Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-01-26 17:12:35    
Sehemu ya hifadhi ya kimaumbile ya Qiangtang ya China

cri

Sehemu ya hifadhi ya kimaumbile ya Qiangtang iliyoko kwenye sehemu ya mpaka kati ya mkoa unaojiendesha wa Tibet, mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Uygur na mkoa wa Qinghai ni moja ya sehemu ambazo mazingira ya viumbe yamehifadhiwa vizuri duniani, na yenye aina nyingi za wanyama na mimea pori.

Sehemu ya hifadhi ya kimaumbile ya Qiangtang ina eneo hekta milioni 29.8. Kwa lugha ya kitibet, maana ya neno la "Qiangtang" ni mbuga pori ya kaskazini isiyokuwa na wakazi. Naibu mkuu wa idara ya kilimo na ufugaji ya sehemu ya Ali mkoani Tibet Bw. Germa alisema:

"Katika sehemu ya hifadhi ya kimaumbile ya Qiangtang kuna nyati, paa wa kitibet, mbuzi wenye kichwa kikubwa, na wanyama wanaokula nyama kama vile mbwa mwitu na mbweha, wanyama wengi waishio huko ni paa wa kitibet na yak pori. Paa wa kitibet wanaishi na kuhamahama kwa makundi, kundi moja la paa wa kitibet huwa na paa zaidi ya elfu kadhaa, majira ya kuzaliana kwa paa yanapowadia, paa wote wanahamia mahali maalum pa kuzaliana bila kujali matatizo gani yatakayowakabili njiani.

Kwenye sehemu ya hifadhi ya kimaumbile ya Qiangtang isiyokuwa na wakazi na isiyokuwa na mwisho wa upeo wa macho, makundi ya mbuzi na punda pori wanaonekana hapa na pale, ndege weupe wanarukaruka juu ya ziwa, lakini jambo la kusikitisha ni kwamba, waandishi wa habari walipotembea kwa gari ndani ya sehemu hiyo walishindwa kuwaona paa wa kitibet.

Katika miaka ya 90 ya karne iliyopita, katika sehemu ya hifadhi ya kimaumbile ya Qiangtang, kila mwaka shughuli za ujangili zinatokea mara kwa mara, na paa wa kitibet walikuwa ni lengo muhimu la ujangili huo, kwa sababu manyoya ya paa wa kitibet yana thamani kubwa kwenye soko la kimataifa. Kwa mfano skafu moja iliyotengenezwa kwa manyoya ya paa wa kitibet inauzwa kwa dola za kimarekani zaidi ya 3000, ambapo ngozi moja ya paa wa kitibet inauzwa Yuan 400 hadi 500 nchini China, na bei yake itakuwa maradufu kwenye soko la kimataifa.

Mwaka 1998, China iliifanya sehemu ya Qiangtang kuwa sehemu ya hifadhi ya kimaumbile ya kitaifa, ilipiga marufuku shughuli zote za uwindaji, na kutuma polisi wakilinda misitu kwa kushirikiana na kikosi cha kupambana na shughuli za ujangili cha huko. Bwana Nimajiabu anayependa wanyama tokea utotoni ni mmoja wa polisi hao.

Mwezi Juni ni wakati wa majira ya kuzaliana kwa paa wa kitibet, siku moja, Bw. Nimajiabu na wenzake wawili waliingia katika sehemu isiyo na wakazi na yenye paa wengi wa kitibet kutekeleza jukumu, wakati huo yalikuwa ni majira ya mvua, lori walilokuwa wakisafiria lilikwama njiani, walipaswa kuacha lori hilo na kutembea kwa miguu kwa kilomita 50 na kufika mahali walikokuwa wanakwenda, kwa jumla iliwachukua muda wa saa 10.

Hata hivyo Bwana Nimajiabu alisema, hawaogopi mazingira magumu ya kazi, linalowasumbua ni lazima wawe na tahadhari kwa mashambulizi kutoka kwa majangili. Akisema:

"Mwaka 2003 nilipotekeleza jukumu kwenye soko moja niligundua ngozi moja ya paka mwitu katika duka moja, na kuitaifisha. Mwenye ngozi hiyo alinichukia sana, na katika majira ya mchipuko ya mwaka 2004, aliponikuta kwenye ukumbi wa kucheza ngoma alinisogelea na kunikata mkono kwa kisu."

Bw. Nimajiabu alisema, nyumbani yeye kamwe hazungumzi kuhusu hatari ya kazi yake, ili wazazi wake na mke wake wasije kuwa na wasiwasi juu yake. Katika miaka ya hivi karibuni, Bw. Nimajiabu na wenzake wamekamata ngozi nyingi za wanyama pori waliopigwa marufuku kuwindwa na bunduki zaidi ya 40.

Naibu mkuu wa idara ya kilimo na ufugaji ya wilaya ya Gaize Bwana Germa alisema:

"Zamani, baadhi ya wafugaji waishio kwenye sehemu ya kaskazini mwa Tibet waliishi kwa kuwinda wanyama pori. Ili kuhifadhi wanyama pori, katika miaka ya karibuni, serikali ya China ilitunga sheria kupiga marufuku shughuli za uwindaji, na kueneza sheria hizo miongoni mwa wakazi wa huko. Hivi sasa wenyeji wa huko wamekuwa na mwamko mzuri wa kuhifadhi wanyama pori."

Katika miaka ya karibuni, idadi na aina za wanyama pori kwenye sehemu ya hifadhi ya kimaumbile ya Qiangtang imeongezeka kidhahiri, lakini hali hiyo pia imeleta matatizo kadhaa kama vile kupungua kwa mbuga za majani, na kuota kwa aina nyingi za majani yenye sumu yanayostawi siku hadi siku. Zaidi ya hayo, punda pori na wanyama wengine pori wanagombea majani na mifugo na kuharibu vibaya mbuga za majani. Hali hiyo imefuatiliwa sana na serikali ya mitaa. Bw. Germa akisema:

"Japokuwa serikali kuu ya China imeongeza fedha kwa sehemu ya hifadhi ya kimaumbile ya Qiangtang, fedha hizo bado haitoshi. Ikiwa tunaweza kuendeleza shughuli za utalii ndani ya sehemu hiyo, si kama tu tunaweza kuwafahamisha watu wa nje hali ya sehemu ya hifadhi ya kimaumbile, bali pia tutaongeza mapato kutokana na utalii, na kuvutia msaada wa kimataifa."

Idhaa ya kiswahili 2006-01-27