Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-01 20:35:15    
Shule ya sekondari ya kimataifa ya Huiwen mjini Beijing

cri

katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na kuinuka kwa kiwango cha elimu ya juu ya China na athari ya kimataifa ya China, wageni wengi zaidi wanachagua kuendelea na masomo yao nchini China, wakiwemo wanafunzi wengi wa sekondari wa nchi za nje. Ili kurahisisha maisha na masomo ya wanafunzi hao na kuwawezesha wajiunge na vyuo vikuu vya China, idara ya elimu ya China imeanzisha shule za kimataifa kwenye miji mikubwa kadhaa.

Shule ya Huiwen iliyoko katikati ya Beijing ni shule moja maarufu ya kiserikali hapa Beijing. Shule hiyo imekuwa na historia ya miaka 130, na ilianzisha idara ya wanafunzi kutoka nje miaka 12 iliyopita.

Jengo jipya lenye rangi ya kijivu lililoko upande wa kaskazini wa shule hiyo ni jengo maalum la idara ya wanafunzi kutoka nje. Ndani ya jengo hilo, wanafunzi wa kidato cha pili cha sekondari ya juu walikuwa wako kwenye kipindi cha lugha ya Kichina.

"hamjambo, wanafunzi?"

"hatujambo."

"leo tunaanza kujifunza somo la 14."

Mwandishi wetu wa habari aliona kuwa, mbinu ya kufundisha ya shule hiyo inatofautiana na ya shule za kawaida za China. Darasani mwalimu hawafundishi wakati wote, bali wanafunzi wanajadiliana na kujifunza kwa vikundi. Wanafunzi wote 20 wa darasa hilo wanapangwa katika vikundi vya wanafunzi wanne au watano, wanaokaa pamoja kusoma na kujadiliana, au kusikiliza kwa makini maelezo ya mwalimu.

Kujifunza kwa vikundi ni mbinu ya kawaida ya kufundisha katika nchi za nje. Mwalimu wa lugha ya Kichina wa darasa hilo Bi. Zhang Shunzhi alieleza kuwa, kuingiza mbinu hiyo kwenye darasa letu ni moja ya hatua zilizochukuliwa na shule hiyo kwa kufuata tabia za kujifunza za wanafunzi wa nje.

"kipindi hiki cha leo kinawafahamisha wanafunzi kuhusu somo hilo, na kinalenga kuondoa matatizo ya kufahamu maneno kabla ya kuyatumia kufundishia. Kwa kutumia mbinu hii ya kujifunza kwa vikundi, wanafunzi wanasoma na kujifunza pamoja kwa ufanisi mkubwa zaidi."

Idara ya kimataifa ya shule ya Huiwen ya Beijing inalenga kutoa mazingira bora ya kujifunza na mbinu za kisasa za kufundishia kwa wanafunzi na kuwawezesha kuingia kwenye vyuo vikuu maarufu vya China. Mkurugenzi wa idara hiyo Bi. Jin Jie alieleza,

"mpango wetu wa masomo unawasaidia wanafunzi waingie kwenye vyuo vikuu maarufu vya China, na pia unawasaidia kupata ustadi kadhaa."

Nchini China, wanafunzi wa nchi za nje wakitaka kujiunga na vyuo vikuu, mbali na mahitaji ya shahada husika, pia wanapaswa kupita mtihani wa kuingia vyuo vikuu. Kwa kawaida mtihani huo unawekwa kutokana na mahitaji ya vyuo vikuu vyenyewe, ikiwemo mitihani ya masomo ya lugha ya Kichina, Hisabati, lugha ya Kiingereza na mtihani wa uwezo wa jumla wa sayansi ya jamii au Sayansi ya kimaumbile. Ili kuwawezesha wanafunzi wapate matokeo mazuri katika mitihani hiyo, mpango wa masomo ya idara hiyo unawekwa kutokana na mahitaji ya mitihani. Kwa mfano, wanafunzi wa nje wanaosoma katika shule hiyo wanapenda kujiunga na vyuo vikuu maarufu kabisa nchini China yaani chuo kikuu cha Beijing na chuo kikuu cha Qinghua, hivyo vitabu vya kiada vya shule hiyo pia vinatungwa na kurekebishwa mara kwa mara kutokana na mahitaji ya mtihani wa kuingia vyuo vikuu hivyo viwili. Aidha, shule hiyo pia inatilia maanani masomo ya lugha ya Kichina, lugha ya Kiingereza sayansi ya kompyuta, na kufanya shughuli mbalimbali kuwapa wanafunzi mazoezi ya mambo ya kijamii ikiwemo kuwashirikisha kwenye kazi za kujitolea na kutembelea sehemu mbalimbali.

