Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-01-05 16:31:52    
Mtandao wa Internet wakidhi mahitaji ya Wachina ya kusoma habari na kujiburudisha

cri

 

 

 

 

 

Kutokana na maendeleo ya kasi ya sayansi na teknolojia, watu wengi zaidi nchini China wanapenda kusoma habari, kutafuta data kutoka kwenye mtandao wa Internet, ambao umekidhi mahitaji ya Wachina ya kusoma habari, na kusikiliza muziki, hata kutazama filamu kwenye mtandao wakati wa mapumziko.

Muda si mrefu uliopita, mwandishi wetu wa habari alifanya uchunguzi kwenye mtaa wa Beijing, ambapo asilimia 90 ya watu waliohojiwa walisema waliwahi kusoma habari kwenye mtandao wa Internet, na asilimia 40 kati yao walisema, mtandao wa Internet umekuwa njia muhimu kwao kupata habari. Bwana Zhang alisema:

"Hivi sasa ni nadra kwangu kununua magazeti, mimi huwa nasoma habari kwenye tovuti za aina mbalimbali za Internet, kama vile tovuti ya Sohu, Xinhua, na CCTV."

Bi. Xu Li alisema:

"Mimi huwa nasoma habari za kisiasa za nchini China na za kimataifa kwenye mtandao wa internet, pia napenda kusoma habari za burudani."

Takwimu zilizotolewa hivi karibuni na kituo cha habari cha mtandao wa Internet cha China zinaonesha kuwa, hivi sasa idadi ya kompyuta zilizounganishwa na Internet nchini China imezidi milioni 100, ambapo nusu yake zinatumiwa kukusanya habari. Si kama tu wakazi wengi wa kawaida wamekuwa wasomaji wa tovuti za Internet, viongozi wa ngazi ya juu pia wameanza kufuatilia nguvu hiyo mpya ya mtandao wa Internet. Kabla ya miaka miwili iliyopita, rais Hu Jintao wa China aliwahi kufahamishwa mapendekezo yaliyotolewa na madaktari kuhusu jinsi ya kupambana na ugonjwa wa SARS kwa kupitia mtandao wa Internet, waziri mkuu Wen Jiabao alipata maoni ya wanafunzi wa vyuo vikuu baada ya kusoma ujumbe ulioandikwa na wanafunzi hao kwenye mtandao wa Internet.

Ili kukidhi mahitaji ya watumiaji wa mtandao wa Internet, vyombo vikuu vya habari vya jadi vya China ambavyo ni pamoja na shirika la habari la Xinhua, gazeti la Renminribao, na kituo cha televisheni CCTV vimetilia maanani sana kuweka habari mpya kwenye tovuti zao za Internet. Mhariri mkuu wa tovuti ya CRI online ya Radio China Kimataifa Bwana Ma Weigong alipozungumzia kwa nini watu wanapenda namna hii mtandao wa Internet alisema:

"Wasikilizaji wa radio na watazamaji wa televisheni wanapaswa kusikiliza au kutazama vipindi wapendavyo kwa kufuata ratiba iliyowekwa, lakini watumiaji wa mtandao wa Internet wana nafasi kubwa ya chaguo, wanaweza kusikiliza au kutazama wakati wowote."

Umaalum wa mtandao wa Internet wa kuwasiliana na watumiaji mtandao pia umewavutia watu wengi sana. Watumiaji mtandao wanaweza kueleza kwa uhuru maoni yao kuhusu mambo yanayofuatiliwa na jamii, na maoni yao yatawasaidia viongozi wa serikali kutunga sera.

Zaidi ya hayo, watumiaji wa mtandao pia wanaweza kuanzisha safu yao wenyewe katika sehemu zilizotolewa na tovuti mbalimbali za Internet, wanaweza kuandika makala yenye umaalum wa kipekee na kuyaweka kwenye safu yao. Bi. Sun alisema:

"Hivi karibuni, nilikwenda katika mikoa ya Shanxi na Mongolia ya ndani pembezoni mwa ukuta mkuu kuwasaidia wakazi wa vijijini kupiga picha, safari hii nimeona kwa macho yangu mwenyewe jinsi wanavijiji wa huko wanavyofanya kazi na kuishi. Baada ya kurudi mjini Beijing, niliandika makala na kuiweka kwenye safu yangu ili kuwafahamisha marafiki ambao hawakuweza kusafiri pamoja nami, mambo niliyoyaona na niliyosikia."

Hivi sasa China ina watumiaji wa safu karibu milioni 10, na wengi wao ni makarani kama Bi. Sun au wanafunzi wa vyuo vikuu. Wakati mwingi watu hao hukaa ofisini au mabwenini wakifanya kazi au kujifunza mambo mbalimbali kwenye kompyuta. Kuandika makala na kusoma yaliyoandikwa kwenye safu zilizoko mtandao wa internet ni njia moja ya kujipumzisha baada ya kazi nyingi. Mhariri mkuu wa tovuti ya Sina inayojulikana sana nchini China Bwana Chen Tong alisema, hivi sasa baadhi ya watu mashuhuri pia wameanzisha safu zao kwenye tovuti za Internet. Akisema:

"Nadharia ya safu kwenye mtandao wa Internet imeanza kujulikana sana nchini China, hivi sasa watu zaidi ya milioni moja wakiwemo watu mashuhuri wameanzisha safu zao kwenye tovuti ya Sina."

Kutokana na maendeleo ya teknolojia mpya, licha ya maandishi yaliyowekwa kwenye mtandao wa Internet, vipindi vya sauti au picha pia vimeanza kutolewa kwenye mtandao wa Internet. Kwa mfano muda si mrefu uliopita, kituo cha Radio China Kimataifa kimeanzisha radio kwenye mtandao, ambapo kituo cha televisheni cha China CCTV kimeanzisha televisheni kwenye mtandao.

Wakati huo huo vipindi vya sauti na picha vinavyotengenezwa na watumiaji mtandao pia vinakaribishwa sana, vipindi hivyo vinaitwa "Podcast". Watengenezaji wa Podcast wanaeleza maoni yao au kusimulia hadithi kwa kutumia sauti, picha hata katuni. Bwana Gaofeng ni mmoja kati ya watu hao, yeye anapenda kucheza gitaa, hutengeneza vipindi vya muziki wa gitaa na kuviweka kwenye mtandao ili kuwaburudisha wengine. akisema:

"Nimefanya hivyo kwa muda mrefu, hiyo ni kazi rahisi."

Kwa kweli, mtandao wa Internet umeongeza sana burudani kwa Wachina, ambazo zinatofautiana na burudani za zamani.

Idhaa ya kiswahili 2005-01-05