Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-01-26 20:38:57    
Majengo katika Enzi ya Tang Song na Yuan

cri
Majengo katika Enzi ya Tang

Enzi ya Tang (618-907) ni kipindi ambacho uchumi na utamaduni katika jamii ya kimwinyi nchini China ulifikia kwenye kilele, ufundi na sanaa za ujenzi wa majengo pia zilikuwa zimeendelea sana. Majengo katika Enzi ya Tang yalikuwa makubwa na ya adhama.

Majengo katika Enzi ya Tang yalikuwa ni makubwa, na mpangilio wa fungu la majengo ni wa busara. Katika mji mkuu wa Enzi ya Tang, Chang An (mji wa Xi'an kwa leo), na mji wa Luoyang kuna makasri makubwa na majumba ya maofisa. Mji wa Chang An ulikuwa mji mkubwa duniani katika enzi hiyo, na mpangilio wa majengo yake ulikuwa wa busara kabisa katika miji yote ya China ya kale, ndani ya mji huo kasri la Daming lilikuwa na eneo zaidi ya mara tatu kuliko Kasri la Kifalme la Beijing.

Majengo katika Enzi ya Tang yanaonesha sayansi ya muundo wa mbao, mshikamano baina ya nguzo na maboriti umeonesha ushirikiano mzuri wa nguvu. Ukumbi wa Buddha katika Hekalu la Foguang mlimani Wutaishan umeonesha wazi mtindo wa majengo ya Enzi ya Tang.

Kadhalika, majengo ya matofali na mawe pia yalikuwa yameendelea sana katika Enzi ya Tang, mifano ya majango hayo ni pagoda ya Dayanta, pagoda ya Xiaoyanta na pagoda ya Qianxunta katika mji wa Xi'an.

Majengo katika Enzi ya Song

Enzi ya Song (960-1279) ilikuwa ni enzi iliyodidimia katika siasa na mambo ya kijeshi, lakini uchumi, viwanda vya kazi za mikono na biashara vilikuwa na maendeleo kwa kiasi fulani, na hasa katika sayansi na teknolojia, hali hiyo iliufanya ufundi wa majengo ufikie kiwango kipya. Majengo katika enzi hiyo yalibadilika kuwa madogo na yenye makini ya mapambo badala ya yale ya majengo makubwa na ya adhama ya Enzi ya Tang.

Katika miji ya Enzi ya Song yalitokea maduka kwenye barabara, na maduka yalipangwa kwa aina ya bidhaa, na majengo ya shughuli za zimamoto, mawasiliano, uchukuzi, maduka na madaraja, yote yaliendelea kwa hatua kubwa. Sura ya mji mkuu wa Enzi ya Song, Bianliang, (mji wa Kaifeng kwa leo) ilionesha wazi hali ya biashara katika miji ya Enzi ya Song. Katika enzi hiyo, nchini China majengo makubwa makubwa hayakujengwa sana, lakini mapambo na rangi za majengo yalizingatiwa zaidi. Ukumbi katika hekalu la Jinxi mkoani Shanxi ni mfano wa majengo hayo.

Majengo ya matofali yaliendelea zaidi katika Enzi ya Song, majengo hayo yalikuwa ni pagoda ya dini ya Buddha na madaraja. Pagoda katika hekalu la Huilingsi mkoani Zhejiang, pagoda la Fanta katika mji wa Kaifeng mkoani Henan na daraja la Yongtong wilayani Zhaoxian mkoani Hebei yote yanastahili kuwa kama ni mifano ya majengo ya matofali katika Enzi ya Song.

Uchumi wa Enzi ya Song uliendelea kwa kiasi fulani, katika enzi hiyo, ujenzi wa bustani ulianza kustawi. Ujenzi wa bustani ulitilia mkazo muunganisho wa uzuri wa bandia na wa kimaumbile, bustani katika enzi hiyo ilikuwa inapambwa kwa milima bandia, maji, maua na miti ili kuleta mazingira kama ya kimaumbile.

Katika Enzi ya Song kulikuwa na kitabu cha "Ufundi wa Ujenzi wa Nyumba". Kitabu hiki kinaeleza kanuni za usanifu na ufundi wa ujenzi wa nyumba, ambacho kinaonesha kuwa ujenzi wa nyumba katika Enzi ya Song ulikuwa umefikia kiwango kipya.

Majengo ya Enzi ya Yuan

Enzi ya Yuan (1206-1368) nchini China ilikuwa ni dola la kifalme lililoundwa na watawala wa kabila la Wamongolia, lakini katika enzi hiyo, majengo hayakuwa na maendeleo, na majengo mengi yalikuwa ya kawaida kutokana na kuzorota kwa uchumi na utamaduni.

Mji mkuu wa Enzi ya Yuan, Dadu (sehemu ya kaskazini ya Beijing kwa leo) ni mwanzo wa mji mkuu wa enzi mbili za Ming na Qing, Beijing. Shughuli za ujenzi katika mji mkuu huo zilikuwa hasa katika ujenzi wa majengo ya ukumbi na bustani, Bustani ya Beihai ya leo mjini Beijing ni kumbukumbu halisi ya enzi hiyo.

Katika Enzi ya Yuan dini ilikithiri sana, hasa dini ya Buddha ya madhehebu ya Kitibet, kwa hiyo mahekalu ya dini yalikuwa mengi.

Majengo ya mbao katika Enzi ya Yuan yaliurithi ufundi wa enzi iliyotangulia ya Song, lakini kutokana na uchumi uliokuwa mbaya na uhaba wa magogo, majengo katika enzi hiyo yalikuwa ya kawaida yakilinganishwa na majengo ya Enzi ya Song iwe kwa ukubwa au kwa umakini.

Idhaa ya Kiswahili 2006-01-26