Mtizamo huo wa elimu wa shule hiyo unawavutia wanafunzi wengi zaidi wa nje. Hivi sasa idara hiyo ina wanafunzi zaidi ya 200, wengi kati yao wanatoka nchi za Asia zikiwemo Korea ya Kusini, Vietnam na Malaysia. Wanafunzi hao waliondoka nyumbani na kuja nchini China wakiwa na umri wa miaka kati ya 12 na 18, kutokana na matumaini makubwa juu ya maendeleo ya China na kuona kuwa wakiweza kujifunza vizuri lugha ya Kichina, kusoma katika vyuo vikuu vya China, kuweza kujifunza utamaduni wa China, kuwa na marafiki wa China, itawasaidia kupata ajira nzuri.

Msichana Du Cuiheng mwenye umri wa miaka 17 anatoka kwenye ukoo wa madaktari wa vizazi vingi wa Vietnam. Mwaka mmoja uliopita, alikuja kusoma katika shule hiyo. Alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, kwa kuwa alipokuwa mtoto, watu wengi walisema anafanana na wachina kwa sura, hiyo alianza kuipenda nchi hiyo hata bila kujua iko wapi.

"Nilikuja nchini China miaka sita iliyopita, nikaona kuwa, China ni kubwa sana na inapendeza. Kwa hiyo, mama yangu aliniambia, 'unapenda udaktari na China, basi nenda China ukajifunze matibabu ya Kichina.' Kwa kuwa wanafunzi wanaosomea matibabu ya Kichina wanapaswa kuwa na msingi imara wa lugha ya Kichina, na katika sekondari ya Huiwen naweza kuboresha kiwango changu cha Kichina, hivyo napendelea kusoma katika sekondari hiyo. Nataka kujiandikisha katika Chuo Kikuu cha Matibabu na Mitishamba ya Kichina siku za baadaye."

Takwimu zilizotolewa na Wizara ya elimu ya China zinaonesha kuwa, katika miaka ya karibuni, idadi ya wanafunzi wa kigeni wanaosoma nchini China imekuwa inaongezeka mwaka hadi mwaka. Ni katika muda wa mwaka mmoja wa 2004 tu, idadi hiyo ilizidi laki moja na elfu 10, kiasi ambacho ni ongezeko la asilimia 42 zaidi kuliko mwaka uliotangulia. Aidha, idadi ya wanafunzi kutoka nje wanaosoma katika shule za sekondari nchini China inaongezeka kwa kiasi kikubwa. Hivi sasa, zipo sekondari zaidi ya kumi aina ya sekondari ya Huiwen ambazo hutoa elimu kwa wanafunzi wa kigeni hapa mjini Bejing. Tokea mwaka 1994, sekondari ya Huiwen imepokea wanafunzi elfu 3 kutoka nchi zaidi ya 30. Baada ya kuhitimu, wanafunzi hao wote walijiunga na vyuo vikuu vya China na asilimia 80 miongoni mwao walijiandikisha katika vyuo vikuu maarufu, vikiwemo Chuo Kikuu cha Beijing na Chuo Kikuu cha Qinghua.

Hata hivyo kuwaelimisha wanafunzi kutoka nje si jambo rahisi. Mkurugenzi wa sekondari ya Huiwen Bi. Jin Jie alisema, wanafunzi kutoka nje na wa Kichina wako sawa katika sekondari hiyo, tofauti ni kwamba, kuwatolea elimu wanafunzi kutoka nje kunahitaji uvumilivu na upendo mwingi zaidi. Kwa kuwa watoto hao wanaishi nchini China kwa wao wenyewe, wanakabiliwa na matatizo ya lugha, na tofauti za kiutamaduni na kimila, wanahitaji misaada mingi kutoka kwa walimu wao.

"Kwa upande wa maisha, tunajitahidi kuwatunza tukijifanya kama wazazi wao. Tunakusudia kuwaelimisha ili wawe na desturi nzuri, tabia nzuri na kuwa na uhusiano mzuri na wenzao."

Mwanafunzi kutoka Korea ya kusini Bibi Seo Ji Young ana umri wa miaka 18 sasa, amesoma katika sekondari ya Huiwen kwa karibu miaka mitatu. Kutokana na misaada kutoka kwa walimu, amezoea kabisa maisha ya shule hiyo ya sekondari.

"Ninapokabiliwa na matatizo, walimu wananisaidia. Mwanzoni nilipokuja, nilikuwa napiga simu nyumbani kila siku. Lakini hivi sasa, wazazi wangu wametulia na mimi siwakumbuki mara kwa mara. Walimu wanasimamia maisha yetu kwa makini sana."

Wanafunzi wenzake wa Bi Seo Ji Young walieleza kuwa, hoteli ya sekondari hiyo ilijengwa miaka mitatu iliyopita, ambapo wanafunzi wawili wanakaa kwenye chumba kimoja chenye televisheni na huduma ya mtandao wa internet. Kutokana na kuwepo kwa wanafunzi wengi kutoka Korea, chakula cha Kikorea kinapatikana katika kantini ya sekondari ambacho kinawavutia sana. Bi Seo Ji Young alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, atashiriki kwenye mtihani wa kujiunga na Chuo Kikuu cha Beijing mwezi Aprili mwaka huu. Anatumai kuwa ataweza kupata mafanikio ambayo yatawafurahisha sana wazazi wake.