Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-01-13 13:17:18    
Mpango mpya wa kiwenzi wa maendeleo ya kiuchumi usio na uchafuzi wa hewa wa Asia na Pasifiki waanzishwa

cri

Mkutano wa kuanzisha "mpango mpya wa kiwenzi wa maendeleo ya kiuchumi usio na uchafuzi wa hewa wa Asia na Pasifiki" ulimalizika tarehe 12 mjini Sydney, Australia. Mpango wenye nchi sita wa kupambna na ongezeko la joto duniani umeanzishwa.

Mpango huo umetolewa kwa msingi wa taarifa ya pamoja kimawazo iliyotolewa mjini Vientiane, Laos, tarehe 28 mwezi Julai na nchi za China, Marekani, Japan, India, Australia na Korea ya Kusini. Huu ni mpango wa ushirikiano mpya katika kanda ya Asia na Pasifiki. Nchi zinazoshiriki katika mpango huo zina watu karibu nusu ya watu wote wa dunia, na matumizi ya nishati na utoaji wa hewa chafu unakaribia nusu ya hewa chafu iliyotolewa duniani. Kwa hiyo madhumuni ya mpango huo ni kuanzisha ushirikiano wa kimataifa wa hiari na usio na nguvu za kisheria, na kwa kupitia ushirikiano huo kusaidiana kwa teknolojia zenye tija kubwa na usafi. Nchi hizo sita zinaona kuwa mpango huo unalingana na "mkataba wa kimsingi wa mabadiliko ya hali ya hewa" wa Umoja wa Mataifa, na ni nyongeza na sio mbadala wa "mkataba wa Kyoto" wa kupambana na tishio la ongezeko la joto duniani.

Mkutano huo uliofanyika tarehe 12 umepitisha nyaraka tatu za "Katiba ya mpango mpya wa kiwenzi wa maendeleo ya kiuchumi usio na uchafuzi wa hewa wa Asia na Pasifiki, "Taarifa ya Pamoja" na "Mpango wa Utekelezaji". Ili kutekeleza mambo yaliyopitishwa katika mkutano huo, vikundi vinane viliundwa ambavyo vitaweka mpango wa utekelezaji kuhusu matumizi na maendeleo ya uzalishaji wa nishati, chuma na chuma cha pua, aluminium, saruji, migodi ya makaa ya mawe, uzalishaji wa umeme na usambazaji wa umeme, ujenzi wa majengo na vyombo vya umeme vya majumbani. Isitoshe, nchi hizo sita zilisisitiza umuhimu wa nishati ya migodi kwa uchumi, na zimeingiza maendeleo ya teknolojia ya kukusanya na kuweka akiba hewa ya kabonda oksaid, usafi wa matumizi ya makaa ya mawe na matumizi ya hewa kwenye matabaka ya makaa ya mawe kama ni mambo muhimu katika "mpango wa utekelezaji".

Kwenye mkutano wa tarehe 12, Marekani na Australia zilitangaza kuwa zitatenga dola za Kimarekani milioni 130 ili kusaidia nchi wanachama wa mpango huo kugeuza viwanda vinavyotumia nishati nyingi na kupunguza utoaji hewa chafu na kuendeleza nishati mbadala yenye tija kubwa.

Mjumbe wa taifa na katibu mkuu wa baraza la serikali ya China Bw. Hua Jianmin kwenye mkutano huo alisema, mpango huo ni majaribio yenye manufaa kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko mabaya ya hali ya hewa. Mpango huo umesisitiza umuhimu wa maendeleo ya uchumi na kuondoa umaskini katika juhudi za kupambana na ongezeko la joto duniani, na umetoa uzito kwa teknolojia katika matumizi ya nishati. Bw. Hua licha ya kusema kuwa China itajitahidi kushiriki kwenye mpango huo, pia alitoa mapendekezo mengi. Alipoeleza juhudi zilizofanywa na China katika hifadhi ya mazingira alisema, China ikiwa nchi yenye watu bilioni 1.3 inakabiliwa tatizo kubwa la usafi wa mazingira. Viongozi wa China wamesema wazi kwamba, China lazima iwe na fikra za kuendeleza uchumi kisayansi, na sera za kuokoa nishati ziwe sera za kimsingi za taifa na kuharakisha ujenzi wa jamii yenye uokoaji wa nishati na upatanifu mzuri na mazingira.

Katika siku za mkutano, wanamashirika zaidi ya 80 waliotoka mashirika makubwa duniani walibadilishana maoni na kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano baina yao na wa kiserikali. Naibu mkurugenzi wa Kamati ya Maendeleo ya Mageuzi ya China Bw. Jiang Weixin alitumai mashirika ya China na mashirika ya nchi zilizoendelea yatashirikiana katika juhudi za kuhifadhi mazingira safi, kuokoa nishati na kupunguza utoaji wa hewa chafu.

Idhaa ya kiswahili 2006-01-13