Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-06 15:09:20    
Magulio katika Sikukuu ya Spring

cri

Tarehe 29 Januari ni sikukuu ya Spring, yaani mwaka mpya kwa kalenda ya Kichina. Sikukuu ya Spring ni sikukuu kubwa ya jadi nchini China, na shamrashamra za kutembelea magulio ni desturi ya Wachina katika sikukuu hiyo.

Katika kila mwaka mpya wa Kichina kutembelea magulio ni aina moja ya utamaduni wa China, magulio hufanyika kwenye mahekalu na bustani, ni mkusanyiko wa shamrashamra za michezo, utalii na ununuzi ya vitu, kwa hiyo pia ni maonesho ya utamaduni wenye historia ndefu wa Kichina. Beijing, ukiwa mji mkuu wa miaka mingi una magulio maarufu zaidi, kila mwaka magulio huvutia watu wengi wa nchini na nchi za nje. Wakati wa sikukuu ya Spring imekaribia, matayaarisho ya magulio ya aina mbalimbali yamepamba moto ili kuwavutia watu wengi zaidi kwenda magulioni kuburudika.

Mjini Beijing kuna sehemu nyingi za magulio, kwa mfano Di Tan, mahali penye madhabahu ya wafalme kutambikia mungu wa ardhi, ni mahali maarufu kwa gulio la sikukuu ya Spring. Di Tan ilijengwa mwaka 1530, gulio la sikukuu ya Spring hufanyika huko kila mwaka kuanzia mwaka 1985. Ofisa wa idara ya bustani Bw. Wang Zhonghua alisema, "Tayari tumepamba mazingira, mbele ya mlango tumetundika taa kubwa za kasri zenye picha za wanyama wanaowakilisha miaka 12. na mlango umepambwa kwa maua na vitambaa vingi virefu vyenye maneno ya kuifurahia sikukuu ya mwaka mpya."

Gulio la Di Tan linafunguliwa tarehe 28 Januari hadi tarehe 4 Februali yaani tarehe 29 Desemba hadi tarehe 7 Januari kwa kalenda ya Kichina. Mwaka huu ni mwaka wa mbwa, kwa hiyo kuna sanamu tano za mbwa kwenye kiwanja mbele ya mlango.

Inasemekana kwamba mwaka huu gulio linalofanyika katika Di Tan limepanga shughuli za "ibada ya kuomba baraka na amani" kama ilivyofanywa na wafalme wa zamani, na watalii wa nchini na nchi za nje watajionea na kuhisi utamaduni mkubwa wa China kwa kuona shughuli hizo na vitu vya sanaa za aina mbalimbali na picha za mwaka mpya za Kichina na vyakula vya kisehemu na udohoudoho.

Ofisa wa Kamati ya Maandalizi ya Shughuli za Gulio la Di Tan Bw. Yang Xiaodong alisema, "Licha ya kuendelea na michezo na shughuli za zamani, mwaka huu tumeongeza mawasiliano ya uso kwa uso kati ya watalii na wasanii wa sanaa za mikono, na watalii wataweza kucheza michezo jukwaani pamoja na wachezaji wa michezo ya sanaa."

Katika bustani ya Long Tan Hu iliyoko katika mtaa wa kusini ya mashariki ya Beijing, shamrashamra muhimu ni maonesho na michezo ya mashindano, kama ya ndondi, mieleka, judo na mashindano mengine.

Gulio litakalofanyika katika Hekalu la Bai Yun Guan litakuwa na michezo ya ngoma ya simba na mironjo, na waumini wa dini ya Dao watafanya ibada ya kuomba amani ya dunia kwenye sehemu maalumu iliyotengwa gulioni.

Kuhusu gulio linalofanyika katika bustani ya Chaoyang ofisa wa kamati ya maandalizi ya sherehe Bw. Jin Rishun alisema, "Mwaka huu kutakuwa na michezo ya mironjo ya wanawake, maonesho ya Bendi Wildcat ya Uingereza na maonesho ya dansi na nyimbo za Russia." Magulio yanajaa utamaduni mkubwa wa jadi wa China, yanaonesha matumaini ya Wachina kuhusu maisha bora kutoka pande mbalimbali. Kwa hiyo Wachina wanapokuwa katika likizo ya sikukuu ya mwaka mpya huwa hawakosi kushiriki kwenye magulio hayo.

Idhaa ya kiswahili 2006-02-06