Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-01-09 20:14:57    
Marekani inabidi kurekebisha sera zake kuhusu mashariki ya kati

cri

Marekani imekuwa kimya kuhusu hali ya waziri mkuu wa Israel Bw Ariel Sharon kuwa mgonjwa mahututi. Lakini kuna baadhi ya maofisa wa Israel na Marekani, ambao wanaona kuwa kuna uwezekano mdogo sana kwa Bw. Sharon kurejea utawala wa nchi hiyo, na serikali ya Bush haina budi kurekebisha sera zake kuhusu mashariki ya kati.

Katika siku za karibuni serikali ya Marekani ilionesha kuwa na wasiwasi kutokana na habari kuhusu hali mbaya ya ugonjwa wa Bw Ariel Sharon, na ilionesha wasiwasi wake mkubwa kutonana na uwezekano wa kupotelewa na Bw Sharon. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi Condoleezza Rice alifuta ziara yake katika Indonesia na Australia ili abaki mjini Washington kufuatilia hali ya ugonjwa wa Bw Sharon pamoja na uwezekano wa kutokea mgogoro katika mashariki ya kati. Mbali na hayo Bi Rice alimtumia ujumbe kaimu waziri mkuu wa Israel Bw. Ehud Ommert kueleza msimamo wa Marekani wa kuendelea kuiunga mkono Israel. Aidha mratibu wa Marekani kuhusu mambo ya usalama wa mashariki ya kati meja Jenerali Keith Dayton amerudi nchini Israel kuwa na mazungumzo kuhusu hali ya hivi sasa ya Palestina na Israel pamoja na maofisa wa nchi hizo mbili. Naye Rais George Bush alipomzungumzia Bw Sharon alimsifu kuwa ni mtu mwenye ujasiri na kuleta amani, na alimwombea apone haraka.

Wachambuzi wanasema kuwa, serikali ya Bush inaona kuwa kufariki dunia kwa Arafat kuliondoa kikwazo cha kufikiwa amani kati ya Palestina na Israel; Sharon aliweza kuongoza watu wa Israel kufanya usuluhisho; Rais Bush anatoa uungaji mkono kwa viongozi wa Israel na Palestina na kuhimiza pande hizo mbili kuelekea kwenye amani. Serikali ya Bush karibu iliweka matumaini yote ya amani juu ya Sharon. Hivi sasa nguzo hiyo inaelekea kuanguka, hali ambayo inaleta mabadiliko kwa sera za Marekani kuhusu mashariki ya kati.

Kwanza, Bw. Bush amepoteza mshirika wa kubuni sera husika. Bw. Sharon alichaguliwa kuwa waziri mkuu wa Israel siku 17 baada ya Bush aapishwe kuwa rais wa Marekani. Bw Sharon ni mtu asiyeweza kujenga urafiki na watu kwa urahisi, laini alikuwa na uhusiano binafsi na Bw Bush. Watu wanaona kuwa sera nyingi za Bush kuhusu mashariki ya kati zilitokana na mawazo ya Bw Sharon.

Lengo la shughuli za kidiplomasia alilotoa Bush, ni kuanzisha nchi ya Palestina na kuleta uhusiano wa amani kati ya Palestina na Israel kabla ya kumalizika kwa kipindi chake cha pili. Rais Bush aliwahi kusema wazi kuziunga mkono Palestina na Israeli kutimiza mpango wa ramani ya amani, akitaka pande mbili za Palestina na Israel zitekeleze majukumu na wajibu wao ili kuleta amani hatua kwa hatua. Wachambuzi wamesema kitu anachounga mkono Bw Bush ni mpango wa upande mmoja wa Sharon.

Pili, pindi Sharon akitoka madarakani, utatokea uwazi kwa muda katika utawala wa Israel, na itakuwa ni vigumu kwa mchakato wa amani ya mashariki kupata maendeleo baada ya uchaguzi mkuu utakaofanyika nchini Israel katika mwezi Machi mwaka huu. Wakati huo huo, mgongano wa wenyewe kwa wenyewe nchini Palestina pia utakuwa mkali zaidi.

Tatu hakuna mtu anayeweza kumbadili Bw Sharon. Baada ya Sharon kuwa mgonjwa mahututi, naibu waziri mkuu wa Israel Bw. Ehud Olmert alikaimu uwaziri mkuu wa nchi hiyo. Lakini baadhi ya vyombo vya habari na wachunguzi wanasema, uwezo wa uongozi wa Olmert ni mdogo ikilinganishwa na uwezo wa Bw Sharon. Hivyo katika muda mfupi ujao, ni vigumu kwa Bw Bush kupata mtu mwingine anayefaa kujaza nafasi aliyoiacha Sharon, ambaye kwa upande mmoja anaweza kupambana vikali na vyama vyenye siasa kali vya Palestina, na kwa upande mwingine anaonekana kuwa na unyumbufu kwenye msimamo na uvumbuzi.

Kutokana na hali hiyo, wachambuzi wanaona kuwa katika miezi michache ijayo serikali ya Bush itafanya marekebisho juu ya sera zake za mashariki ya kati, kwa upande mmoja itamlinda waziri mkuu mpya wa Israel, kwa upande mwingine itaiunga mkono Palestina ili kuuwezesha mchakato wa amani kati ya nchi hizo mbili ufuate "mpango wa ramani".