Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-02 20:43:54    
Wakazi wa Beijing wapenda kuteleza kwenye theluji katika majira ya baridi

cri

Kituo cha kuteleza kwenye theluji cha Longfengshan cha wilaya ya Mentougou kilichoko kwenye sehemu ya magharibi ya Beijing kina kilomita 30 hivi kutoka sehemu ya mjini. Mwandishi wetu wa habari alipokwenda kwenye kituo hicho siku ya wikiendi, aliwakuta watu wengi wanaoteleza kwenye theluji. Bi. Gao Qing alisema:

"Kila ifikapo majira ya baridi mimi na wenzangu huja hapa kuteleza kwenye theluji. Najisikia vizuri sana ninapoteleza kwenye theluji kama nikiruka angani."

Kituo cha kuteleza kwenye theluji cha Longfengshan chenye eneo la mita za mraba laki tano, kinawavutia watelezaji wengi kutokana na kuwa na njia bora ya utelezaji kwa watu wanaoanza kujifunza kuteleza kwenye theluji. Kituo cha Longfengshan ni kituo cha wastani cha mchezo wa kuteleza kwenye theluji hapa Beijing, na mji wa Beijing una vituo zaidi ya 10 vikubwa zaidi kuliko hicho cha Longfengshan. Kila kituo kina vigari vya kamba vinavyovutwa kwa waya, na njia ya tramu inayowavuta watelezaji hadi mlimani, na ubao wa kutelezea kwenye theluji, na mavazi husika. Kila kituo pia kina idara za kutoa huduma, kama vile duka la kuuzia vifaa vya kutelezea, mkahawa, ukumbi wa mapumziko, na shule ya kufundisha mchezo wa kuteleza kwenye theluji. Vituo hivyo licha ya kutoa huduma kwa watalii, pia vimeanzisha michezo mingine ya kuteleza kwenye theluji, kama vile kupanda pikipiki kwenye theluji, na sehemu kwa ajili ya watoto kucheza.

Meneja mkuu wa kituo cha kuteleza kwenye theluji cha Longfengshan Bw. Zhang Lixin alikuwa hodari kuteleza kwenye theluji na anafahamu vizuri maendeleo ya soko la mchezo wa kuteleza kwenye theluji hapa Beijing. Akisema

"Kituo cha kwanza cha mchezo wa kuteleza kwenye theluji cha Beijing kilifunguliwa mwaka 2000, ilipofika mwaka 2005, mjini Beijing kumekuwa na vituo vikubwa zaidi ya 10 vya mchezo wa kuteleza kwenye theluji, idadi ya wachezaji wa mchezo huo imeongezeka na kufikia milioni moja ya hivi sasa kutoka ile ya elfu kadhaa ya mwaka 2000. Soko la mchezo wa kuteleza kwenye theluji mjini Beijing linastawi mwaka hadi mwaka."

Mjini Beijing hakuna theluji nyingi, kila ifikapo mwishoni mwa mwezi Novemba, vituo vyote vya mchezo wa kuteleza kwenye theluji hutengeneza theluji kwa mitambo maalum.

Lakini kwa nini watu wengi wa Beijing wanapenda kuteleza kwenye theluji? Mtaalamu wa elimu ya jamii wa China alisema, kutokana na kuinuka kwa kiwango cha maisha cha watu wa China, wakazi wa Beijing wanafuatilia zaidi maisha ya kisasa na ya kujenga afya. Zamani katika majira ya baridi, watu wengi walikuwa wanakaa nyumbani tu wakicheza karata, kunywa pombe au kuimba nyimbo. Kuteleza kwenye theluji ni burudani tofauti, vituo vyote vya mchezo wa kuteleza kwenye theluji viko katika sehemu ya milimani, mazingira na hewa ni mazuri sana. Kufanya mazoezi katika mazingira yenye hewa nzuri kunasaidia afya, hivyo watu wengi wanapenda kwenda milimani kujiburudisha katika kuteleza kwenye theluji.

