Kutokana na hesabu ya kura isiyokamilika ya tarehe 26, kundi la Hamas limeshinda kwenye uchaguzi kwa viti zaidi ya 70 kati ya viti vyote 132 vya bunge. Hii inamaanisha kwamba kundi la Hamas lililokuwa nje ya bunge limekuwa kundi muhimu katika bunge. Hali hiyo imevutia uangalizi mkubwa wa kimataifa kuhusu mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati. Kuhusu suala hilo mwandishi wetu ametuletea ripoti yake baada ya kufanya mahojiano na mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati Bw. Yin Gang.
Bw. Yin Gang alisema, matokeo ya uchuguzi huo yanashitusha, na sababu za ushindi huo ni nyingi. Alisema,
"Kwanza, Hamas ni kundi kubwa, limefanya mambo mengi ya hisahi nchini Palestina, lilianzisha vituo vya watoto yatima, vituo vya kuwatunza wazee na shule, na watu wanaofanya mashambulizi ya silaha katika kundi hilo ni wachache sana. Tokea mwezi Aprili mwaka jana kundi la Hamas lilianza kuheshimu mkataba wa kusimamisha mashambulizi na kutangaza kuwa linataka kushiriki kwenye uchaguzi wa bunge na kushika njia ya kutatua matatizo kwa njia ya siasa, kwa hiyo limepata imani kubwa zaidi ya watu wa Palestina. Pili, kundi la Hamas linafanya kazi kwa tija kubwa na nidhamu kali. Viongozi wa kundi hilo wana juhudi kubwa ya kazi bila ufisadi. Ikilinganishwa na hali hiyo, Fatah iliyokuwa ikitawala katika miaka kumi iliyopita haikufanya kazi kwa juhudi, na tija ya kazi ni duni." Bw. Yin Gang aliongeza kusema kuwa kuondoka kwa jeshi la Israel kutoka Gaza ni kitendo kilichoamuliwa na upande mmoja tu wa Israel, bali sio matokeo ya mkataba wa pande mbili kati ya mwenyekiti wa mamlaka ya Palestina Bw. Abbas na Israel, kwa hiyo watu wa Palestina wanaamini propaganda ya Hamas kuwa kuondoka kwa jeshi la Israel kunatokana na mapambano ya kijeshi ya Hamas.
Bw. Yin Gang anaona kuwa haitakuwa rahisi kwa Hamas kutoka kundi lenye silaha hadi kuwa chama halali cha kisiasa na kupanda kwenye ulingo wa siasa nchini Palestina. Alisema,
"Hali hiyo inataka Hamas irekebishe sera zake za zamani na kubadilisha kabisa kundi hilo kuwa jumuyia halisi ya kisiasa. Hapo awali ilitangaza kuwa katu haitaacha silaha na kutoitambua Israel. Lakini sasa inaipasa: kwanza itangaze kuitambua Israel, pili iunganishe jeshi lake na jeshi la usalama la Palestina, tatu kufanya mazungumzo kwa msingi wa mkataba wa Oslo na Israel kuhusu suala la amani kwa ardhi. Kama mambo hayo matatu hayatatimizwa serikali itakayoundwa na Hamas haitatambuliwa na jumuyia ya kimataifa."
Hali ambayo Hamas imeshinda uchaguzi inafadhaisha jumuyia ya kimataifa. Bw. Yin Gang alisema,
"Hakika ushindi wa Hamas kwenye uchaguzi utaathiri mambo mengi mfululizo nchini Palestina. Ama Israel ama pande nne za amani ya Mashariki ya Kati, zote zitatoa masharti kwa Hamas katika muda mfupi ujao. Masharti hayo ni: Kwanza, kuitambua Israel. Pili, kuacha silaha. Tatu, kufanya mazungumzo na Israel juu ya msingi uliokuwa umewekwa. Kama kweli Hamas itatangaza kubadili kabisa msimamo wake wa awali na kuwa jumuyia mpya ya kidini, basi Israel haina budi kukubali matokeo ya uchaguzi na kuwasiliana na Hamas. Kama msukosuko ukitokea nchini Palestina na Hamas inashindwa kuunda serikali au serikali haitatambuliwa na jumuyia ya kimataifa, basi Israel itachukua hatua kwa upande mmoja, kuondoa jeshi lake kutoka sehemu zisizo salama za ukingo wa magharibi wa mto Jordan na kuharakisha ujenzi wa ukuta wa kutenganisha pande mbili, "amani" itapatikana kwa kutenganishwa na ukuta na kukata mawasiliano na Palestina ili kukwepa mgogoro. Lakini amani hiyo haitakuwa ya kweli, bali ni ya muda tu."
Idhaa ya kiswahili 2006-01-27
|