Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-01-26 17:17:23    
Wachina wafanya maandalizi ya kusherehekea sikukuu ya Spring kwa furaha

cri

Tarehe 29 Januari ni sikukuu ya Spring-yaani sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa kichina, ambayo ni sikukuu muhimu kabisa nchini China. Kabla ya kufika kwa sikukuu hiyo, lakini wachina waishio mijini na vijijini wameanza pilikapilika za maandalizi, hasa katika sehemu ya vijijini, kwa sababu sasa ni kipindi cha mapumziko ya kilimo, hivyo kazi kubwa kwa wakulima kwa sasa ni kufanya maandalizi ya kusherehekea mwaka mpya.

Katika kijiji cha Donghan kilichoko karibu na Xi'an, mji mkuu wa mkoa wa Shanxi, kaskazini magharibi mwa China, kundi la wakulima kumi kadhaa walikuwa wanafanya mazoezi ya michezo ya sanaa, baadhi yao walipiga ngoma na filimbi, na wengine walicheza ngoma ya Yanggo, ilikuwa imejaa hali ya shamrashamra. Wakulima hao watafanya maonesho ya michezo ya sanaa ili kusherehekea sikukuu ya Spring.

Familia nyingi za kijiji hicho zimefanya maandalizi kwa ajili ya sikukuu ya Spring: kwa mfano kupaka rangi upya kwenye nyumba zao, kununua picha na karatasi ndefu zilizoandikwa maneno ya kusherehekea mwaka mpya wa jadi, aina mbalimbali za picha zinazoweza kubandikwa kwenye madirisha, ambazo zote zinaonesha matumaini yao kwa neema na maisha bora ya mwakani. Kwa mujibu wa utaratibu wa kalenda ya jadi ya kichina, mwaka huu ni mwaka wa "mbwa", hivyo sura inayopendeza ya mbwa huonekana kwenye picha za mapambo zilizobandikwa na kila familia.

Mzee Ma Hongzhi mwenye umri wa miaka 70 alisema, mwaka huu familia yake itasherehekea sikukuu ya Spring kwa kufuata desturi za jadi. Akisema:

"Kabla ya mkesha wa sikukuu ya Spring, maandalizi yote yanakuwa yamemalizika. tumesafisha nyumba, kuandaa vyakula vya nyama, mayai na mboga za aina mbalimbali. Baada ya kuingia mwezi wa kwanza wa jadi, hatutapika mikate kwa siku kadhaa."

Familia ya mzee Ma Hongzhi inaamua kuandaa vyakula vyote vitakavyotumiwa katika sikukuu za Spring, hivyo wataweza kusherehekea sikukuu kwa furaha. Bila kufanya kazi za nyumbani Familia ya mzee Ma ina watu 7 wa vizazi vitatu, watakula Jiaozi katika mkesha wa sikukuu ya Spring kama ilivyokuwa desturi. Watoto wanatarajia kwa shauku kubwa kufika kwa mkesha wa sikukuu ya Spring, kwani usiku huo watapewa zawadi ya fedha, na kurusha fataki.

Wanavijiji wa China wanafuata desturi hizo za jadi mwaka hadi mwaka. Lakini kutokana na maendeleo ya jamii na kuinuka kwa kiwango cha maisha, katika miaka miwili ya karibuni mila za wanavijiji wa mkoani Shanxi kusherehekea sikukuu ya Spring zimekuwa zinabadilika, kwa mfano, siku zamani, watu walikuwa hawaondoki nyumbani katika siku 15 za mwanzo, lakini kutokana na idadi ya wanavijiji wanaotafuta kazi za vibarua nje kuongezeka, hivi sasa baadhi ya wanavijiji wanafunga mizigo ya kuondoka nyumbani baada ya siku chache tu za kusherehekea sikukuu ya Spring. Baadhi ya wakulima wanaofanya kazi mijini wanawaalika wazazi wao kusherehekea sikukuu ya Spring mijini.

Sasa tunakuja kuangalia jinsi wakazi wa mijini wanavyoandaa kusherehekea sikukuu ya Spring. Hivi sasa miji yote nchini China imejaa furaha, ambayo maduka mengi yamepambwa kwa mapambo ya sikukuu, kwenye mikahawa simu za kuagiza chakula cha usiku wa kuamkia mwaka mpya wa jadi zinaita mara kwa mara. Kutokana na kuongezeka kwa mapato, wakazi wengi wa mijini wanakula chakula cha mkesha wa mwaka mpya mikahawani badala ya kupika wenyewe.

Licha ya kula chakula kizuri cha mkesha wa mwaka mpya mikahawani, katika kipindi cha sikukuu ya Spring, wakazi wengi pia wamepanga kutalii nje. Bi. Gao Xiunu kutoka mji wa Tianjin atakwenda Hong Kong kusherehekea mwaka mpya pamoja na wanafamilia wake na marafiki. Akisema:

"Ni jambo la furaha sana kwa familia nzima kutalii. Siku za kawaida sisi sote tunashughulika na kazi au masomo, hatuna fursa nyingi za kutalii pamoja, na kumpeleka mtoto atalii na kufahamu mambo ya duniani."

Mwaka huu itakuwa vigumu kidogo kwa wakazi wa sehemu ya Jiujiang, mkoani jiangxi, kusini ya China kutokana na kukumbwa na tetemeko la ardhi miezi kadhaa iliyopita. Lakini mwandishi wetu wa habari alipotembelea sehemu hiyo alishuhudia kuwa, hali ya huko ilikuwa nzuri zaidi kuliko alivyofikiria. Kijiji cha Yangqiao cha mji wa Jiujinag ni sehemu iliyokumbwa vibaya na tetemeko la ardhi, zaidi ya nusu ya nyumba za familia 300 za kijiji hicho zilibomoka, wanakijiji walipaswa kuishi katika mahema. Kada mmoja wa huko alisema, chini ya uongozi wa serikali, wako mbioni kuwasaidia wanakijiji kujenga nyumba zao.

Akiingia ndani ya hema ya Bwana Wang Jiaqing na familia yake, mwandishi wetu wa habari hakusikia baridi hata kidogo, kwenye meza kuna televisheni ya rangi, VCD, kwenye kitanda cha watu wawili kuna tandiko. Kwenye "ukuta" wa hema zilibandikwa picha zilizoandikwa "baraka", zikionesha matarajio ya sikukuu na hisia za wenyeji kwa maisha ya siku zijazo. Bw. Wang Jiaqing alisema japo kuwa familia yake ilikumbwa na maafa, lakini amepewa msaada na serikali, hana shida ya chakula na makazi, akisema:

"ingawa tulikumbwa na tetemeko la ardhi, lakini tutasherehekea sikukuu ya Spring kama tulivyofanya siku zote, ila tu tunachelewa kidogo kutayarisha vitu vya kusherehekea mwaka mpya wa jadi."

Mkuu wa serikali ya wilaya alisema, serikali ya huko imewapatia wanakijiji waliokumbwa na maafa matandiko, nguo nzito, mchele na vitu vingine vya kila siku, ili kuhakikisha familia zote zinasherehekea sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China.

Idhaa ya kiswahili 2006-01-27