Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-01-17 18:07:43    
Kuchaguliwa kwa watu mashuhuri kwenye mambo ya uchumi ni jambo jipya muhimu katika maendeleo ya uchumi wa China

cri

Matokeo rasmi ya uchaguzi wa watu mashuhuri kwenye sekta ya uchumi ya China mwaka 2005 yalitangazwa hivi karibuni. Uchaguzi huo ulifanyika kwa upigaji kura za maoni ya raia na uteuzi wa wataalamu. Watu kumi mashuhuri kwenye mambo ya uchumi wote walikuwa waendeshaji wa kampuni au viwanda, ingawa walipendwa na umma na wataalamu kutokana na sababu mbalimbali, lakini maendeleo ya kampuni na viwanda ni kigezo muhimu cha kupima mchango waliotoa kwa maendeleo ya uchumi na jamii ya China.

Ni dhahiri kwamba uchumi wa China umepata maendeleo makubwa yanayofuatiliwa na watu duniani katika miaka zaidi ya 20 iliyopita, wastani wa ongezeko la zaidi ya 9% la pato la taifa limefanya uchumi wa China kuchukua nafasi ya 6 duniani mwaka 2004. Lakini wakati uchumi wa taifa unapokuwa na ongezeko la kasi, baadhi ya matatizo yakiwa ni pamoja na uwezo mdogo wa uvumbuzi na nyongeza ndogo ya thamani ya mazao ya kampuni na viwanda vya China yameibuka. Ili kudumisha maendeleo ya uchumi wa China, watu wengi zaidi nchini China, wanataka kampuni na viwanda vizalishe mazao ya teknolojia ya kisasa na yenye haki-miliki ya China.

Katika mazingira kama hayo, ofisa mtendaji wa kwanza wa kampuni ya elektroniki ya Zhongxing Bw. Deng Zhonghan alipewa tuzo ya juu kabisa ya mwanauchumi mashuhuri wa China mwaka 2005. Bw. Deng aliongoza kampuni yake kuvumbua COMS chip ya China yenyewe, ambayo inachukua zaidi ya 60% ya COMS chip ya kompyuta duniani. Katika sherehe ya utoaji tuzo, Bw. Deng Zhonghan alisema,

"Kampuni kuweka lengo la uvumbuzi ni mwelekeo wa maendeleo ya uchumi wa China katika siku za baadaye. Ninaona, mimi ninachukua tuzo hiyo kwa kuwakilisha watu wote wanaofuata njia ya kufanya utafiti wa uvumbuzi wa China. Hii ni alama ya uchumi wa uvumbuzi wenye haki-miliki ya China."

Ikiwa tunasema Bw. Deng Zhonghan na kampuni yake wanawakilisha moja ya njia ya mageuzi ya maendeleo ya uchumi wa China, basi kuchaguliwa kwa meneja mkuu wa kampuni ya mafuta ya asili ya petroli ya baharini ya China Bw. Fu Chengyu kunaonesha wazo la kampuni na viwanda vya China kujiendeleza katika nchi za nje linaungwa mkono na watu wengi nchini.

Mwaka 2005, kampuni ya mafuta ya baharini ya China ilitoa dola za kimarekani bilioni 18.5 kwa Unical, kampuni ya mafuta ya 9 kwa ukubwa nchini Marekani ya kununua kampuni hiyo. Ingawa ununuzi huo haukufanikiwa kutokana na shinikizo la kisiasa nchini Marekani, lakini kwa jinsi anavyoona Bw. Fu Chengyu, uzoefu huo umenufaisha kampuni ya mafuta ya baharini ya China hata sekta ya uzalishaji mali ya China.

"Wenye hisa za kampuni yetu hawaoni kama tulishindwa, kwani tulichuana na mshindani wetu kwenye soko la mitaji la duniani kwa kufuata kanuni za kimataifa, ingawa ununuzi huo haukufanikiwa kutokana na sababu tunazozifahamu, lakini watu wenye hisa za kampuni yetu wamefurahia kitendo chetu hicho, soko la mitaji linaona kampuni yetu ni kampuni iliyokomaa. Aidha, ununuzi huo umeboresha sura ya kampuni za China kwenye soko la kimataifa, matokeo hayo hayapatikani kwa pesa."

