Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-01-13 20:29:24    
Wananchi wa China na Afrika watakiwa kuongeza maelewano na maingiliano ili kufanya vizuri zaidi ushirikiano katika sekta mbalimbali

cri

Hivi karibuni mwandishi wetu wa Habari alipata fursa ya kufanya mahojiano na Bwana Abdullah Hamisi mwanafunzi kutoka Zanzibar Tanzania anayesoma kwenye chuo kikuu cha sayansi na teknolojia hapa Beijing, China. Yafuatayo ni mahojiano kati ya Mwandishi wetu na Bwana Abdullah.

Mwandishi wa habari: Sasa mwaka 2005 umekwisha, na tayari tumeingia katika mwaka 2006. Bwana Abdullah tukizungumzia mwaka 2005 uliopita unapata kumbukumbu gani?

Abdullah: Kwangu mimi ni mwaka 2005 ulikuwa ni mgumu hasa kwa wanafunzi kama mimi tunaotoka nchi za nje tunaosoma hapa nchini China, kwa sababu tulipaswa kutumia lugha ya kichina katika masomo mbalimbali, tena masomo hayo ni mengi na ya aina mbalimbali. Lugha ya kichina si rahisi kujifunza hasa kwa sisi wageni, lakini hali yangu si mbaya sana.

Mwandishi: Huu ni mwaka wako wa nne sasa tangu uanze kusoma hapa Beijing, China, unashirikiana vipi na wanafunzi wengine wa China shuleni na nje ya shule?

Abdullah: Hivi sasa nikiwasiliana na wachina hakuna ugumu wowote, tunafahamiana na tunaelewana, na nimepata bahati sasa hivi kujua maisha ya kichina, juhudi zao katika kazi na mambo mengine ya maisha ya kila siku.

Mwandishi: Unaona uelewa kati ya wachina kuhusu Afrika na uelewa wa waafrika kuhusu China ukoje?

Abdullah: Naona baadhi ya wachina hasa vijana bado hawana uelewa mzuri kuhusu hali ya Afrika, na hata waafrika walioko kule nyumbani hawana uelewa mzuri kuhusu China. Naona ni wajibu kwa vyombo vya habari kuzungumzia na kueleza hali halisi ya Afrika kwa wachina hao, tunatakiwa kuongeza maelewano na maingiliano ili China na Afrika ziweze kufanya ushirikiano mzuri katika sekta mbalimbali. Hivi sasa wanafunzi wa nchi za Afrika wanaosoma nchini China wanaishi vizuri, tunaona waafrika na wachina hata wamarekani tuko sawa katika fikra na mambo mengine mengi.

Mwandishi: Na unaweza kutueleza jinsi nyie wanafunzi kutoka Afrika mnavyoshirikiana na wachina nje ya masomo?

Abdullah: Waafrika wengi wanajua wachina ni wakarimu. Nchini Tanzania, wachina wanatoa ushirikiano wa dhati, na tumekuwa tunashirikiana nao katika sekta za uchumi, siasa na jamii. Urafiki wetu ni mzuri. Hakuna tofauti kubwa kati ya China na Tanzania, watu wote tuna lengo moja. Hata ushirikiano tulionao hapa China nje ya masomo, hauna tofauti na ule wa nchi zetu.

Mwandishi: Ukiwa hapa Beijing kusoma, unawakumbuka watu wa nyumbani Zanzibar au unakumbuka chakula ambacho ulizoea kula nyumbani?

Abdullah: Najua nyumbani ni nyumbani, sasa nimeshazoea maisha nchini China lakini siwezi kusahau nyumbani. Kwa upande wa chakula ninachoweza kusema ni kuwa nimegundua kitu kimoja kinachotofautiana na jinsi sisi tunavyoandaa chakula kule nyumbani. Sisi nyumbani tunapoandaa chakula, hatuzingatii sana lishe tunazingatia utamu wa chakula, lakini hapa nchini China watu wanaangalia zaidi chakula bora, upishi wa aina mbalimbali wa chakula unazingatia lishe zaidi.

Mwandishi: Unaonaje hali ya michezo ya hapa China na ya Afrika ya mashariki?

Abdullah: Naona sisi tuko nyuma sana kwenye baadhi ya michezo kuliko wachina. Nimeona watoto wadogo wenye umri wa miaka mitatu hadi minne wanaanza kuandaliwa tokea mwanzo kabisa katika michezo mbalimbali, na baadaye wanakuwa wanamichezo wakubwa. Ingawa katika nchi zetu kuna watoto wanaokuwa na vipaji, lakini vipaji hivyo katika michezo ya mpira wa kikapu au mpira wa mikono na miguu haviendelezwi kutokana na kutokuwa na miundo mbinu mizuri ya michezo.

Idhaa ya Kiswahili 2006-01-13