Kikundi cha upinzani chenye silaha, the Movement for the Emancipation of the Niger Delta, tarehe 18 kilitangaza kuwa kikundi hicho kitafanya mashambulizi kwa mashirika yote ya nchi za nje yanayochimba mafuta kwenye sehemu ya kusini nchini Nigeria. Wachambuzi wanaona kuwa kauli hii inaashiria kwamba hali ya usalama itazidi kuwa mbaya katika sehemu hiyo.
Barua ya wazi ya kutoka kwa kikundi hicho kwa vyombo vya habari inasema, kimekwisha fanya mashambulizi kwa visima vya mafuta vya Shirika la Total la Ufaransa na Shirika la Agip la Italia, na kitashambulia kisima cha Shirika la Chevron la Marekani. Kikundi hicho kilisema, shabaha zake zikiwa ni kushambulia visima, mabomba ya kusafirisha mafuta, vifaa vya kusafisha mafuta, matangi ya kuwekea mafuta pamoja na wafanyakazi na jamaa zao wa mashirika hayo, lengo la mwisho ni kuizuia serikali ya Nigeria isisafirishe mafuta kwa nchi za nje.
Majuma kadhaa yaliyopita, kikundi cha Movement for the Emancipation of the Niger Delta kilifanya mashambulizi mfululizo kwenye visima vinne vya Shirika la Shell ambalo ni kubwa kuliko mashirika mengine ya nchi za nje nchini Nigeria, na kiliwateka nyara wafanyakazi wanne kutoka Ulaya. Hivi sasa shirika hilo limewaondoa wafanyakazi wake zaidi ya 30 kutoka huko na linafikiria kuwaondoa wafanyakazi wote wenyeji. Mashambulizi yalisababisha Shirika la Shell kupunguza uzalishaji wa mafuta kwa mapipa laki 2.6 kwa siku ambayo ni asilimia 10 ya mafuta yote yanayozalishwa nchini Nigeria.
Nigeria inazalisha mafuta mapipa milioni 2.6 ya mafuta kwa siku, ni nchi inayozalisha mafuta kwa wingi barani Afrika na ni nchi ya sita ya kusafirisha mafuta kwa nchi za nje duniani, moja kwa tano ya mafuta yanayotumika Marekani yanatoka Nigeria. Sehemu ya delta ya Niger kusini mwa Nigeria ni sehemu muhimu kwa uzalishaji wa mafuta na gesi nchini humo, ambapo karibu mafuta yote na gesi yote yanazalishwa huko, mapato zaidi ya asilimia 90 ya Nigeria yanapatikana kutoka huko.
Lakini, utajiri wa mafuta na gesi haujawahi kuwaletea wananchi wa Nigeria manufaa yoyote. Kinyume chake migogoro haikuwahi kusimama kati ya makabila na mashirika katika mapambano ya kugombea haki ya kusimamia maliasili ya mafuta na gesi. Kutokana na takwimu, watu zaidi ya elfu moja wanakufa kila mwaka katika migogoro ya kisilaha katika sehemu ya delta ya Niger. Kutokana na msukosuko wa muda mrefu, maendeleo ya uchumi na jamii kwenye sehemu hiyo yanaathiriwa vibaya, na imekuwa sehemu iliyo nyuma kabisa kiuchumi nchini Nigeria, asilimia 70 ya watu wa huko wanaishi chini ya mstari wa umaskini kabisa, wakazi wa huko mara kwa mara wanafanya mashambulizi ya silaha kwa mashirika ya nchi za nje yanayochimba mafuta na kuharibu mazingira.
Wachambuzi wanaona kuwa kiasi kidogo katika bajeti ya serikali kinachotumika kwenye sehemu hiyo ambayo ni sehemu muhimu inayozalisha mafuta ni chanzo muhimu cha kusababisha mashambulizi ya kisilaha. Na sababu nyingine ni kwamba ili kujipatia maslahi, mashirika ya nchi za Magharibi yalichukua hatua mbalimbali ili kuvutia na kufarakanisha nguvu za aina mbalimbali za wenyeji, hatua hizo zimechangia kupata nguvu kwa kikundi haramu chenye silaha, na mwishowe hatua hizo zimeleta matokeo ya "kujipalia moto".
Idhaa ya kiswahili 2006-01-19
|