Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-01-12 16:44:25    
Maisha ya wakulima wa China kuwa mazuri siku hadi siku

cri

China ni nchi yenye wakulima wengi, kati ya idadi kubwa ya watu wa China, zaidi ya milioni 800 ni wakulima. Ikilinganishwa na wakazi wa mijini, kiwango cha maisha ya wakulima wengi bado ni cha chini. Katika miaka ya karibuni, namna ya kuboresha maisha ya wakulima limekuwa jukumu kubwa la serikali katika ngazi tofauti.

Mji wa Dalian, mkoani Liaoning, kaskazini mashariki mwa China ni mji mzuri wa pwani. Katika miaka kadhaa iliyopita, mkulima Luo Chuangyuan kutoka mkoa wa Henna, katikati ya China alikwenda huko Dalian kufanya kazi ya kibarua cha Ujenzi. Mwanzoni mwa mwaka 2005, alitaka kupata fidia kutokana na kukatwa mguu wake wa kulia kwenye ajali kazini. Lakini mwajiri wake alikataa kumlipia gharama za matibabu na fidia za kimaisha, familia yake ikakumbwa na shida kubwa. Alipaswa kuomba msaada kutoka kwa shirikisho la wafanyakazi. Akisema:

"Mimi sikuweza kutatua suala hilo mwenyewe. Lakini kutokana na msaada wa shirikisho la wafanyakazi, hatimaye nilipewa fidia za Yuan elfu 60."

Muda si mrefu uliopita, mwandishi wetu wa habari alimkuta Bw. Luo Chuangyuan nyumbani kwake, amewekewa mguu wa bandia, na kukarabati nyumba yake. Hivi sasa licha ya mapato ya kilimo, kupanda miti ya matunda na kufuga nguruwe, Bw. Luo Chuangyuan pia anapewa msaada wa serikali kila mwezi kutokana na ulemavu wake.

Shirikisho la wafanyakazi lililomsaidia Bw. Luo Chuangyuan lilianzishwa na serikali ya wilaya ya Xinxian nyumbani kwake kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wa huko kulinda haki na maslahi walipofanya kazi za vibarua nje ya mkoa wa Henan. Katika muda wa zaidi ya mwaka mmoja uliopita, shirikisho hilo limeshughulikia kesi zaidi ya 30 katika mji wa Dalian peke yake.

Kutokana na kuharakishwa kwa mchakato wa utandawazi wa miji nchini China, idadi ya wakulima wanaofanya kazi za vibarua mijini kama Bw. Luo Chuangyuan imeongezeka siku hadi siku, hivi sasa idadi hiyo imefikia milioni 120. Licha ya kuwepo kwa uwezekano wa kukumbwa na matukio ya ajali kazini, wakulima vibarua pia wanakabiliwa na mgogoro wa kucheleweshwa kwa mishahara. Ili kutatua tatizo hilo, katika miaka miwili iliyopita baraza la serikali la China lilitoa waraka maalum, serikali za miji na mikoa pia zimeunda vikundi vya uongozi vya kurudisha mishahara ya wakulima vibarua iliyocheleweshwa, na kuanzisha idara maalum kushughulikia kazi hiyo. Bw. Yin Jiaqi aliyefanya kazi ya kibarua mjini Dalian alisema:

"Katika nusu ya kwanza ya mwaka uliopita nilifanya kazi katika kampuni ya ujenzi wa nyumba ya Dalian, nilikuwa nikifanya kazi ya kubomoa nyumba, mshahara wangu kwa mwezi ulikuwa ni Yuan 1800. Lakini kampuni hiyo ilicheleweshwa kwa makusudi kunipatia mshahara wangu. Nilipofahamu utaratibu uliowekwa na kamati kuu kuhusu kupiga marufuku kuchelewesha mishahara ya wakulima vibarua, nilikabidhi kesi yangu katika idara ya huduma na usimamizi wa nguvukazi, suala langu lilitatuliwa haraka."

Imefahamika kuwa, katika nusu ya kwanza ya mwaka uliopita, idara za huduma na usimamizi wa nguvukazi katika ngazi tofauti kwa jumla zilishughulikia kesi elfu 70 za aina hiyo, na kuwarudishia wakulima mishahara yao ya Yuan zaidi ya bilioni 3.

Jambo lingine linalomfurahisha Bw. Yin Jiaqi ni kwamba, binti yake anaweza kusoma shule kama watoto wengine wa wakazi wa Dalian, hana haja tena ya kulipa nyongeza ya gharama za masomo. Hii ni hatua nyingine muhimu iliyochukuliwa nchini China kwa ajili ya kulinda haki na maslahi ya wakulima vibarua. Binti wa Bw. Yin Jiaqi anayesoma katika shule moja ya msingi iliyoko katikati ya mji wa Dalian alisema kwa furaha:

"Nasoma darasa la nne, walimu na wanafunzi wenzangu wote wananipenda, mimi hucheza pamoja nao. Matokeo yangu ya masomo yanachukua nafasi ya nne darasani."

Wakati wakulima vibarua walipohakikishiwa haki na maslahi yao ya aina mbalimbali, maisha ya wakulima wanaobaki nyumbani pia yamekuwa mazuri siku hadi siku. Bw. Chen Shangjun mwenye umri wa miaka zaidi ya 40 anaishi katika kijiji kimoja na wakulima wengine wawili tuliowataja, familia yake yenye watu 5 ina nyumba ya ghorofa na ua mkubwa, licha ya kulima nafaka na mboga kwenye shamba lenye hekta 0.4, wakati wa mapumziko ya kilimo, Bw. Chen na ndugu yake huenda nje ya kijiji chao kufanya kazi za vibarua. Jambo lingine linalomfurahisha Bw. Chen na wakulima wengine ni kusamehewa au kupunguzwa kodi za kilimo. Alisema:

"Zamani kila mtu alipaswa kulipa kodi ya kilimo Yuan zaidi ya 200 kwa mwaka, hivi sasa familia yangu inaweza kuokoa Yuan 1400 za kodi kwa mwaka."

Mwaka 2005, miji na mikoa 26 kati ya 30 nchini China imetangaza kuondoa kodi za kilimo. Juhudi za wakulima wa kulima nafaka zimehamasishwa kwa kiasi kikubwa. Katika mwaka wa 2006, kodi za kilimo za wakulima wote zitafutwa kabisa, maisha ya wakulima bila shaka yataboreshwa zaidi.

Licha ya hayo, bado kuna hatua nyingine za kuboresha maisha ya wakulima kama vile, wilaya ya Xinxian mkoani Henan imefanya jaribio la kuanzisha utaratibu wa tiba ya ushirika vijijini, ili kutatua suala la wakulima la kukosa huduma za matibabu. Yaani wakulima wakitoa Yuan kumi kwa mwaka, wakiugua wanaweza kulipiwa asilimia 80 ya gharama za matibabu. Hatua hiyo inawaridhisha sana wakulima.

Imefahamika kuwa ifikapo mwaka 2010, utaratibu huo wa tiba ya ushirika wa vijijini utawanufaisha wakulima wote nchini China. Kwa ujumla maisha ya wakulima wa China yamekuwa mazuri siku hadi siku, serikali ya China imeamua kuimarisha uungaji mkono kwa kilimo, ili kuongeza mapato ya wakulima na kulinda vizuri haki na maslahi yao.

Idhaa ya kiswahili 2006-01-12