Mkutano wa 6 wa wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika, ambao ulifanyika kwa siku 2 huko Khartoum, mji mkuu wa Sudan, ulifungwa tarehe 24. Katika mkutano huo wakuu wa nchi, viongozi wa serikali pamoja na wawakilishi wapatao 36 walishiriki kwenye majadiliano kuhusu masuala ya utamaduni, elimu, ushirikiano kati ya Umoja wa Afrika na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, na waliafikiana kwenye nyaraka nyingi. Vyombo vya habari vinaona kuwa huo ni mkutano wenye ufanisi mkubwa. Tuchukue mfano wa uchaguzi wa nchi mwenyekiti wa awamu mpya wa Umoja wa Afrika, mkutano huo umepiga hatua moja muhimu ya kuhimiza Umoja wa Afrika utatue wenyewe masuala yake na kuhimiza mchakato wa utandawazi wa uchumi wa Afrika.
Katika siku za mwanzo za mkutano huo, namna ya kuchagua nchi mwenyekiti wa awamu mpya wa Umoja wa Afrika ilikuwa suala moja lenye matatizo, ambalo iliathiri ratiba ya mkutano huo. Kutokana na mazoea yake, nchi mwenyeji wa mkutano wa wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika, Sudan ingekuwa nchi mwenyekiti wa awamu mpya wa Umoja wa Afrika, lakini kutokana na uhusiano wa wasiwasi kati yake na jirani yake Chad uliokuwepokwa kwa karibu miezi miwili iliyopita, Chad inapinga kithabiti Sudan kuwa mwenyekiti wa awamu mpya wa Umoja wa Afrika. Aidha viongozi wa makundi yanayoipinga serikali ambao wanashiriki kwenye mazungumzo ya amani yanayofanyika huko Abuja, mji mkuu wa Nigeria chini ya usimamizi wa Umoja wa Afrika, walisema endapo Sudan ingechaguliwa kuwa nchi mwenyekiti wa Umoja wa Afrika wangejitoa kwenye mazungumzo ya amani ya Abuja. Kati ya nchi wanachama wengine wa Umoja wa Afrika pia kuna migongano mikubwa kuhusu suala la nchi mwenyekiti na ni vigumu kuwapatanisha.
Kutokana na kukabiliwa na shinikizo la ndani na nje pamoja na tofauti za maoni, mkutano wa Umoja wa Afrika tarehe 23 uliamua kuunda kamati maalumu inayoshirikisha wakuu wa nchi au viongozi wa serikali za nchi saba za Misri Djibouti, Tanzania, Zimbabwe, Botswana, Senegal na Gabon kujadili na kufanya uamuzi kuhusu suala la nchi mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na kufanya suala hilo lipitishwe kwenye mkutano. Tarehe 24 mkutano wa Umoja wa Afrika uliamua kuwa Congo Brazzaville iwe mwenyekiti wa Umoja wa Afrika wa sasa, na Sudan itakuwa mwenyekiti wa awamu ijayo, na wadhifa huo utachukuliwa zamu kwa kanda mbalimbali za Umoja wa Afrika.
Wachambuzi wanaona kuwa katika mkutano wa mwaka huu, uchaguzi wa nchi mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ulionekana kama ni suala kuhusu utaratibu, lakini hali halisi ni kwamba suala hilo ni muhimu sana kwa kufanikisha mkutano wa Umoja wa Afrika wa mwaka huu na kuhimiza mchakato wa utandawazi wa Afrika.
Kwanza hivi sasa utandawazi wa uchumi umeendelezwa sana, bara la Afrika linakabiliwa na majukumu makubwa ya kuondokana na migogoro ya vita, utokomezaji wa hali ya umaskini na kuleta ustawi wa uchumi. Hivyo utatuzi mzuri wa suala la nchi mwenyekiti wa Umoja wa Afrika unaonesha nia ya nchi za Afrika ya kuimarisha umoja, kutenda vitendo kwa pamoja na kulinda amani na utulivu wa Afrika.
Pili, utatuzi wa suala la nchi mwenyekiti wa Umoja wa Afrika utahimiza mchakato wa amani na usuluhishi wa mgogoro nchini Sudan. Rais Omar Al Bashir wa Sudan amesema, serikali ya Sudan ina imani ya kutatua kwa njia ya amani suala la Darfur kabla ya mwaka 2007.
Tatu, viongozi wa nchi za Umoja wa Afrika wamechagua Congo Brazzaville iwe mwenyekti wa sasa wa Umoja wa Afrika na kuchagua Sudan kuwa mwenyekiti wa awamu ijayo kutokana na msimamo wa kuimarisha umoja wa nchi za Afrika na kulinda amani na utulivu wa bara la Afrika, jambo ambalo limeonesha nia ya viongozi wa nchi za Umoja wa Afrika ya kutatua matatizo ya Afrika kwa kutegemea busara na uwezo wao.
Wachambuzi wamesema, nchi za Afrika zinatakiwa kukabili masuala mawili makubwa ya amani na maendeleo kwenye msingi wa kuondoa tofauti zao, kuimarisha umoja na kuhimiza utandawazi barani Afrika.
|