Tarehe 10 Iran imeanza kutumia tena vifaa vya kufanyia utafiti wa nishati ya nyuklia vilivyofungwa kwa muda wa miaka miwili, kitendo hicho kimesababisha wasiwasi mkubwa kwa jumuyia ya kimataifa, na kulifanya suala la nyuklia la Iran lililokuwa limepoa baada ya mazungumzo kurudishwa siku chache zilizopita kuzama tena katika hali mbaya.
Naibu mwenyekiti wa kamati ya taifa ya nishati ya nyuklia ya Iran Mohammad Saidi tarehe 10 alitangaza kuwa, mapema katika siku hiyo Iran imeondoa lakiri zilizofungwa kwenye vifaa vya kufanyia utafiti wa nishati ya nyuklia. Alidokeza kuwa, Iran inaanza kutumia vifaa hivyo katika siku hiyo na kurudisha rasmi shughuli za utafiti. Msemaji mwanamke wa Shirika la Nishati ya Atomiki Duniani Melissa Fleming katika siku hiyo amethibitisha kwamba Iran imeanza rasmi kutumia vifaa vya nishati ya nyuklia vilivyopo huko Natanz mbele yawakaguzi wa Shirika la Nishati ya Atomiki Duniani. Katibu mkuu wa Shirika hilo Bw. Baradei pia alidokeza kuwa Iran iliwahi kumweleza kuwa itaanza shughuli za kusafisha uranium kwa kiwango kidogo.
Shughuli za Iran za kuanzisha tena utafiti wa nishati ya nyuklia zimezifanya Marekani, Uingereza, Russia na Ujerumani ziwe wasiwasi mkubwa, zikisema kwamba zitasawazisha msimamo ili kukabiliana na matokeo yatakayotokea.
Wachambuzi wanaona kuwa kitendo hicho cha Iran kinalenga moja kwa moja duru jipya la mazungumzo kati yake na Umoja wa Ulaya yatakayofanyika tarehe 18 mwezi Januari, lakini bado haijulikani kama mazungumzo hayo yanaweza kufanyika kama ilivyopangwa, na pia ni changamoto kwa uvumilivu wa Umoja wa Ulaya. Tokea nchi tatu za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zianze mazungumzo na Iran mwezi Oktoba mwaka 2003, mazungumzo yalijaa kukuru kakara. Mwezi Agosti mwaka jana Umoja wa Ulaya uliotoa mapendekezo mkupuo yanayohusu kuipatia Iran "fadhila" nyingi za kiuchumi, ushirikiano wa sayansi na teknolojia na kuisaidia ijiunge na WTO ili kuishawishi iache shughuli za nishati ya nyuklia. Lakini Iran ilikataa mapendekezo hayo na ilianza matayarisho ya shughuli za kusafisha uranium tarehe 8 mwezi Agosti, na kusababisha mazungumzo kusimama kwa zaidi ya miezi minne hadi tarehe 21 mwezi Desemba mwaka jana. Hivi sasa ni vigumu kubaini kama Umoja wa Ulaya unaendelea kuwa na uvumilivu kuhusu kutatua suala hilo kwa njia ya kidiplomasia. Katika suala la nyuklia la Iran, nchi za Umoja wa Ulaya na Marekani zimeafikiana kimawazo, kwamba Marekani inaunga mkono mazungumzo kati ya Umoja wa Ulaya na Iran, kama mazungumzo yakifanikiwa, basi itakuwa furaha kwa wote; kama mazungumzo yakishindwa, basi Umoja wa Ulaya na Marekani zitajitahidi kuwasilisha suala la nyuklia la Iran kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kwa hiyo, sasa uamuzi uko kwa Umoja wa Ulaya, na uamuzi huo utafanywa kutokana na jinsi mazungumzo yatakavyokuwa.
Iran inaona kuwa hatua ya Iran inachukuliwa kwa mujibu wa sheria ya kimataifa na uungaji mkono wa raia wake. Kwa kuwa nchi iliyotia saini "mkataba wa kutoeneza silaha za nyuklia" Iran ina haki ya kutumia nishati ya nyuklia kwa amani. Ni kuwa na teknolojia ya nishati ya nyuklia tu ndio Iran inaweza kulinda hadhi yake ya kuwa nchi kubwa Mashariki ya Kati. Iran inaona kuwa hadi sasa Marekani haijaweza kujinasua katika usumbufu wa Iraq, na hata kwa kiasi fulani inategemea Iran. Isitoshe Iran ni nchi ya pili inayozalisha mafuta kwa wingi katika OPEC, katika hali ambapo bei ya mafuta inapanda bila kupungua, nchi za Magharibi zikiiwekea vikwazo Iran hazitaweza kuungwa mkono na nchi nyingine. Kutokana na sababu hizo Iran inaelekea lengo lake la nishati ya nyuklia hatua kwa hatua.
Vyombo vya habari vinaona kuwa yumkini shughuli zilizoanzishwa hivi sasa zitaua mjadala. Umoja wa Ulaya umekuwa ukifikiria kuitisha mkutano wa dharura wa Shirika la Nishati ya Atomiki Duniani ili kujadili hatua itakayochukuliwa. Baadhi ya vyombo vya habari vimefafanua kwamba, kutokana na kuwa Russia imetangaza kuanza tena mazungumzo na Iran mwezi Februari kuhusu pendekezo la Russia, nchi za Magharibi pengine zitasubiri zaidi ili Russia itoe mchango katika utatuzi wa suala la nyuklia la Iran.
Idhaa ya Kiswahili 2006-01-11
|