Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-01-10 19:41:08    
Njia ya maendeleo ya mabasi ya Yutong katika nchi za nje

cri

Mwezi Novemba mwaka 2005, bas moja la kifahari lilisafirishwa kwenda Marekani kutoka mji wa Tianjin, sehemu ya kaskazini ya China, jambo ambalo limemaliza historia ya China kutokuwa na mabasi yanauzwa kwenye masoko ya nchi zilizoendelea za Ulaya na Marekani. Mwaka 2006, China itasafirisha mabasi 100 ya aina hiyo kwenda Marekani. Kiwanda kinachotengeneza mabasi ya aina hiyo ni kiwanda cha mabasi ya Yutong kilichoko mjini Zhengzhou. Katika kipindi hiki cha leo nitawaeleza jinsi kiwanda cha Yutong kinavyojitahidi kukuza nguvu yake ya ushindani na kupanua soko la nchi za nje.

Kiwanda hicho ambacho kimeanza kuuza mabasi nchini Marekani kilikuwa ni kiwanda cha magari kisichojulikana sana nchini China katika miaka zaidi ya 10 iliyopita. Wakati ule nchini China kulikuwa na viwanda vya magari zaidi ya elfu moja. Kampuni ya Yutong ilipojenga kiwanda chake cha magari, iliweza tu kutengeneza aina kumi hivi za magari ya kawaida. Lakini kutokana na juhudi zake, kampuni hiyo ilianza kujulikana nchini kutokana na mabasi makubwa na wastani inayotengeneza, ambayo yaliuzwa kwenye nchi karibu 30 zikiwemo Russia, Misri, Iran na Cuba lakini ilikuwa ni vigumu kwa kiwanda hicho kuuza mabasi yake nchini Marekani.

Marekani ni nchi inayojulikana duniani kwa kuwa na vigezo vigumu vya kiwango cha teknolojia cha kuruhusu mabasi ya nchi za nje kuingia kwenye soko lake la magari. Hadi hivi sasa bado ni mabasi machache tu yanayotengenezwa kwenye nchi za Ulaya, Japan na Korea ya Kusini yanayoingia kwenye soko la Marekani. Kuingia Marekani kwa kampuni ya Yutong hakutokani na oda ya mabasi, bali kunatokana na kukamilisha mradi mmoja mkubwa.

Kazi ya kwanza iliyofanywa baada ya Kampuni ya Yutong kupata oda ya magari ya Marekani ilikuwa ni kufanya utafiti kuhusu kanuni husika na vigezo vya teknolojia vya mabasi ya Marekani. Mwakilishi wa kampuni ya Yutong barani Amerika Bw. Zhang Yaowu alisema,

"Kitabu chenye kanuni husika za wizara ya mawasiliano ya Marekani kina kurasa kiasi cha 760, nilikitafsiri kwa muda wa mwezi mmoja, kwanza ni kufahamu masharti husika ya Marekani, na kufanya usanifu wa magari yetu kulingana na viwango vya Marekani."

Shinikizo kutoka soko la Marekani haliko kwenye sheria peke yake, mtazamo wa kiutamaduni na mazoea ya ununuzi wa vitu na tatizo gharama kubwa pia ni changamoto zinazowakabili wasanifu wa China. Mhandisi Zhu Yongsheng mwenye umri wa miaka 28 alishiriki kwenye kazi zote za mradi huo, alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa kwenye soko la mabasi la hivi sasa, usanifu umekuwa kitu muhimu zaidi kinachohusiana na mauzo. Uimara, usalama na zana za kisasa zimekuwa vitu vinavyoathiri moja kwa moja mauzo ya mabasi:

"Marekani imeweka masharti magumu kuhusu usalama. Kwa mfano, madirisha ya pembeni, hapa kwetu ni madirisha yenye vioo visivyofunguka, lakini nchini Marekani watu hawataki hivyo, wanataka madirisha ya pembeni yawe yanaweza kufunguliwa kwa nje na juu. Mabadiliko mengine yanaonekana kwenye ujia ndani ya bas pamoja na ukubwa wa viti.

Jitihada zao hazikupotea bure, baada ya jitihada za muda wa karibu miezi 16, kikundi cha wasanifu kilifaulu kusanifu basi linaloendana na mahitaji ya soko la Marekani. Mabasi ya Yutong hayauzwi nchini Marekani peke yake, kabla ya hapo mabasi 400 yaliyotengenezwa na Kiwanda cha Yutong yaliuzwa nchini Cuba mwaka 2005, ambayo inachukua nafasi ya kwanza kwa wingi wa magari yaliyoagizwa katika oda moja kwa kampuni hiyo. Katika nusu ya kwanza ya mwaka 2005 pato la kampuni ya Yutong kutokana na mauzo ya mabasi katika masoko ya nchi za nje lilifikia dola za kimarekani milioni 37, likiwa ni ongezeko la mara karibu 7 ikilinganishwa na kipindi kama hiki katika mwaka uliotanguliwa. Hivi sasa kampuni ya Yutong imekuwa kituo kikubwa kabisa barani Asia kwa utengenezaji wa mabasi. Mratibu mkuu wa jumuiya ya viwanda vya magari mkoani Henan Bw. Liu Xiaoming alisema, mafanikio ya kampuni ya Yutong katika masoko ya nchi za nje, kwa kiwango kikubwa yalitokana na teknolojia ya kisasa inayotumia.

