Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Marekani na Russia ambazo ni pande nne zinazoshiriki katika suala la Mashariki ya Kati, tarehe 30 zimetoa taarifa ikilitaka Kundi la Hamas liitambue Israel na kuacha matumizi ya nguvu. Kundi la Hamas limekataa ombi hilo siku hiyo hiyo, lakini bado linakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka pande mbalimbali tangu lipate ushindi katika uchaguzi wa wiki iliyopita.
Katika taarifa iliyotolewa baada ya kukutana mjini London, pande hizo nne zimeeleza bayana kuwa, vyama vyote vitakavyojiunga na serikali mpya ya Palestina lazima viache matumizi ya nguvu, kuitambua Israel na kukubali mapatano ya amani yaliyofikiwa hapo awali. Kutokana na hatua hiyo, inalibidi kundi la Hamas litoe uamuzi wa kubadilisha sera yake kwa Israel au la.
Kundi la Hamas lilikuwa limetuliza sera yake kuhusu Israel kabla ya kushiriki kwenye uchaguzi. Ilani yake ya uchaguzi haikutaja kanuni ya "kuangamiza Israel na kurudisha ardhi zote katika kando ya magharibi ya Mto Jordan", ambayo ni kanuni inayoshikiliwa na Hamas tangu iasisiwe. Hata hivyo chama hicho kilisema kuendelea na juhudi za kuleta ukombozi wa Palestina kwa njia mbalimbali ikiwemo mapambano ya silaha.
Ni wazi kwamba msimamo huo hauwezi kukidhi matakwa ya pande nne zinazoshiriki katika suala la Mashariki ya Kati, hali ambayo inalifanya kundi la Hamas lishindwe kutambuliwa wala kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa, na serikali itakayoongozwa na kundi hilo itakabiliwa na tatizo kubwa la fedha. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi. Condoleezza Rice katika mkutano wa London alisema, lazima serikali ijayo ya Palestina ishughulikie kuleta amani na Israel na Hamas inabidi kukubali haki ya kuwepo kwa Israel. La sivyo Marekani haitatoa misaada ya fedha kwa serikali itakayoongozwa na Hamas.
Serikali ya Israel imesimamisha kuikabidhi Palestina dola milioni 3.5 za kimarekani, kwa kisingizio kwamba pesa hizo huenda zitatumika kwa kuwasaidia magaidi katika mashambulizi dhidi ya raia wa Israel. Umoja wa Ulaya ambao ni mfadhili mkubwa kuliko wengine wa Palestina umesema kuwa, kuendelea kuipatia Palestina misaada ya fedha au la kunaambatana na vyama vipi vitashiriki kwenye serikali mpya ya Palestina na sera ya serikali hiyo.
Wachambuzi wanasema iwapo Marekani, Israel na Umoja wa Ulaya zitasimamisha misaada ya fedha, serikali ya Palestina haitaendelea kwa kuwa nusu ya matumizi yake inategemea misaada ya kimataifa. Katika hali hii, kundi la Hamas si kama tu halitatimiza ahadi za kuinua maisha ya watu na kufanya mageuzi, bali kitaweza kushindwa kuwalipa mishahara watumishi wa serikali.
Aidha Hamas imepata uongozi wa serikali ya Palestina kwa njia ya uchaguzi wa kidemokrasia, lakini bado inakabiliwa na tishio la mashambulizi ya kijeshi kutoka Israel. Waziri wa ulinzi wa Israel Bw. Shaul Mofaz tarehe 28 alisema, nchi yake haitaondoa mipango ya kuwaua viongozi wa Hamas bila kujali hadhi ya kundi hilo katika serikali ijayo ya Palestina.
Wakati huo huo, Hamas pia inakabiliwa na tatizo la kujenga serikali ya mseto itakayotambuliwa na jumuiya ya kimataifa haraka iwezekanavyo. Kutokana na kutokuwa na uzoefu wa kuongoza serikali na kuwekwa pembezoni na Marekani na nchi nyingine za magharibi, ni vigumu kwa kundi la Hamas kuunda serikali bila ushirikiano wa vyama vingine. Kwa hiyo, baada ya kupata ushindi kwenye uchaguzi, viongozi wake walikuwa wakieleza nia ya kuanzisha serikali ya mseto na kundi la Fatah, lakini pendekezo hilo halijakubaliwa na Fatah. Na wafuasi wa vyama hivyo viwili walikuwa wanapingana mara kwa mara.
Ndiyo maana kundi la Hamas linapaswa kurudi nyuma kwa kiasi fulani na kufanya chaguo lake kuhusu kuacha msimamo mkali na kutekeleza sera zenye unyumbufu kwa kufuata hali halisi .
|