Baada ya kumalizika vita nchini Liberia, Bibi Ellen Johnson-Sirleaf, ambaye ni rais mteule wa kwanza wa kike aliapishwa kushika wadhifa huo tarehe 16 huko Monrovia, mji mkuu wa nchi hiyo. Bibi Ellen Johnson-Sirleaf mwenye umri wa miaka 67 ni rais wa kwanza wa mwanamke aliyechaguliwa na wapiga kura katika historia ya bara la Afrika.
Bibi Ellen Johnson-Sirleaf katika sherehe ya kuapishwa kwake siku hiyo alisema, serikali mpya atakayoiongoza itajitahidi kuhimiza amani na utulivu nchini humo, kufanya shughuli za ujenzi mpya wa nchi baada ya kumalizika kwa vita na kurejesha imani ya watu wa nchi hiyo. Baadhi ya wakuu wa nchi na viongozi wa serikali za nchi za Afrika wakiwemo mwenyekiti wa Umoja wa Afrika aliye rais wa Nigeria Bw. Olusegun Obasanjo, mjumbe maalumu wa rais Hu Jintao wa China aliye waziri wa mambo ya nje Bw. Li Zhaoxing na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi Condoleezza Rice walihudhuria sherehe hiyo.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe vililipuka nchini Liberia mwezi Desemba mwaka 1989. Vita hivyo vilivyodumu kwa miaka 14 vimesababisha vifo vya watu zaidi ya laki mbili, watu wengi kukimbia makazi yao na kuzorotesha sana uchumi wa nchi hiyo. Mbali na hayo vita hivyo vya nchini Liberia vimesababisha migogoro ya nchi za jirani na kuathiri vibaya amani na maendeleo ya uchumi ya sehemu ya Afrika ya magharibi. Mwezi Agosti mwaka 2003, rais wa zamani wa nchi hiyo Charles Taylor alilazimika kujiuzulu na kukimbilia Nigeria kutokana na shinikizo kubwa la majeshi yaliyoipinga serikali, vita vya nchini Liberia vikamalizika. Baada ya hapo makundi mbalimbali ya kisiasa nchini humo yalisaini mkataba wa amani na kuanzisha serikali na bunge la muda zilizoshirikisha watu wa makundi mbalimbali. Mwezi Oktoba mwaka jana uchaguzi mkuu wa kwanza ulifanyika nchini Liberia, ambapo Bibi Ellen Johnson-Sirleaf alifanikiwa kuingia katika raundi ya pili ya upigaji kura.
Wachambuzi wanaona kuwa kuanzishwa serikali mpya nchini Liberia baada ya kumalizika vita, ni hatua muhimu ya kihistoria katika mchakato wa amani nchini humo. Hatua hiyo ina maana muhimu katika kuleta amani na utulivu nchini, kuanzisha ujenzi mpya baada ya vita na kutuliza hali ya sehemu yote ya Afrika ya magharibi. Lakini wachambuzi pia wanaeleza kuwa mchakato wa amani nchini Liberia utakabiliwa na changamoto nyingi kali, na serikali mpya ya nchi hiyo itakabiliwa majukumu makubwa.
Kwanza, serikali mpya inakabiliwa suala moja muhimu la kulinda amani na utulivu vilivyopatikana baada ya kumalizika kwa vita. Tangu kumalizika kwa vita hivyo, kulikuwa na askari karibu laki 1 wa makundi mbalimbali walionyang'anywa silaha. Lakini bado kuna baadhi ya watu wa makundi ya zamani yaliyokuwa yanaipinga serikali, ambao bado hawajasalimisha silaha zao, jambo ambalo ni tishio kubwa kwa amani na utulivu wa Liberia hata kwa usalama wa nchi jirani.
Pili, Ingawa rais wa zamani Charles Taylor ameishi kwa miaka zaidi ya miwili katika nchi ya nje, lakini waungaji mkono wake walioko nchini Liberia ni wengi. Endapo serikali mpya itamrejesha haraka Taylor na kumfungulia mashitaka kwenye mahakama ya Umoja wa Mataifa iliyoko Sierra Leone, basi ni vigumu kulinda hali ya utulivu iliyopatikana nchini Liberia.
Tatu ingawa mgogoro uliotokea katika uchaguzi mkuu nchini Liberia umetulia, lakini mgongano wa maslahi kati ya makundi mbalimbali bado upo. Na jinsi serikali mpya atakayoiongoza Bibi Ellen Johnson-Sirleaf itakavyopunguza mgongano wa makundi mbalimbali kwa kuteua viongozi wa serikali mpya, pia ni jambo linalofuatiliwa na watu.
Nne, ujenzi mpya wa taifa baada ya kumalizika kwa vita ni jukumu muhimu zaidi linaloikabili serikali mpya. Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mingi vimefanya miundo mbinu ya maji, umeme na mawasiliano kuwa katika hali mbaya sana. Ukosefu wa ajira umefikia zaidi ya 85%. Endapo misaada ya kimataifa haitafikishwa nchini humo, basi ujenzi mpya wa nchi hiyo utaathiriwa vibaya, hali ambayo itatishia moja kwa moja utulivu wa nchi hiyo.
|