Bw. Zhou Qiang anayefanya kazi katika kampuni moja ya software ya Beijing anacheza mchezo wa kuteleza kwenye theluji mara kwa mara, anaupenda sana mchezo huo, Alisema:

"Mwanzoni nilidhani kuteleza kwenye theluji ni mchezo wa kujiburudisha tu, lakini baada ya kufahamu namna ya kuteleza kwenye theluji nimeanza kuupenda zaidi mchezo huo. Naona kuteleza kwenye theluji ni mchezo mzuri zaidi kuliko michezo mingine."

Ili kuwawezesha wakazi wa Beijing wasiokuwa na magari kuweza kucheza mchezo wa kuteleza kwenye theluji kwa urahisi, hivi sasa vituo vidogo vya kuteleza kwenye theluji vimeanzishwa mjini Beijing. Kituo cha kuteleza kwenye theluji cha Yabuluoni cha bustani ya Chaoyang cha Beijing kinatoa huduma usiku na mchana. Licha ya kuteleza kwenye theluji, kituo hicho pia kimeanzisha michezo mingine ya kujiburudisha kama vile kuendesha pikipiki kwenye theluji, kuteleza kwa gurudumu, na kucheza mpira wa miguu kwenye theluji. Pia kimeweka sehemu kwa ajili ya watoto kucheza kwenye theluji. Kutokana na kuwa na michezo mingi, ingawa kituo hicho kina eneo dogo, lakini kinawavutia watu wengi wanaojifunza kuteleza kwenye theluji.

Kwenye kituo cha mchezo wa kuteleza kwenye theluji cha Yabuluoni, mwandishi wetu wa habari alimkuta Bi. Li Tao aliyekwenda na marafiki zake. Alisema:

"Hii ni mara yangu ya kwanza kuteleza kwenye theluji, mwanzoni sikuweza kujizuia kuanguka, lakini sasa nimeanza kufahamu jinsi ya kuteleza kwenye theluji na kuweza kusikia hali ya urukaji angani. Kweli huo ni mchezo mzuri."

Kwa sababu kuteleza kwenye theluji bado ni mchezo mpya kwa wakazi wengi wa hapa Beijing, hivyo kila kituo kina walimu kadha wa kadha wanaowafundisha watelezaji wapya ustadi wa utelezaji kwenye theluji. Bwana Jiang Dongen ni mmoja wa walimu hao, alisema kuteleza kwenye theluji kunahitaji kasi, hivyo baadhi ya watelezaji walipoanza kujifunza huanguka mara kwa mara hata kupata majeraha madogo. Akisema:

"Watu wengi ni walioanza kujifunza kuteleza kwenye theluji, viatu vya kutelezea kwenye theluji huwa ni vigumu, na havifai miguu yao kama viatu vya kawaida, hivyo ni rahisi kwao kuanguka au kuumia."

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya watu wanadhani kuwa, kuteleza kwenye theluji ni mchezo wenye hatari, hivyo vijana ni wengi zaidi kati ya mashabiki wa mchezo huo. Bw. Jiang alisema kuteleza kwenye theluji hakuna hatari, watelezaji wapya wakifahamu namna ya kuchukua tahadhari, au wasiwe na haraka wakati wa kujifunza ustadi wa kuteleza, si rahisi kuumia. Kama ajuavyo watelezaji wengi waliowahi kupata majeraha madogo hawapunguzi hamu ya kupenda mchezo wa kuteleza kwenye theluji, wengi wao wamekuwa hodari wa kuteleza kwenye theluji.

Bw. Jiang aliongeza kuwa kutokana na mwelekeo wa hivi sasa wa maendeleo ya mchezo wa kuteleza kwenye theluji, wakazi wa Beijing watakaopenda mchezo wa kuteleza kwenye theluji wataongezeka mwaka hadi mwaka, na inakadiriwa kuwa, mwaka kesho watu wengi zaidi watashiriki mchezo huo wa kuteleza kwenye theluji.