Tarehe 9 Iran ilipotangaza kutaka kuanza utafiti wa nishati ya nyuklia, Umoja wa Ulaya, Marekani pamoja na Shirika la Nishati ya Atomiki Duniani mara zilionesha msimamo wa kupinga kwa maneno makali. Vyombo vya habari vilizingatia kwamba hadi jioni ya tarehe hiyo, Iran haijatangaza kwa nchi za nje kuanzisha rasmi utafiti huo.
Msemaji wa serikali ya Iran katika asubuhi ya siku hiyo alipohojiwa na waandishi wa habari mjini Tehran alisema, Iran itarudisha utafiti wa nishani ya nyuklia kama mpango ulivyopangwa katika tarehe 9 chini ya usimamizi wa Shirika la Nishati ya Atomiki Duniani. Na alisema kwamba utafiti huo hauhusiani na sheria, kwani Iran ilisimamisha utafiti huo kwa hiari.
Kiongozi wa kiroho wa Iran Ayatolah Ali Khamenei alisema, Iran inakaribisha nchi za Ulaya na nchi nyingine kushiriki kwenye mpango wa nyuklia wa Iran. Lakini adhabu na vitishio vyovyote havitatikisa nia ya Iran, kwani Iran haitaacha asilan haki yake ya kupata teknolojia ya nyuklia.
Waziri mkuu wa Austria, nchi mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya kwenye mkutano wa kwanza na waandishi wa habari mwaka huu alisema kwamba Austria haijaridhika hata kidogo na Iran kuhusu suala la nyuklia, na ina wasiwasi kuhusu sera fulani za Iran. Alisema, kama Iran ikirudisha shughuli za nyuklia, kuna uwezekano wa kuadhibu Iran, lakini hatua hiyo ni ya mwisho. Waziri wa mambo ya nje wa Austria alisema kuwa kurudisha utafiti wa nyuklia "ni kupiga hatua ya makosa katika njia ya makosa".
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani alisema kuwa serikali ya Ujerumani ina wasiwasi mkubwa kuhusu kauli iliyotolewa karibuni na Iran kuhusu suala la nyuklia. Aliona kuwa kitendo cha Iran kimevunja "Mkataba wa Paris" wa kusimamisha shughuli zote za kusafisha uranium uliotiwa saini na Iran, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza mwezi Novemba mwaka 2004, na kusema kwamba atajadiliana na mawaziri wa mambo ya nje wa Ufaransa na Uingereza kuhusu suala hilo. Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa tarehe 9 alitumai Iran "itabatilisha mara moja uamuzi huo bila masharti yoyote".
Vyombo vya habari vya Magharibi vilimnukuu mwanadiplomasia mmoja wa Umoja wa Ulaya mjini Vienna akisema kuwa, kama kweli Iran itarudisha shughuli za nyuklia, Umoja wa Ulaya utaomba Shirika la Nishati ya Atomiki Duniani liitishe mkutano wa dharura katika mwezi huu ili kujadili suala la nyuklia la Iran na itakuwa pamoja na Marekani kuomba Shirika hilo litoe onyo la mwisho kwa Iran na kuiwekea wakati maalumu kusimamisha tena shughuli zake, alisema kama Iran ikikaidi, nchi hizo mbili zitaomba Shirika hilo liwasilishe suala la nyuklia la Iran kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuiadhibu kiuchumi.
Msemaji wa Ikulu wa Marekani tarehe 9 alipohojiwa na waandishi wa habari alisema, jumuyia ya kimataifa imekuwa na wasiwasi siku hadi siku kuwa Iran inatumia kisingizio cha matumizi ya amani lakini kwa kweli inafanya utafiti na kutengeneza silaha za nyuklia. Alionya kuwa ikiwa Iran haitatekeleza ahadi zake kwa jumuyia ya kimataifa, suala la nyuklia la Iran litawasilishwa kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Katibu mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki Duniani tarehe 9 alipohojiwa na waandishi wa habari wa kituo kimoja cha televisheni alisema, jumuyia ya kimataifa imekuwa ikikata tamaa kuhusu suala la nyuklia la Iran, na kusema kwamba Iran inapaswa iwe wazi zaidi na ishirikiane kwa juhudi na Shirika la Nishati ya Atomiki Duniani.
Habari zinasema kwamba hadi saa tatu za usiku tarehe 9 Iran ilikuwa bado haijatangaza rasmi kwa nchi za nje kuanzisha tena utafiti wa nyuklia. Hali hiyo ilisababisha vyombo vya habari vya Ulaya kufikiria mengi. Baadhi vinafikiri kwamba Iran inaelewa fika nini maana ya hatua yake hiyo, kwa hiyo bado inayumbayumba. Baadhi vinaona kuwa nia ya kurudisha utafiti wa nyuklia haitabadilika ila tu wataalamu wa Shirika la Nishati ya Nyuklia Duniani hawajafika kwenye mahali pa kazi, kwa hiyo haijaondoa lakiri lililopo vifaa vya nyuklia.
Idhaa ya kiswahili 2006-01-10
|