Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-01-09 14:37:33    
Mwongozaji wa Filamu Bi.Ma Liwen

cri

Bi. Ma Liwen ana umri wa miaka 34, anaonekana amekomaa zaidi kuliko umri wake. Jinsi anavyojitosa katika juhudi za kutengeneza filamu, inajulikana katika nyanja ya filamu. Katika muda wa miaka mitano alimaliza kutengeneza filamu mbili ambazo hazikutumia fedha nyingi, moja ni "Mtu Aliyenipenda Sana Amefariki", nyingine ni "Sisi Wawili". Filamu hizo mbili zote zimepata tuzo nchini China na nchi za nje. Kwa mwongozaji asiyekuwa na uzoefu wa miaka mingi, si raisi kupata mafanikio kama hayo. Bi. Ma Wenli alisema,

"Filamu hizi mbili hazikunitia hasara, na zinasifiwa. Naona nimefanikiwa."

Mwaka 2001 Ma Liwen alimaliza kutengeneza filamu "Mtu Aliyenipenda Sana Amefariki". Filamu hiyo imetengenezwa kwa mujibu wa riwaya yenye jina hilo iliyoandikwa na mwandishi wa kike Zhang Jie, inaeleza kwamba mwandishi mmoja wa kike aliyefanikiwa katika juhudi zake alirudi nyumbani kumwangalia mama yake mwenye umri wa miaka zaidi ya themanini, akakuta mama yake kazeeka sana. Daktari alimwambia kwamba mama yake ana ugonjwa wa kupooza ubongo, anahitajika kufanya mazoezi mepesi. Mwandishi alijitahidi kumhamasisha mama yake afanye mazoezi, lakini siku moja asubuhi alikuta mama yake amekufa kwenye mashine ya mazoezi. Hii ni filamu inayosisimua sana, mapenzi kati ya mama na binti yaliyoelezwa kwa kina, yanalingana na maisha ya kawaida ya kila siku. Filamu hiyo imepata tuzo za aina tatu za hadithi, uongozaji na waigizaji mwaka 2002 nchini China.

Bi. Ma Liwen alizaliwa katika sehemu ya kusini ya China, katika miaka ya tisini alihamia Beijing na kujiendeleza katika Chuo Kikuu cha Tamthilia na Opera. Ili apate nyumba ya kupanga alipanda baiskeli kuzunguka akiuliza uliza, mwishowe alipanga nyumba moja ya mjane mmoja mzee. Wakati alipokuwa anaishi na mzee huyo zilitokea hadithi nyingi. Mwaka jana Bi. Ma Liwen alisikia kwamba mzee huyo aliaga dunia, kumbukumbu nyingi zilizomsikitisha zilimjia akilini. Alitumia mambo yaliyokuwa kati yake na mzee huyo kutengeneza kuwa filamu "Sisi Wawili".

Filamu "Sisi Wawili" inaeleza kwamba bibi mmoja mzee mjane aliyeishi peke yake siku moja alijiwa na mwanafunzi mmoja msichana aliyetaka kupanga nyumba yake moja ndogo, tokea hapo maisha ya mzee huyo yalibadilika. Mwanzoni hao wawili mara kwa mara walizozana kutokana na mambo madogo madogo, na siku moja mwanafunzi huyo alihama, wakati huo mzee aliona kama amekosewa na kitu. Baadaye mjukuu wake wa kike alitumia ile nyumba na mzee alihamia kwenye maskani yake kijijini, muda mfupi baadaye mzee huyo alifariki akimwachia mwanafunzi msichana huyo majonzi mengi. Siku chache zilizopita, filamu hiyo ilipata tuzo za uongozaji na mwigizaji wa kike.

Bi. Ma Liwen alisema, filamu "Sisi Wawili" ilitengenezwa kwa mujibu wa mambo ya kweli yaliyotokea maishani mwake. Alisema, "Mambo yaliyoelezwa kwenye filamu, yote ni yangu niliyopata, nilitumia majira yote manne ya mwaka kutengeneza filamu hiyo. Ni filamu inayonielezea mimi mwenyewe."

Filamu hiyo ilipooneshwa nchini Japan watazamaji walivutiwa na filamu yenyewe, mara walicheka na mara walihuzunika. Hisia za binadamu hazina mipaka ya nchi.

Bi. Ma Liwen alisema, kila alipotaka kutengeneza filamu alikuwa anakumbwa na matatizo mengi lakini hakurudi nyuma kutokana na nia yake thabiti. Alianza kuanda filamu yake ya kwanza mwaka 1996 na alipomaliza ilikuwa mwaka 2000. Katika muda huo matatizo yaliyompata hatayasahau. Bi. Ma Liwen hakuwa mhetimu rasmi wa chuo kikuu na hakujulikana kutokana na kutengeneza filamu nyingi. Kwa hiyo kupata uwekezaji kwake ilikuwa ni shida. Bi. Ma Liwen alisema, "Mwanzoni, ilikuwa shida sana kukusanya fedha ili nimudu kutengeneza filamu, ingawa filamu yangu ya kwanza haikuhitaji fedha nyingi lakini nilitumia miaka kadhaa kukusanya fedha. Hali hiyo ni kawaida kuwepo kabla watu hawajanifahamu na kuwa na imani nami."

Ili kutengeneza filamu, Bi. Ma Liwen alikumbwa na matatizo mengi, mpaka sasa bado ni mseja. Mara nyingi alivutiwa na wanawake waliolewa wakifurahia maisha yao ya mume na watoto, lakini anashindwa kuacha juhudi zake. Yeye hatilii maanani sifa na umaarufu bali anachukulia juhudi zake kama ni safari ya maisha yake.

Idhaa ya kiswahili 2006-01-09