Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-01-11 20:47:36    
China kuanzisha ushirikiano wa kimataifa kuhusu elimu ya juu

cri

Chuo Kikuu cha Beijing ni moja kati ya vyuo vikuu maarufu vya China vinavyojulikana duniani. Katika miaka ya hivi karibuni, chuo kikuu hicho chenye historia ya zaidi ya miaka 100 kiliimarisha maingiliano ya kimataifa kwa kuingiza vitabu vya kiada kutoka nchi za nje na kufanya utafiti kwa kushirikiana na vyuo vikuu vya nchi nyingine duniani. Bw. Xia Hongwei anayefanya kazi katika idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika chuo kikuu hicho alisema, Chuo kikuu hicho kinanufaika kutokana na maingiliano na ushirikiano wa kimataifa, akisema:

"Maingiliano ya kimataifa yameleta wazo jipya la elimu kwa Chuo Kikuu cha Beijing. Vitabu vya kiada na njia ya elimu kutoka nchi za nje vinawasaidia sana walimu wetu, na kuwawezesha kujifunza matunda ya kisasa ya elimu, walimu wetu wanaunganisha matunda hayo ya kisasa na hali halisi ya hivi sasa nchini China, na kutumia mchaganyiko huo katika ufundishaji wa kila siku, na wamepata mafanikio."

Aidha Chuo Kikuu cha Beijing kinafanya utafiti kwa kushirikiana na vyuo vikuu vya nchi za nje. Kwa mfano, katika mwaka 2001, Chuo Kikuu cha Beijing kilishirikiana na Chuo Kikuu cha Yelu cha Marekani kuanzisha maabara za biolojia na kilimo, na kufanya utafiti kwa pamoja. Katika miaka minne tangu maabara hizo zianzishwe, maprofesa wa biolojia na jeni wa Chuo Kikuu cha Yelu karibu wote wametembelea Chuo Kikuu cha Beijing, walianzisha semina, kubadilishana maoni na maprofesa wa Chuo Kikuu cha Beijing, na kujadili masuala ya kitaaluma waliyoyafuatilia. Hivi sasa vyuo vikuu hivyo viwili vinabadilishana walimu kufanya tafiti katika maabara zao, na wametoa kwa pamoja makala kadha wa kadha za taaluma.

Mwanafunzi mmoja wa chuo cha mambo ya fedha katika Chuo Kikuu cha Umma cha China anayeitwa He Li, wakati huu anapokaribia kuhitimu masomo yake ana pilikapilika nyingi. Kwa kuwa Chuo Kikuu cha Umma cha China kinashirikiana na Chuo Kikuu cha Columbia cha Marekani kuanzisha mradi wa elimu ya sera na usimamizi wa mambo ya uchumi na fedha, mwanafunzi wa China baada ya kumaliza masomo ya shahada ya kwanza anaweza kujiandikisha kwenye mradi huo, akifaulu kwenye mtihani husika, anaweza kuendelea na masomo kwa miaka miwili, mwaka mmoja katika Chuo Kikuu cha Umma cha China, mwingine katika Chuo Kikuu cha Columbia cha Marekani, baada ya miaka miwili, atapewa shahada ya pili, hivi sasa He Li anajiandaa kwa mtihani wa kujiunga na mradi huo. Heli akisema:

"Marekani inaongoza duniani wa kiwango cha uchumi wake, bila shaka utafiti wake wa nadharia ya uchumi pia uko mbele duniani, kwa kushiriki kwenye mradi huo naweza kupata habari za uchumi wa Marekani moja kwa moja."

Imefahamika kuwa katika miradi ya elimu iliyoanzishwa kwa ushirikiano, karibu yote ni fani ya uendeshaji wa viwanda na biashara, lugha na fasihi, upashanaji habari za uchumi, sanaa na elimu ya ualimu. Kazi ya elimu inashughulikiwa na nchi za nje, na China inahughulikia uendeshaji wa miradi hiyo. China inatumai kuwa kwa kupitia midadi hiyo, inaweza kuingiza njia za kisasa za elimu na uzoefu wa usimamizi kutoka nchi za nje, ili kuinua kiwango cha wahadhiri wa vyuo vikuu vya China na kuwaandaa watu wenye ujuzi wa fani za kielimu zilizo za dhaifu.

