Mkutano wa Baraza la Uchumi Duniani umefungwa tarehe 29 huko Davos, Usiwisi. Maendeleo ya uchumi wa China na India na athari zake kwa uchumi wa dunia yalitawala majadiliano yaliyofanyika kwenye mkutano wa mwaka huu wenye kauli mbio isemayo "maendeleo, uvumbuzi na mustakabali". Kwa mujibu wa waandaaji, ajenda na masuala yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo yalihusu hasa mambo ya kiuchumi ili kuepusha mambo ya kisiasa.
Vyombo vya habari vya Ulaya vimechambua kuwa, dunia inafuatilia nchi mbili kubwa zinazoendelea Barani Asia kwa sababu, kwa upande mmoja kuinuka kwa nchi hizo hakika kutaleta athari kubwa kwa siasa na uchumi duniani katika kipindi kirefu. Na kwa upande mwingine, China na India zinazivutia nchi zilizoendelea kwa masoko makubwa na nguvu kazi nafuu wakati bidhaa zao zinauzwa vizuri katika nchi tajiri.
Mwenyekiti wa Baraza la uchumi duniani Bw. Klaus Schwab alisema, kutokana na kuinuka kwa uchumi wa China na India, uti wa mgongo wa uchumi wa dunia umehamia Mashariki kutoka kwa Magharibi. Hata hivyo, ustawi wa nchi hizi mbili si tishio kwa nchi nyingine, bali ni fursa nzuri.
Katika kipindi cha mkutano wa mwaka huu wa Baraza la uchumi duniani, yalifanyika makongamano mawili yakijadili kwa nyakati tofauti "ustawi wa China" na "ustawi wa India". Waliohudhuria makongamano hayo walisema, kuinuka kwa uchumi wa China na India ni mabadiliko muhimu kuliko mengine katika uchumi wa Asia na wa dunia nzima tokea miaka ya 80 ya karne iliyopita, jambo ambalo ni fursa nzuri kwa dunia. Hali kadhalika walieleza imani yao kubwa kwa mustakabali mzuri wa uchumi wa China.
Naibu waziri mkuu wa China Bw. Zeng Peiyan akihutubia mkutano huo tarehe 25 alisisitiza kuwa, hivi sasa uchumi wa China unaendelea vizuri, ambao umepiga hatua kubwa katika kurekebisha mifumo na bado una nguvu kubwa ya kisoko, hali ambayo inatoa nafasi kwa makampuni ya Kichina na Kigeni kuimarisha ushirikiano. Aliwakaribisha wanaviwanda wa nchi mbalimbali waendelee kushiriki na kuunga mkono ujenzi wa kisasa wa China, kuongeza biashara na uwekezaji vitega uchumi ili kupata manufaa ya pamoja katika ushirikiano na makampuni ya China.
Mazungumzo ya kibiashara ya raundi ya Doha pia yalizingatiwa kwenye mkutano huo wa Baraza la uchumi duniani. Mazungumzo hayo yaliyoanza mwaka 2001 yamekwama. Licha ya kufikia makubaliano kadhaa kwenye mkutano wa mawaziri wa Jumuiya ya Biashara Ulimwenguni, WTO uliofanyika huko Hong Kong mwezi Desemba, mwaka jana, lakini bado yanakabiliwa na changamoto kubwa katika kuyatekeleza, hususan jinsi ya kukamilisha mazungumzo yote kabla ya mwishoni mwa mwaka huu kama ilivyopangwa. Mkuu wa Jumuiya ya WTO Pascal Lamy alisema katika mkutano huo kuwa, pande zinazohusika zinapaswa kurudi nyuma kwa kiasi kikubwa zaidi.
Ingawa masuala machache ya kisiasa yalizungumzwa kwenye mkutano wa Davos mwaka huu, suala la nyuklia la Iran lilikuwa la kwaza la kujadiliwa. Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Jack Straw alisema, suala hilo linapaswa kutatuliwa kwa njia ya kidiplomasia badala ya nguvu ya kijeshi. Lakini alionya kuwa suala hilo litawasilishwa kwa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa iwapo Iran haitabadilisha msimamo wake katika suala la usafishaji wa uranium. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier pia alieleza maoni ya namna hiyo. Na kwa upande wa Iran, hivi karibuni ilikubali kufikiria pendekezo la Russia la Iran kuhamishia shughuli za kusafisha uranium nchini Russia, na nchi hizo mbili zinafanya mazungumzo ili kuzishirikisha nchi nyingi zaidi zijiunge na mpango huo wa Russia. Na hii imechukuliwa kuwa ni hatua ya maendeleo.
Mbali na hayo, masuala mengine yaliyozungumzwa kwenye mkutano huo wa Baraza la uchumi duniani yanahusu uchumi wa dunia, eneo la Mashariki ya Kati na Iraq, nishati, bei ya mafuta ya petroli na maafa ya kimaumbile yanayotokea mara kwa mara.
|