Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-01-19 16:46:44    
Wanawake wa China wapenda vitu vya anasa vyenye chapa maarufu

cri

Katika miaka ya karibuni, kutokana na kuongezeka kwa mapato, baadhi ya Wachina ambao wengi wao ni wanawake vijana wameanza kufuatilia vitu vya anasa vyenye chapa maarufu. Na mwenendo huo umeleta faida kubwa kwa uuzaji wa bidhaa nyingi zenye chapa maarufu duniani kwenye soko la China.

Bi. Chen Qianqian ni msichana mrembo, anafanya kazi katika kampuni moja ya Guangzhou, mkoani Guangdong, kusini mashariki mwa China, kila wikiendi yeye anapenda kutembelea maduka yanayouza bidhaa zenye chapa maarufu. Akisema:

"Mimi napenda kutembelea maduka yanayouza bidhaa zenye chapa maarufu kama vile mkoba wa Beli, marashi ya Chanel, na kipodozi cha Lancome. Ingawa vitu hivyo vinauzwa kwa bei kubwa, lakini ni vitu vyenye sifa bora."

Kama alivyo Bi. Chen Qianqian, hivi sasa wanawake vijana wengi wa China wanapenda kununua bidhaa zenye chapa maarufu na zenye bei kubwa. Ukitembelea mitaani utawakuta wasichana wengi waliobeba mikoba yenye chapa maarufu na saa maarufu zilizotengenezwa nchini Uswisi. Ukitembelea maduka makubwa ya Beijing, Shanghai na miji mingine nchini China utaona wanawake vijana ni watumiaji muhimu wa vitu vya anasa. Kwa mfano watumiaji wengi wa kipodozi cha Lancome ni wanawake wenye umri wa miaka 25 hadi 34. Ripoti moja ya uchunguzi inasema kuwa, mwaka 2004 watumiaji wa China ambao wengi wao ni wanawake vijana, walinunua asilimia 12 ya vitu vya anasa duniani.

Kwa nini vitu vya anasa vinawavutia wanawake vijana namna hii? Bi. Wu Qin anayependa bidhaa za chapa maarufu alisema:

"Kwa kawaida utengenezaji wa bidhaa za chapa maarufu ni mzuri sana, tena huduma za bidhaa hizo baada ya kuuzwa ni za kuaminika. Kwenye maduka yanayouza bidhaa za chapa maarufu huwa hakuna wateja wengi kama ilivyokuwa katika maduka ya kawaida, hivyo yanawavutia watu wenye pesa na wanaopenda vitu vya anasa."

Mifuko, mikoba, marashi, saa na nguo zenye chapa maarufu huuzwa kwa Yuan elfu kadhaa au zaidi, lakini wanawake vijana wakikuta vitu hivyo, wale wanaopenda huvinunua bila kujali matumaini makubwa.

Hivi sasa wasichana wa China wanaonunua vitu vya anasa wanaweza kugawanyika kwa aina mbili, wa aina moja ni wale matajiri wanaopenda kupata huduma bora ili kukwepa misongamano ya watu; na wa aina nyingine ni wale wanaofanya kazi katika kampuni, hasa kampuni zilizowekezwa na wafanyabiashara wa nchi za nje, labda itawagharamu mshahara wa mwezi mmoja kwa ajili ya kununua kitu kimoja cha anasa.

Uchunguzi uliofanywa kwa njia ya mtandao wa internet unaonesha kuwa, baadhi ya wanawake vijana hata wananunua vitu vya anasa kwa kuomba mkopo kutoka kwa benki. Na hamu kubwa ya wanawake hao kununua vitu vya anasa imeleta faida kubwa kwenye mauzo ya bidhaa nyingi za chapa maarufu duniani, na kwa upande mwingine kampuni zinazozalisha bidhaa hizo huvutiwa kuongeza uwekezaji nchini China.

Duka la Xidan liko kwenye mtaa maarufu wa biashara wa Xidan mjini Beijing, naibu meneja mkuu wa duka hilo Bwana Zhou Jingtang alisema, mauzo ya vitu vya anasa ya duka hilo ni mazuri. Kwa mfano, duka la Xidan limekuwa na kaunta kadhaa maalum zinazouza saa za chapa maarufu za kimataifa, kama vile Omega, Longines na Tissout. Akisema:

"Hivi sasa saa za mkono zenye chapa maarufu zinanunuliwa sana, kwa mfano thamani ya mauzo ya saa za Omega inafikia Yuan milioni moja kwa mwezi, saa moja ya dhahabu ya Omega inauzwa kwa Yuan zaidi ya laki moja, lakini zinawafurahisha sana wateja."

Bwana Zhou alisema hivi sasa wafanyabiashara wengi wa saa na saa za mkono wanatarajia kuanzisha kaunta maalum katika duka la Xidan. Kaunta ya kuuza saa za mkono za Rolex itafunguliwa muda mfupi ujao, na bidhaa za chapa nyingine kadhaa za saa za mkono zenye mitindo maalum pia zitaingia katika duka hilo.

Vitu vya anasa vinavyopendwa na wanawake vinaleta faida kubwa kwenye soko la China. Kwa mfano vipodozi aina ya Lancome vilivyotengenezwa na kampuni ya O'real ya Ufaransa vimeweka kaunta zaidi ya 60 nchini China, mauzo yake yanatia fora duniani. Na thamani ya mauzo ya vipodozi vya Lancome huchukua nafasi ya kwanza katika maduka 10 makubwa yanayouza vipodozi nchini China. Kutokana na faida kubwa, hivi sasa kampuni ya O'real inazingatia kuongeza uwekezaji nchini China.

Wataalamu wa elimu ya jamii wanachambua kuwa, hali ya wanawake wa China kupenda kununua vitu vya anasa inatokana na maendeleo makubwa ya uchumi na jamii, na kuinuka kwa kiwango cha maisha. Wanawake vijana wengi hawana mzigo mkubwa wa kifamilia, hivyo wanaweza kumudu ununuzi wa vitu vya anasa. Lakini profesa Zhou Xiaozheng kutoka taasisi ya utafiti wa sheria na jamii ya chuo kikuu cha umma cha China aliainisha:

"Ni rahisi kwa wanawake kuchochewa hamu ya kununua vitu vya anasa, si kama tu kutokana na sifa bora ya vitu vyenyewe, bali pia ni kutokana na kuwa, vitu vya chapa maarufu vinaweza kukidhi mahitaji yao ya kihisia."

Profesa Zhou alisema hivi sasa soko la vitu vya anasa nchini China bado liko katika kipindi cha mwanzo, watumiaji huvutiwa na bidhaa mpya za kisasa, huu ni mchakato wa lazima wa maendeleo ya jamii. Inaaminika kuwa kutokana na maendeleo ya uchumi na jamii, hamu ya wachina ya kununua vitu vya anasa itatulia na kupevuka siku hadi siku.

Idhaa ya kiswahili 2006-01-19