"Kampuni ya Yutong licha ya kujifunza teknolojia ya kisasa na uzoefu wa usimamizi vya moja ya kampuni tatu zinazochukua nafasi za mbele duniani, vilevile imefaulu na kudumisha umaalum wake katika mabasi inayotengeneza na katika teknolojia. Hii ni muhimu na ya mafanikio katika sekta ya magari."

Kampuni kubwa maarufu aliyotaja Bw. Liu katika eneo la uzalishaji wa mabasi duniani ni MAN Commercial Vehicle Co. Ltd nchini Ujerumani ambayo ni moja ya kampuni maarufu 500 duniani. Mwaka 2002 kampuni ya Yutong na kampuni hiyo ziliwekeza Yuan milioni 320 ili kuanzisha kampuni ya ubia kati yao, na zimejenga kituo cha teknolojia huko Munich. Kampuni hiyo ya ubia inashughulikia uzalishaji na uuzaji wa fremu na vipuri vya mabasi ya hali ya juu ya wastani. Hivi sasa viwanda vya mabasi vya China bado havina sifa nzuri ya kutengeneza fremu za magari, hivyo kampuni ya Yutong iliingia soko la magari ya hali ya juu bila matatizo.

Licha ya kujifunza teknolojia ya kisasa ya Ulaya, kampuni ya Yutong inazingatia utafiti wa teknolojia yake yenyewe. Hivi sasa kampuni hiyo imekuwa kituo pekee cha teknolojia ya mabasi cha ngazi ya taifa nchini, na ni kituo cha utafiti cha wataalamu waliopata shahada ya udakatari. Kampuni ya Yutong inatoa mitaji ya utafiti kwa 4% ya pato lake kutokana na mauzo ya magari, kiasi ambacho kinakaribia kiwango cha uwekezaji kwa utafiti wa teknolojia cha kampuni za kisasa za magari duniani. Hivi sasa pato la kampuni ya Yutong kutokana na mauzo ya magari ya aina mpya imezidi 40% ya jumla ya pato la kampuni hiyo kwa mwaka. Hivi sasa kampuni ya Yutong imekuwa na hataza za aina zaidi ya 90, ambazo zinachukua nafasi ya kwanza nchini China.

Kuweza kutumika kwa muda mrefu kwa mabasi ya Yutong kunatokana na uwekezaji wa kampuni hiyo katika utafiti wa sayansi na teknolojia. Lengo la wateja la kununua mabasi ni kuyatumia katika shughuli za uchukuzi, mabasi yakidumu kwa miaka mingi, basi gharama za uchukuzi itapungua. Mwakilishi wa kampuni ya Yutong kwenye eneo la mashariki ya kati Bw. Li Shuwei alimwambia mwandishi wa habari, kuweza kutumika katika mazingira ya joto kali, yenye upepo mkubwa na ya jangwa ni sababu ya mabasi ya Yutong kupendwa katika soko la mashariki ya kati. Alipozungumzia hali ya mwanzoni ya kujaribu kuingia soko la Iran, alisema, "mengi ya mabasi yanayotumika nchini Iran hivi sasa ni magari yanayotoka Ulaya, hasa ni magari aina ya Benz, lakini yako katika hali isiyo nzuri kutokana na kutumika kwa miaka mingi na hayakupata matunzo mazuri, hivyo serikali ya Iran imeweka mpango wa kubadilisha mabasi yanayotumika nchini humo. Mwaka 2005 Iran ilituma ujumbe mara mbili kufanya uchunguzi nchini China, na hatimaye ilichagua magari ya kampuni ya Yutong na kununua mabasi 1,000.

Hivi sasa kampuni ya Yutong imekuwa na uwezo wa kutengeneza mabasi makubwa na wastani 18,000 na fremu za magari 8,000 kwa mwaka. Lengo lingine muhimu la kampuni ya Yutong ni kufanya pato lake lifikie Yuan bilioni 30 kwa mwaka baada ya miaka mitano hadi saba, na kuchukua nafasi ya 5 katika sekta ya utengenezaji wa mabasi duniani.

Idhaa ya Kiswahili 2006-01-10