Siku zote kuwapeleka wanafunzi kusoma katika nchi za nje ni njia muhimu ya China ya kujifunza sayansi na teknolojia na njia za kisasa za elimu kutoka kwa nchi nyingine. Katika miaka 25 iliyopita, kuna wanafunzi laki 8 wa China waliosoma katika nchi za nje, hasa katika miaka ya karibuni, kutokana na maendeleo ya kasi ya uchumi wa China na kuongezeka kwa uwezo wa kifedha wa watu wa China, kila mwaka wanafunzi elfu kumi kadhaa wanakwenda kusoma nchi za nje. Na wanafunzi kutoka nchi za nje wanaokuja kusoma nchini China pia wanazidi kuongezeka. Katika mwaka 2004 tu, idadi ya wanafunzi kutoka nchi za nje waliokuja kusoma nchini China ni laki 1.1, idadi ambayo iliongezeka kwa asilimia 40 ikilinganishwa na ile ya mwaka 2003, na wanafunzi hao wanatoka kwenye nchi zaidi ya 170, nchi zenye wanafunzi wengi zaidi wanaosoma nchini China kusoma ni Korea ya Kusini, Japan, Marekani, Vietnam na Indonesia.

Kijana anayeitwa Ki Joon Kwon anatoka Korea ya Kusini, hivi sasa yeye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa kitivo cha usimamizi wa uchumi cha Chuo Kikuu cha Beijing. Anaona kuwa kuja China kusoma ni chaguo zuri zaidi maishani mwake, kwani makampuni makubwa nchini Korea ya Kusini, hasa Idara za Mambo ya Fedha za Korea ya Kusini zinahitaji watu wanaoifahamu vizuri China na kujua mambo mengi kuhusu China, hivyo mtu wa Korea ya Kusini akihitimu kutoka kwenye vyuo vikuu maarufu vya China, atapata mshahara mzuri zaidi kuliko aliyehitimu kutoka kwenye Chuo Kikuu cha Seoul, ambacho ni chuo kikuu maarufu zaidi nchini Korea ya Kusini. Alisema:

"Kutokana na mazingira mazuri yanayotolewa na serikali na makampuni makubwa ya Korea ya Kusini, hivi sasa watu wengi zaidi wa nchi yetu wanakuja kusoma nchini China, kati ya wenzangu wa shule ya sekondari ya juu, sita au saba wanasoma katika Chuo Kikuu cha Beijing."

Katika miaka ya karibuni, China imechukua hatua mbalimbali za kuweka mazingira mazuri zaidi kwa masomo na maisha ya wanafunzi wanaotoka nchi za nje, zikiwemo kuinua kiwango cha walimu, kukamilisha utaratibu wa bima ya matibabu kwa wanafunzi kutoka nchi za nje, na kuanzisha mfumo wa kompyuta wa kuhifadhi habari za wanafunzi hao na kutoa huduma nyingi kwa wanafunzi hao.

Kazi nyingine muhimu ya maingiliano ya kimataifa kwa China katika elimu ya hali ya juu ni, kutoa misaada kwa nchi zinazoendelea na kuziwezesha nchi hizo kunufaika na mafanikio iliyoyapata China katika eneo la elimu, sayansi na teknolojia. Kwa mfano, tangu kuzaliwa kwa China mpya hadi mwaka 2004, China imetoa misaada ya mafunzo ya kiserikali kwa watu elfu 17 wa nchi 50 za Afrika, kuwasaidia kuja kusoma nchini China, pia China imewapeleka walimu 530 barani Afrika kuzisaidia nchi hizo kuendeleza fani za elimu za nchi hizo zilizo za dhaifu.

Ofisa wa waizara ya elimu ya Ethiopia Bw. Sintayehu Woldemichael siku za karibuni alipohudhuria mkutano mmoja wa kimataifa hapa Beijing alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, tangu mwaka 2004, China imeanza kutoa misaada mingi zaidi ya mafunzo kwa wanafunzi wa Ethiopia wanaosoma nchini China, Ethiopia inaishukuru sana China kwa urafiki na misaada yake. alisema:

"Vyuo vikuu vyote nchini Ethiopia vina uhusiano na vyuo vikuu vya China, vyuo vikuu vya nchi hizo mbili kufanya utafiti kwa ushirikiano na kubadilishana walimu kunanufaisha pande mbili zote." Alisema hivi sasa, walimu 70 wa China wanafundisha katika vyuo vikuu nchini Ethiopia, walikwenda nchini humo na sayansi na teknolojia na njia za kisasa za elimu.