Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-06 20:36:55    
Palestina yashughulikia uundaji wa serikali mpya

cri

Mwenyekiti wa mamlaka ya Palestina Bw. Mahmood Abbas tarehe 4 huko Gaza alikuwa na mazungumzo ya kwanza pamoja na viongozi wa kundi la Hamas baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa kamati ya utungaji sheria ya Palestina, na kuwa na majadiliano kuhusu uanzishaji wa serikali mpya ya nchi hiyo. Wachambuzi wamesema, mazungumzo hayo yanaonesha uwezekano wa Hamas kuchukua nafasi muhimu katika serikali mpya ya Palestina.

Kwanza inaonekana katika uundaji wa serikali mpya itakayoundwa, kuwa kundi la Hamas ambalo lilipata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa kamati ya utungaji sheria, halitaki kuchukua nafasi muhimu peke yake katika serikali mpya, na limeliomba kundi la Fatah lishirikiane na kundi hilo katika uundaji wa serikali mpya, lakini kundi la Fatah lilikubali kwa shingo upande, hali ambayo inalifanya kundi la Hamas kuona kama ni fedheha. Lakini wachambuzi wa Palestina wanaona kuwa, ingawa kuna tofauti kubwa kati ya Hamas na Fatah, lakini "ushirikiano" wa pande hizo mbili utakuwa unaendana na maslahi ya taifa zima la Palestina na kuchangia kuitoa Palestina katika hali ya shida ya kisiasa ya hivi sasa. Hamas inaweza kuitumia Fatah kuziba pengo lake la upungufu wa uzoefu wa utawala, kuwajibika kisiasa kwa pamoja, wakati Fatah itaweza kupunguza shinikizo za nchi za nje dhidi ya Palestina kutokana na Hamas kuchukua nafasi muhimu katika serikali ya nchi hiyo, ili kujiimarisha na kunyanyuka upya. Ushirikiano wa vyama hivyo viwili utahimiza mageuzi ya ndani ya Palestina, kuanzisha serikali adilifu na ya uwazi. Mmoja wa viongozi wa Hamas Bw. Ismail Haniyeh hivi karibuni alidokeza kuwa katika siku mbili zilizopita, viongozi wa Hamas na Fatah walikuwa na mikutano mingi ya faragha wakibadilishana maoni kuhusu kuanzishwa kwa uhusiano wa wenzi wa kisiasa na serikali mpya.

Pili, ni kuhusu kazi itakayofanywa kundi la Hamas katika uamuzi wa sera za ndani na nje za serikali ya Palestina. Sababu muhimu ya kushinda katika uchaguzi wa kamati ya utungaji sheria kwa Hamas ni kuhusu mambo ya ndani, ambayo iliahidi kufanya mageuzi ya jamii na siasa, kuboresha maisha ya watu wa nchi hiyo pamoja na mambo mengine yanayofuatiliwa na wapiga kura wa nchi hiyo. Kutokana na kuwa kundi la Hamas linafuata sera ya upinzani dhidi ya Israeli, hivyo halina haraka ya kutwaa madaraka kuhusu mambo ya kidiplomasia. Wachambuzi wamesema katika serikali mpya ya Palestina, huenda Bw Abbas na wanachama wa kundi la Fatah walioko katika serikali watashughulikia mambo ya kidiplomasia na Israel pamoja na nchi za magharibi, wakati maofisa waliotoka Hamas watashughulikia zaidi mambo ya ndani ya nchi hiyo.

Tatu, madaraka ya udhibiti wa jeshi la usalama la Palestina yataathiri sana utulivu wa nchi ya Palestina. Jeshi la usalama la Palestina hudhibitiwa na wizara ya mambo ya ndani ya serikali, hivi sasa wanajeshi wa usalama zaidi ya elfu 60 wote wanatoka kundi la Fatah, baada ya Hamas kushinda katika uchaguzi wa kamati ya utungaji sheria, baadhi ya maofisa wa Fatah walisema hawatatii amri za Hamas. Hivi karibu kuna habari zilizosema kuwa Bw Abbas anajaribu kutoa wizara ya usalama kutoka katika serikali na kuiweka chini ya uongozi wa Ikulu. Lakini mmoja wa viongozi wa kundi la Hamas Bw. Ismail Haniyeh tarehe 4 baada ya kuwa na mazungumzo na Bw Abbas alisema, Bw Abbas amekubali kundi la Hamas lidhibiti baadhi ya vikosi vya usalama.

Nne, ni kama serikali mpya ya Palestina itatambuliwa na jumuiya ya kimataifa au la. Baada ya kundi la Hamas kushinda katika uchaguzi wa kamati ya utungaji sheria, jumuiya ya kimataifa inataka kundi la Hamas liitambue Israel, kuvunja jeshi, kucha matumizi ya nguvu ya kimabavu na kukubali mpango wa ramani ya amani ya mashariki ya kati. Kuhusu madai ya jumuiya ya kimataifa, msimamo wa mwisho wa kundi la Hamas uko wapi? Wachambuzi wa siasa wa Palestina wanasema, Hamas haiwezi kuwa na mabadiliko ya kugeuka nyuma kabisa katika "usiku mmoja". Watu wanatarajia makundi mbalimbali ya kisiasa ya Palestina yatazingatia maslahi ya taifa ili kuanzisha kipindi kipya ya siasa ya Palestina.

Idhaa ya Kiswahili 2006-02-06