Wawakilishi wa viwanda vya serikali waliochaguliwa kuwa wanauchumi mashuhuri wa China mwaka 2005 ni pamoja na mkurugenzi mkuu wa kampuni ya maziwa ya Yili Bw. Pan Gang, ambaye alikabidhiwa wadhifa huo wakati menejimenti ya ngazi ya juu ya zamani ya kampuni hiyo ilikuwa na kashfa kuhusu mambo ya fedha, na aliongoza kampuni hiyo kuwa na pato la Yuan zaidi ya bilioni 10. Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya uchukuzi wa baharini ya China Bw. Wei Jiafu, ambaye kampuni yake ilikusanya Yuan milioni 100 na kuanzisha shirika la kwanza la kampuni za China la kusaidia watu maskini na wanaohitaji msaada. Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya injini za dizeli ya Huifang Bw. Tan Xuguang, ambaye kampuni yake imevumbua injini yenye nguvu inayofanya kazi kwa kasi ya China. Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Haixin Bw. Zhou Houjian, ambaye kampuni yake imefanikiwa katika uvumbuzi na kuzalisha kifaa cha hali ya juu cha kuboresha mawimbi ya Video.

Hali maalumu nyingine ya uchaguzi huo ni kulingana kwa idadi ya wanaviwanda binafsi na wawakilishi wa viwanda vya serikali waliochaguliwa, wakiwemo Bw. Deng Zhonghan aliyepewa tuzo ya juu kabisa, mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Wanda ya mji wa Dalian Bw. Wang Jianlin, ambaye alianzisha shirika la kusaidia wakulima vibarua wa mijini, mkurugenzi mkuu wa kampuni ya magari ya Chery yenye hataza ya China. Licha ya hayo, kuna mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Tatu Moja Bw. Liang Wengen, ofisa mtendaji wa kwanza wa tovuti ya Baidu Bw. Li Yanhong. Mwenyekiti wa shirikisho la wanaviwanda na wafanyabiashara wa China Bw. Huang Mengfu alisema, kuchaguliwa kwa watu kama wao, kunaonesha kwamba umuhimu wa uchumi binafsi katika uchumi wa China umeimarika.

"Uchumi binafsi unatoa 75% ya ajira nchini China, uchumi binafsi na wanaviwanda binafsi wametoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya uchumi wa China."

Mbali ya kuchaguliwa kwa wanauchumi mashuhuri wa mwaka, harakati hizo za uchaguzi zilitoa tuzo ya huduma ya jamii kwa kuwapa moyo watu waliohimiza maendeleo ya uwiano kati ya uchumi na jamii nchini. Kiongozi wa kituo cha utamaduni wa kijiji cha dunia, Beijing bibi Liao Xiaoyi alipewa tuzo hiyo.

Tangu kuanzishwa jumuiya hiyo isiyo ya kiserikali ya kijiji cha dunia hapa Beijing mwaka 1995, bibi Liao Xiaoyi alipiga video zaidi ya 100 kuhusu hifadhi ya mazingira ya asili, na kuanzisha "baraza la waandishi wa habari kuhusu nishati endelevu". Alitoa wito wa kutaka umma kutumia mabasi badala ya motokaa binafsi ili kupunguza hewa chafu zinazotolewa na magari pamoja na matumizi ya nishati. Bibi Liao Xiaoyi ni mtu pekee nchini China aliyepewa tuzo kubwa ya mazingira na maendeleo ya kimataifa inayojulikana kama tuzo ya Sophie. Kamati ya uchaguzi ilipoandika maelezo kuhusu sifa za bibi Liao ilisema, watu wengi wanafuatilia hifadhi ya mazingira, lakini yeye ni mwangalifu mkubwa zaidi, anabadilisha matumizi ya kimaisha ya umma kuwa vitendo vyenye ufanisi katika kuhifadhi mazingira ya asili. Bibi Liao Xiaoyi alipohojiwa na mwandishi wa habari alisema, maendeleo ya kasi ya uchumi yameleta shinikizo kubwa kwa muundo wa mazingira ya China, shughuli za hifadhi ya mazingira zinatakiwa kushirikisha serikali, viwanda na umma kwa pamoja.

Uchaguzi wa wanauchumi mashuhuri wa mwaka 2005 ulifuatiliwa na watu wengi nchini China, idadi ya watu walioshiriki kwenye upigaji kura kwenye tovuti ilikuwa milioni kadhaa.