Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-01-24 19:37:34    
Mkutano wa wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika wafuatilia umoja na utulivu wa Afrika

cri

Mkutano wa 6 wa wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika ulifunguliwa tarehe 23 huko Khartoum, mji mkuu wa Sudan, wawakilishi wa nchi wanachama 53 wakiwemo wakuu wa nchi na viongozi wa serikali wapatao kiasi cha 30, watajadili masuala ya usalama, maendeleo, migogoro ya kikanda ya Afrika, mchakato wa utandawazi na uendelezaji wa utamaduni na elimu barani Afrika.

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika amabaye ni rais Olusengun Obasanjo wa Nigeria, rais Omar al Bashir wa nchi mwenyeji wa mkutano huo wa mwaka huu, rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini, kiongozi wa Libya Muammar Kadhafi, rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, mshauri maalumu wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mambo ya Afrika Bw. Mohamed Sahnoun na katibu mkuu wa Umoja wa nchi za Kiarabu Bw. Amr Moussa walishiriki kwenye sherehe ya ufunguzi ya siku hiyo.

Katika siku ya kwanza ya mkutano, masuala yaliyozingatiwa zaidi ni kuimarisha umoja wa nchi za Afrika na ulinzi wa amani na utulivu wa bara la Afrika. Kwenye ufunguzi wa mkutano, mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ambaye ni rais Olusegun Obasanjo wa Nigeria alisema, maendeleo ya uchumi na jamii ya nchi mbalimbali za Afrika hayatatimizwa bila kujitahidi kupunguza hali ya wasiwasi ya kanda hiyo na kumaliza mapema iwezekanavyo migogoro na ghasia kwenye sehemu hiyo. Alisema katika mwaka uliopita, kutokana na jitihada za nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, hali ya usalama katika nchi za Guinea Bissau, Togo, Burundi, Liberia na Cot d'ivoire imeboreshwa kwa mfululizo, mchakato wa amani unapiga hatua, jambo ambalo linaonesha nia na uwezo wa nchi za Afrika wa kulisaidia bara lao kuondokana kabisa na migogoro. Alisema mchakato wa amani nchini Somalia umekwama, mgogoro wa mpaka kati ya Ethiopia na Eritrea haujatatuliwa, na suala la Darfur la Sudan ni changamoto kali inayolikabili bara la Afrika. Amezitaka pande mbalimbali husika zitoe mchango katika kuboresha hali ya usalama barani Afrika.

Rais Omar al-Bashir wa Sudan, ambayo ni nchi mwenyeji wa mkutano huo, alipotoa hotuba kwenye ufunguzi wa mkutano wa siku hiyo alisema, Sudan inapenda kushirikiana na nchi jirani pamoja na nchi wanachama wengine wa Umoja wa Afrika ili kulinda amani na utulivu wa barani Afrika. Rais Bashir alisema, Sudan inatarajia Umoja wa Afrika utaendelea kutekeleza jukumu lake la kulinda amani kwenye sehemu ya Darfur, kwani ni kwa kufanya hivyo tu, ndipo wanaweza kuthibitisha kuwa Afrika ina uwezo wa kutatua yenyewe matatizo ya ndani.

Mshauri maalumu wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mambo ya Afrika Bw. Mohamed Sahnoun kwenye mkutano huo alisoma barua ya pongezi ya Bw. Kofi Annan akisema, Umoja wa Mataifa utaendelea kuwa na ushirikiano mkubwa na Umoja wa Afrika, kusaidia kuboresha hali ya usalama kwenye sehemu ya Darfur na kuendelea kuhimiza mchakato wa amani nchini Sudan.

Suala lingine muhimu lililofuatiliwa sana na watu kwenye mkutano wa ufunguzi ni kuhusu Sudan kuwa nchi mwenyekiti wa mkutano ujao wa Umoja wa Afrika au la. Kutokana na mazoea ya Umoja wa Afrika, nchi mwenyeji wa mkutano wa Umoja wa Afrika itakuwa chaguo la kwanza la kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika wa awamu mpya. Lakini katika muda wa karibu miezi miwili iliyopita, wasiwasi ulitokea katika uhusiano kati ya Sudan na Chad, aina, mazungumzo ya amani ya Darfur nchini Sudan bado hayajapata maendeleo, hivyo hivi sasa kuna tofauti kubwa ya maoni miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kuhusu Sudan kuwa nchi mwenyekiti wa Umoja wa Afrika wa awamu mpya.

Ofisa wa Umoja wa Afrika tarehe 23 huko Khartoum alidokeza, ili kulinda umoja wa nchi za Afrika, Umoja wa Afrika umeamua kufanya mazungumzo ya dharura baada ya kumalizika kwa mkutano wa siku hiyo ambayo yatakayoshirikisha viongozi wa nchi 5 za Misri, Gabon, Zimbabwe, Djibouti na Burkina Faso.