwi kwenye garimoshi. Hivi karibuni kwenye garimoshi moja lililokuwa linakwenda mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani kutoka Beijing, watu wanaojitolea wa jumuiya ya msalaba mwekundu walisambaza vijitabu kwa abiria, na abiria wote wakaanza kusoma kwa makini. Mwandishi wetu alimhoji msafiri mmoja kutoka Hispania. Alisema:

"Nchini kwetu, pia kuna shughuli kama hizo. Nadhani hii ni shughuli nzuri na maalum. Na watu wengi watanufaika kutokana na shughuli hiyo."

Shughuli kama hiyo inafanyika kwenye magarimoshi yote ya njia kuu nchini China. Naibu mkurugenzi wa jumuiya ya msalaba mwekundu ya China Bi. Jiang Yiman alisema:

"tunaona kuwa watu wanaohamahama mara kwa mara wanapaswa kuzingatiwa katika shughuli za kuzuia maambukizi ya Ukimwi. Kwa kupitia majaribio hayo, tutapata uzoefu na baadaye tukapanua shughuli hizi hatua kwa hatua."

Mbali na shughuli hizo, idara husika zikiwemo wizara ya afya ya China pia zimeanza kueneza ujuzi wa Ukimwi vijijini, kubandika mabango yenye picha na maelezo kuhusu kinga na tiba ya Ukimwi katika kila kijiji kote nchini ili kuwapatia zaidi wakulima na jamaa zao ujuzi zaidi kuhusu Ukimwi; kwenye sehemu za ujenzi ambazo wakulima wengi wanafanya kazi, idara husika pia zinaonesha filamu za maelezo ya ugonjwa huo na kutoa bure vifaa vya kujikinga dhidi ya Ukimwi. Mkulima mmoja Bw. Sun Yue anayefanya kazi za vibarua mjini Beijing alisema:

"wakati tunapoingia mijini na kuzoea maisha ya mijini, ni lazima tujidhibiti na tusifanye mapenzi ovyo vvyo, ili tusije tukaharibu maisha na familia yetu."

Hivi karibuni, serikali ya China imeanzisha mradi mmoja wa kutoa mafunzo kuhusu ugonjwa wa Ukimwi kwa wakulima wanaofanya kazi za vibarua mijini kote nchini China. Shughuli za mradi huo ni kuhusu kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2010, kumpa kila mkulima anayefanya kazi za kibarua mijini kijitabu kimoja kuhusu kinga na tiba ya ugonjwa wa Ukimwi na kondomu mbili wakati anaporudi kijijini; idara husika za kilimo na ujenzi zitaweka ujuzi kuhusu Ukimwi kwenye kitabu cha mafunzo ya kazi za vibarua kwa wakulima, idara za kazi na huduma za jamii zitakapotoa mafunzo kwa wakulima, lazima ziongeze vipindi visivyopungua viwili vya elimu kuhusu kinga na tiba ya Ukimwi. Serikali ya China inalenga kuwaelimisha zaidi asilimia 65 ya wakulima wanaofanya kazi za vibarua mijini kuhusu Ukimwi ifikapo mwishoni mwa mwaka 2006, na kiasi hicho kufikia asilimia 85 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2010.