Waziri mkuu wa Israel aliyesifiwa kuwa ni "tingatinga" katika ulingo wa siasa, Bw. Sharon amelazwa hospitali na kupoteza fahamu, wakati watu wa Israel wanapomwombea dua apone, wanaona kuwa maisha yake ya kisiasa yamefikia mwisho.
Bw. Sharon ambaye alikuwa mkulima, askari na jemadari anazungumzwa sana kwa maoni tofauti. Akiwa askari alishinda vita vingi kati ya Israel na nchi za Kiarabu na kusifiwa kuwa ni "mfalme wa Israel". Katika vita vya nne vya Mashariki ya Kati mwaka 1973, Bw. Sharon aliongoza jeshi lake kuvuka mto wa Suez na kusambaratisha vibaya jeshi la Misri, akageuza hali mbaya ya Israel katika vita. Lakini machoni mwa Waarabu wengi Bw. Sharon ni "mchinjaji" anayependa vita. Katika vita vya Lebanon mwaka 1982 Wapalestina 1500 waliuawa, Bw. Sharon hawezi kukwepa hatia hiyo. Mwaka 2000 Sharon aliingia kwa nguvu kwenye sehemu ya mlima wa hekalu na kusababisha mgogoro wa umwagaji damu uliodumu kwa miaka zaidi ya minne kati ya Palestina na Israel, watu wa Palestina elfu kadhaa wamepoteza maisha.
Akiwa mwanasiasa, baadhi ya watu wanasema kwamba Bw. Sharon ni "tingatinga" linalosonga mbele kijasiri na halitasimama bila kufikia lengo lake, lakini baadhi ya watu wanasema, yeye ni "dikteta" asiyekuwa na msimamo maalumu, leo hivi kesho vile. Miaka thelathini iliyopita, alipokuwa waziri wa makazi, kwa moyo wa "tingatinga" alipanua eneo la nchi yake na kujenga makazi katika sehemu ya Palestina, hivyo alijipatia jina la "baba wa makazi". Miongo kadhaa imepita sasa, "tingatinga" hilo kwa kutumia uwezo wote wa kisiasa alipita taa nyekundu moja baada ya nyingine bila kujali hatari na alifyeka makazi yote 21 ya Wayahudi, alishutumwa wa watu wa mrengo wa kulia kuwa ni "mhaini".
Bw. Sharon ni mkaidi, alijulikana kwa kukataa amri ya kijeshi alipokuwa jeshini. Lakini mkaidi huyo aliyekuwa kama mwewe alipokuwa uzeeni alijichomeka mabawa ya "njiwa", kwamba sio tu aling'ang'ania kukabidhi ardhi aliyonyakua kwa Palestina bali aliendelea kutimiza lengo lake la kisiasa kwa kujihatarisha kwa kuachana na marafiki zake wa miaka mingi wa mrengo wa kulia na kuunda chama kipya ili kubakiza nyayo zake katika kipindi chake kipya cha utawala.
Mabadiliko ya kisiasa ya Bw. Sharon alipokuwa uzeeni yalileta uwezekano wa kubadilisha uhusiano uliokuwa mbaya kati ya Palestina na Israel, alitetea kutekeleza mpango wake wa upande mmoja na jumuyia ya kimataifa inaona kuwa mabadiliko hayo ni fursa nzuri kuanzisha tena mchakato wa amani, na Sharon anaonekana kuwa ni kiongozi wa Israel anayeweza kufikia mkataba wa amani na Palestina. Lakini mkakati wa Sharon kuhusu uhusiano kati ya Palestina na Israel unazungumzwa kwa maoni tofauti, kwamba watu wa Palestina wanaona kuwa kuondoka kwa Israel kutoka sehemu ya Gaza ni ujanja wa Sharon kula hasara ndogo ili kupata faida kubwa.
Kwa kuwa na ugumu na ulaini, nia thabiti inayoambatana na hali ilivyo, Bw. Sharon aliweza kudumisha maisha yake ya kisiasa katika mazingira ya kisiasa yaliyobadilika badilika. Watu wa Israel wanaona kuwa ushawishi wa Bw. Sharon ni mkubwa ambao unaweza kulingana na wa waziri mku wa kwanza wa Israel Bw. David Ben-Gurion. Tokea mwaka 2001 Bw. Sharon alipokuwa waziri mkuu wa Israel, amekuwa kiini cha ulingo wa siasa, na hali ya utulivu imetokea katika Israel yenye hali ya utatanishi. Sasa "tingatinga" hilo lilimezimika ghafla, hakika litaacha nafasi tupu kwenye ulingo wa siasa wa Israel.
Idhaa ya kiswahili 2006-01-06
|