Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-01-13 16:47:25    
Thamani ya biashara kati ya China na Afrika kuzidi dola za kimarekani bilioni 30

cri

    Takwimu kutoka Idara ya forodha ya China zinaonesha kuwa, katika miezi 10 ya mwanzo ya mwaka 2005, thamani ya biashara kati ya China na Afrika imefikia dola za kimarekani bilioni 32.17, kiasi ambacho kimezidi thamani ya jumla ya mwaka 2004.
Wataalamu wanakadiria kuwa, mwaka 2005 thamani ya biashara kati ya China na Afrika inatazamiwa kuzidi dola za kimarekani bilioni 37, na mwaka 2004 kiasi hicho kilikuwa ni chini ya dola za kimarekani bilioni 30. Katika miezi 10 ya mwanzo ya mwaka 2005, ongezeko la thamani ya biashara kati ya China na Afrika lilifikia asilimia 39.1.
    Ofisa wa Wizara ya Biashara ya China alisema, tangu Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika lianzishwe mwaka 2000, ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Afrika umeingia katika kipindi kipya cha kupata maendeleo ya kasi na tulivu, na katika sekta zote. Thamani ya biashara iliongezeka maradufu katika miaka 5 iliyopita, na miundo ya biashara imekuwa ikiboreshwa.
    Katika miaka ya hivi karibuni, thamani ya biashara ya bidhaa zinazoagizwa kutoka Afrika kuja nchini China imekuwa ikizidi ile ya bidhaa zinazouzwa barani Afrika. Miundo ya uuzaji wa bidhaa za China katika nchi za Afrika inazidi kuboreshwa, na thamani ya mitambo ya umeme na bidhaa za teknolojia mpya ya hali ya juu za China inachukua karibu nusu ya thamani ya jumla ya bidhaa za China zinazouzwa barani Afrika, na pia inaongezekea kwa haraka. 
    Katika miezi 10 ya mwanzo ya mwaka 2005, thamani ya bidhaa zilizouzwa barani Afrika imefikia dola za kimarekani bilioni 15.25, kiasi ambacho kinaongezeka kwa asilimia 38.9 kuliko mwaka juzi, na thamani ya bidhaa zilizoagizwa kutoka Afrika ilikuwa bilioni 16.92, kiasi ambacho kiliongezeka kwa asilimia 39.4. 
   Ofisa wa Wizara ya biashara ya China alisema, mwaka 2005 hali ya jumla ya kisiasa barani Afrika ilikuwa tulivu zaidi, na ongezeko la uchumi lilipata maendeleo ya kasi. Nchi za Afrika zilikuwa zinatilia maanani zaidi kuimarisha mawasiliano ya kiuchumi na kibiashara kati yake na China. Kuimarishwa kwa mawasiliano kati ya viongozi wa ngazi ya juu wa China na wa nchi za Afrika kunaonesha matumaini ya viongozi wa pande hizo mbili katika kuimarisha ushirikiano wa kirafiki, na kusukuma mbele kwa nguvu maendeleo ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya pande hizo mbili.
    Kuanzia tarehe 1 Januari mwaka 2005, China ilisamehe ushuru wa bidhaa 190 za nchi 28 zilizoko nyuma kiuchumi zinazouzwa nchini China, na hatua hii imezifanya nchi za Afrika kuongeza bidhaa zake zinazouzwa nchini China kwa zaidi ya mara moja. 
Ofisa wa Wizara ya Biashara ya China alisema, serikali ya China inahamasisha kampuni za China kuanzisha biashara barani Afrika. Maeneo ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya China na Afrika yamekuwa yakiongezeka zaidi. Miradi ya China barani Afrika inaenea katika sekta mbalimbali, zikiwemo biashara, uendelezaji wa maliasili, mawasiliano na uchukuzi, kilimo na uendelezji wa kilimo na mazao ya kilimo.
    Kutokana na takwimu za mwanzo, kuanzia mwezi Januari hadi Oktoba mwaka 2005, thamani ya uwekezaji barani Afrika ilifikia dola za kimarekani milioni 175. Hadi kufikia mwezi Oktoba mwaka 2005, uwekezaji wa jumla wa mashirika ya China barani Afrika ulifikia dola za kimarekani bilioni 1.075. China ilisaini Makubaliano ya kunufaishana na kuhakikisha uwekezaji na nchi 28 za Afrika, na kusaini Makubaliano ya kukwepa kutoza kodi mara mbili na nchi 8 za Afrika.
    Wakati huo huo, shughuli za mikataba za mashirika ya China barani Afrika pia zilidumisha ongezeko la kasi. Katika miezi 10 ya mwanzo ya mwaka 2005, thamani ya mikataba ya shughuli za wafanyakazi iliyosainiwa na mashirika ya China barani Afrika ilifikia dola za kimarekani bilioni 6.34. 
    Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika limekuwa sehemu muhimu kwa pande hizo mbili kuimarisha mazungumzo na kuhimiza ushirikiano. Mwaka 2005, China na Afrika zilichukua hatua mbalimbali kupanua ushirikiano wa kunufaishana chini ya baraza hilo. Hivi sasa China na nchi 35 za Afrika zimeanzisha utaratibu wa Kamati ya pamoja ya uchumi na biashara ya pande hizo mbili. Utaratibu huo umefanya kazi nzuri katika kuratibu ushirikiano huo wa kiuchumi na kibiashara kati ya pande hizo mbili, na kutatua kwa njia mwafaka matatizo yaliyopo kwenye ushirikiano huo wa kiuchumi na kibiashara kati ya pande hizo mbili.
    Ofisa wa Wizara ya Biashara ya China alisema, misaada inayotolewa na China kwa Afrika ni sehemu muhimu katika ushirikiano kati ya pande hizo mbili. Kadiri uwezo wa uchumi wa China unavyoongezeka, ndivyo China inavyoongeza nguvu katika kutoa misaada kwa Afrika. Pia China inatoa mafunzo ya utaalam kwa nchi za Afrika katika sekta mbalimbali. Ofisa huyo anaamini kuwa, mwaka 2006 ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya pande hizo mbili utapata maendeleo makubwa.

Idhaa ya kiswahili 2006-01-13