Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-01-30 20:52:48    
Mazungumzo kuhusu mbwa katika mwaka wa mbwa

cri

Tarehe 29 mwezi huu ni sikukuu ya mwaka mpya wa Kichina. Katika kalenda ya Kichina kila mwaka unawakilishwa na mnyama mmoja, kwa hiyo kuna jumla ya wanyama kumi na wawili wanaowakilisha miaka 12. Kuanzia tarehe 29 mwezi huu watu wa China watauaga mwaka wa kuku na kuingia katika mwaka mpya wa mbwa.

Katika kalenda ya Kichina kila miaka 12 ni duru moja, na kila mwaka unawakilishwa na mnyama mmoja, jumla kuna wanyama wa aina 12, nao ni panya, ng'ombe, chui, sungura, dragoni, farasi, mbuzi, kima, kuku, mbwa na nguruwe. Matumizi ya majina ya wanyama hao kuwakilisha miaka yalianza katika karne ya 6 K.K. nchini China. Lakini kuna usemi tofauti kuhusu mwanzo wa matumizi ya majina ya wanyama hao kuwakilisha miaka. Baadhi wanasema yalitokana na muungano wa namna ya kuhesabu miaka ya kabila la Wahan na ya makabila madogo madogo. Na wengine wanasema kuwa matumizi hayo yalikuja kutoka India. Pia kuna usemo tofauti kuhusu mfululizo wa wanyama 12.

Usemi unaowavutia watu zaidi unasema kuwa mfululizo huo unatokana na wakati mnyama fulani anapokuwa na shughuli zaidi katika siku. Kuanzia Enzi ya Han, karne ya 3 kabla ya kuzaliwa Kristu, China ilianza kuhesabu majira ya siku kwa vipindi 12. Usiku wa manane ulianzia saa 5 mpaka saa saba usiku, katika muda huo panya huwa na shughuli nyingi, kwa hiyo amepangwa kuwa wa kwanza. Kuanzia saa moja mpaka saa tatu za jioni ni kipindi cha mbwa kulinda usalama, kwa hiyo amepangwa kuwa wa 11. Wakati mwaka wa mbwa unapokaribia, tunawaletea maelezo ya mnyama mbwa katika utamaduni wa China.

Mbwa ni rafiki mkubwa wa binadamu, nchini China kuna mazungumzo mengi na ya kuvutia yanayomhusu mbwa.

Mbwa ni mnyama anayefahamiana na biandamu, kuna hadithi nyingi za siku za kale na za hivi sasa nchini China na hata nchi za nje kuhusu mbwa kuwaokoa na kuwalinda mabwana wao, na kugoma chakula mpaka kufa kutokana na mabwana wao kufariki. Watu wa kabila la Waman katika sehemu ya kaskazini ya China wana mila ya kuheshimu na kuwapenda mbwa, na mila hiyo inatokana na babu yao Nurhachi.

Nurhachi ni mwanzilishi wa Enzi ya Qing, enzi ya mwisho ya kimywinyi na ya kifalme nchini China, aliishi mwishoni mwa karne ya 16 na mwanzoni mwa karne ya 17. Kabla ya Enzi ya Qing ilikuwa ni Enzi ya Ming. Inasemekana kwamba siku moja Nurhachi alifukuzwa na askari wa Enzi ya Ming, alisalimisha roho yake kwa farasi akiwa na mbwa wake aliyekaa naye usiku na mchana, alipofika kwenye genge alikuwa hana njia, basi kapiga mjeledi farasi wake akaruka gengeni pamoja na farasi, kwa kuwa farasi alikuwa chini yake, Nurhachi hakufa lakini alipoteza fahamu. Askari wa Enzi ya Ming walipofika kwenye genge na kuangalia chini wakaona kunguru waliozungukazunguka juu yake, walidhani Nurhachi pengine amekwisha kufa, ili kuondoa wasiwasi wakawasha fungu la majani na kutupa chini wakitaka kumchoma Nurhachi hadi awe majivujivu. Baada ya askari kuondoka, mbwa alikimbilia mto na kulowesha manyoya, kisha akaenda kumzimia moto. Nurhachi alikuwa salama, lakini mbwa wake alikufa kutokana na uchovu na kuchomwa moto.

Baadaye Nurhachi alianzisha Dola la Jin, na dola hilo lilianzisha Enzi ya Qing kuitawala China na mbwa wakawa rafiki wa kabila la Waman. Tokea hapo Waman wamekuwa na mila ya kutoruhusu kuwaua mbwa na kula nyama yao, kuvaa kofia ya ngozi ya mbwa au godoro la ngozi ya mbwa. Watu wa kabila la Waman wanawatunza mbwa kwa makini sana, hata mbwa wakizeeka na kutoweza kulinda usalama pia wanatendewa vema, na baada wao kufa, wanapatiwa mazishi. Kama walivyo watu wa kabila la Waman, makabila ya Wapumi, Walagu na Watibet wanafanya vivyo hivyo.

Mbwa ni watii kwa binadamu. Inasemekana kwamba mwanzilishi wa Enzi ya Han, Liu Bang, aliwaita maofisa wake wenye uaminifu kuwa ni "mbwa wazuri". Katika karne ya 13, mwanzilishi wa Enzi ya Yuan, Genghis Khan, alikuwa na majemadari wanne wakubwa, aliwaita "mbwa wanne". Kadhalika, nchini China kuna usemi wa "kuhudumia mabwana kiaminifu kama farasi na mbwa", na kuna usemi "mbwa hachukii umaskini wa bwana wake". Yote hayo yameonesha kwamba mbwa ni waaminifu wakubwa wa mabwana wake.

Mbwa wanaonelewa kuwa wapole, waaminifu, wakali na wapendwa.

Mwishoni mwa mwaka 2005 na mwanzoni mwa mwaka 2006, nchi nyingi zimetoa stempu za "mwaka wa mbwa" wa Kichina. Stempu ya mwaka wa mbwa iliyotolewa na China ni picha ya mbwa mdogo aliyevaa nguo nyekundu, pamoja stempu za vitu vya sanaa mbalimbali za mbwa vinauzwa na kununuliwa sana zikiwa pamoja na mbwa wa kuashiria utajiri, mbwa wa kulinda mlangoni, sanaa hizo zinachangia furaha ya Wachina wanapokaribisha mwaka mpya wa mbwa.

Idhaa ya Kiswahili 2006-01-30