Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-02 20:59:10    
Mradi wa "kutoa ujoto" wa China

cri

Wakati mwaka mpya wa Kichina ulipokaribia, harakati iitwayo "kutoa ujoto" iliyokuwa imefanyika kwa zaidi ya mwezi mmoja na kuwanufaisha makumi na maelfu ya Wachina wenye matatizo ya kiuchumi ilikuwa imekamilishwa. Harakati hizo zinafanyika kila mwaka chini ya uongozi wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi la China. Tokea ilipoanzishwa miaka kumi iliyopita, harakati hiyo ya serikali inayolenga kuwasaidia wananchi maskini ni harakati kubwa inayowanufaisha watu wengi kabisa nchini China.

"kutoa ujoto" ni harakati ya kuwashirikisha Wachina wasaidiane, ambapo kusaidiana ndio utamaduni wa Kichina. Sikukuu ya Spring ni mwaka mpya kwa kalenda ya Kichina, na pia ni sikukuu muhimu kuliko nyingine katika jamii ya Wachina. Ili wafanyakazi wenye matatizo ya kiuchumi waweze kusherehekea sikukuu hiyo kwa furaha, Shirikisho la vyama vya wafanyakazi la China tokea miaka ya 90 ya karne iliyopita, lilianzisha harakati iitwayo "kutoa ujoto", ambapo kila inapokaribia Sikukuu ya Spring, wananchi wenye matatizo ya kiuchumi wanapewa pesa na vitu. Na hatua kwa hatua serikali katika ngazi mbalimbali za China zimekuwa zinashiriki katika harakati hiyo.

ikilinganishwa na miaka iliyopita, harakati ya mwaka huu ilipata mafanikio zaidi kutokana na uungaji mkono mkubwa wa serikali kuu. Mwishoni mwa mwaka 2005, Rais Hu Jintao wa China alitoa mfano kwa kushiriki kwenye harakati hiyo kwa mtu binafsi, ambapo alitoa pendekezo la kuwapatia furaha na upendo wananchi wenye matatizo ya kiuchumi, hususan waliokumbwa na maafa ya kimaumbile. Hapo baadaye, viongozi wengine wakafuatia kutekeleza pendekezo hilo kwa kutoa michango ya fedha na vitu. Kwa mujibu wa takwimu, katika muda wa mwezi mmoja tangu harakati hiyo ianzishwe, ilipokea jumla ya Renminbi Yuan milioni 240, sawa na dola za kimarekani milioni 30, pamoja na nguo na matandiko milioni 23 laki 5 na elfu 20. Wananchi zaidi ya milioni 20 walinufaika na michango hiyo.

Msomi kutoka Taasisi ya sayansi ya jamii ya Shanghai Bw. Lu Xiaowen alisema, "Kuwasaidia watu maskini na wenye matatizo ni utamaduni mzuri wa jadi wa Kichina. Baada ya kuwepo kwa miaka 10, harakati ya 'utoaji ujoto' kwa mara nyingine tena ilitiliwa maanani na kuwashirikisha wananchi wengi watoe michango, ni kutokana na kwamba, inaambatanisha utamaduni wa Kichina na moyo wa kuwahudumia wananchi unaofuatiliwa na Chama tawala cha Kikomunisti, inaonesha mawazo mapya ya chama hicho katika kuitawala China, nayo ni kwamba lengo la maendeleo ni kwa ajili ya wananchi, wananchi huleta maendeleo na matunda ya maendeleo yanawanufaisha wananchi. "

China imekuwa na maendeleo ya kasi kwa miaka mingi mfululizo, lakini kutokana na idadi kubwa ya watu na maafa ya kimaumbile yanayoikumba mara kwa mara, China bado ina watu wengi wenye shida ya kiuchumi. Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya mambo ya kiraia, hivi sasa kuna wananchi wasiopungua milioni 60 wanaoathiriwa na maafa ya kimaumbile kila mwaka, aidha wakazi wa mijini wapatao milioni 20 wanaishi chini ya kiwango cha mapato duni, pia kuna wanavijiji maskini milioni 75, na wananchi hao wanahitaji misaada.

Bw. Huang Zhenhua ni mkazi wa Shanghai ambaye hana ajira. Alisema alikuwa anaogopa Sikukuu ya Spring, kwa sababu jamaa walipomtembelea nyumbani kwake, alikuwa hana uwezo wa kuwaalika chakula kizuri kutokana na umaskini. Alisema alikuwa anajiona kuwa ni miongoni mwa watu wanaoishi maisha ya kiwango cha chini kabisa katika jamii.

Mke wa Bw. Huang alifariki dunia miaka mingi iliyopita. Sasa Bw. Huang, mama yake mwenye umri wa miaka 80 na binti yake anayesoma sekondari wanategemea pato lisilozidi Renminbi Yuan elfu 1 kwa mwezi, ambalo ni sawa na dola za kimarekani 120 hivi. Mwak huu harakati ya "kutoa ujoto" iliwapa matandiko mawili, nguo zaidi ya 10 pamoja na vyakula mbalimbali pamoja na wali, nyama na mayai. Bw. Huang alieleza kuwa, "Kumbe nimeelewa maana ya methali isemayo 'Wape watu makaa theluji inapoanguka'."

Katika miaka ya hivi karibuni, harakati hiyo imepata maendeleo. Mbali na kutoa chakula na pesa wakati wa mwaka mpya wa Kichina, imeongezwa hatua nyingine ya kutoa misaada katika siku za kawaida za mwaka mzima. Mkoa wa Guizhou ambao ni miongoni mwa mikoa maskini ya China ni mfano mzuri, ambapo zawadi zilizotolewa na serikali ya mkoa huo mwaka huu zilikuwa pamoja na nafasi za ajira zipatazo elfu moja.

Katika miaka ya hivi karibuni, idadi ya wananchi walionufaika na harakati ya "kutoa ujoto" pia iliongezeka. Katika mji wa Shanghai serikali imefuata sera mpya kwamba, familia inayoishi chini ya mara 1.5 ya pato duni lililotangazwa na serikali ni familia maskini, na watu wenye matatizo mbalimbali katika maisha ya kawaida pia wanapewa misaada.

Hapo mwanzoni ilikuwa ni wakazi wa miji tu waliopewa misaada. Lakini sasa imebadilika ambapo Shirikisho la vyama vya wafanyakazi la China limetangaza kuwa, litaongeza Renminbi Yuan milioni 5, sawa na dola za kimarekani laki 6 kwa ajili ya kuwasaidia wakulima.

Wananchi waliopewa misaada si watu pekee walionufaika na harakati hiyo ambayo imedumu kwa miaka zaidi ya 10, bali pia wananchi waliotoa michango. Bw. Lin Yu wa mji wa Shanghai alichangia nguo 7 mwishoni mwa mwaka 2005, alisema "Kwa kushiriki katika harakati ya namna hii, najiona kuwa naweza kutoa mchango kwa jamii."

Bw. Xia Xiaowen ni ofisa wa serikali mjini Chongqing, ametoa michango kwa miaka mingi. Alieleza kuwa, "Harakati hiyo ni nafasi nzuri ya kuwaelimisha watumishi na maofisa wa serikali. Sasa imeshapita miaka zaidi ya 20 tangu China ianze kufuata sera ya mageuzi na kufungua mlango, lakini bado kuna wananchi wengi wanaoishi maisha magumu, kwa hiyo hatuna kisingizio chochote cha kujiona wakubwa amakulegalega kazini."