Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-07 16:10:19    
Hali ya ununuzi wa vitu katika sikukuu ya Spring

cri

"Kujinyima kwa matumizi" ni mazoea mema yaliyoendelea kwa miaka maelfu kadhaa ya watu wa China, hata katika jamii ya hivi sasa yenye vishawishi vingi, na "kuweka akiba nyingi ya fedha benki" pia ni imani ya wachina wengi. Lakini kila kitu kinaweza kuwa na tofauti na hali yake ya kawaida, kila mwaka kuna kipindi fulani ambapo wachina wanaweza kusahau kwa muda mazoea yao na kununua sana vitu wanavyovitaka. Kipindi hicho ndicho kinachofanya watu waridhike sana yaani sikukuu ya Spring, ambayo ni siku kuu kubwa kabisa kwa wachina.

Kula chakula cha jioni pamoja na watu wote wa familia katika mkesha wa sikukuu ya Spring, ni jadi ya wachina katika kipindi cha sikukuu ya Spring. Hapo nyuma wachina wengi walikuwa wanakula mlo huo muhimu majumbani mwao, lakini hivi sasa pamoja na kuongezeka kwa pato na mahitaji yao, wachina wengi wanakula mlo huo muhimu katika mahoteli na migahawa. Mahoteli na migahawa ambayo hapo zamani ilifunga milango yao katika kipindi cha sikukuu ya Spring, hivi sasa biashara yao ni motomoto mwaka hadi mwaka katika kipindi cha sikukuu ya spring. Viti vya mahoteli na migahawa maarufu katika miji mikubwa ya Beijing, Shanghai, Chongqing na Guangzhou vyote viliagizwa hata miezi zaidi ya miwili kabla ya sikukuu ya Spring. Migahawa ya nyama ya bata ya kuokwa ya Quanjude, ambayo ni maarufu inayojulikana nchini na nchi za nje, ni vivyo hivyo. Kiongozi husika wa kampuni ya Quanjude bibi Liu Guifang alisema,

"Viti vingi vya migahawa yetu viliagizwa na watu, katika mkesha wa sikukuu ya Spring, viti vyote vilijaa. Pato letu katika kipindi cha sikukuu ya Spring mwaka uliopita lilikuwa Yuan milioni 10, tunatarajia pato letu la mwaka huu litakuwa kubwa zaidi kuliko lile la mwaka uliopita."

Aidha, maduka ya chakula cha haraka yanayoendeshwa na wafanyabiashara wa kigeni pia yalibuni mbinu ya kuchukua nafasi ya chakula katika kipindi cha sikukuu ya Spring, migahawa ya McDonalds ilitoa vyeti vya zawadi ili kuvutia wateja, wakati migahawa ya KFC ilitundika mapambo ya jadi ya kichina. Inakadiriwa kuwa pato la sekta ya chakula nchini China katika kipindi cha sikukuu ya Spring linaweza kuzidi Yuan milioni 200.

Mbali na hayo, maduka ya biashara ya rejereja ya wafanya biashara wa kigeni pia yalitumia mbinu zenye umaalum wa kichina ili kuvutia wateja. Supamaketi za Wal-Mart na Carrefour zilifuata jadi za kichina, zikapamba maduka yao kwa kutundika taa kubwa nyekundu za kichina au kubandika mapicha ya sikukuu ya Spring, licha ya hayo zimeweka kaunta maalumu za kuuza peremende, sigara na nyama ya kubanikwa ili kuvutia wateja.

Mapumziko ya siku 7 katika kipindi cha siku kuu ya Spring, yametoa nafasi nzuri kwa wachina kutembelea sehemu ya nje. Kutembelea nchi za nje ni shughuli zinazopendwa na watu wengi katika kipindi cha sikukuu. Bibi Chi Rui anayeishi katika mji wa Shenyang, sehemu ya kaskazini mashariki ya China, na alifunga ndoa siku chache zilizopita, alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa katika kipindi cha sikukuu ya Spring, yeye na mume wake hawataki kushinda nyumbani, bali wanataka kutembelea Hong Kong.

"Tunataka kufahamu mazoea ya mazingira ya maisha ya wakazi wa Hong Kong, hasa tunataka kununua vitu, Hong Kong ina bidhaa nyingi maarufu, tena zinauzwa kwa bei nafuu katika kipindi cha sikukuu. Zaidi ya hayo Disneyland imejengwa huko Hong Kong, tunataka kuitembelea pia. Tunafikiria kutumia Yuan elfu 30 hadi 40 kama vile tunajifurahisha katika kipindi cha fungate."

Wachina wengi wana wazo kama la bibi Chi Rui na mumewe, katika kipindi cha siku kuu ya Spring wanataka kutembelea Hong Kong, Macao na nchi za Asia ya kusini mashariki, ambazo siyo mbali sana na China. Meneja wa soko la utalii wa Shirika la Utalii wa Kimataifa la China Bw. Zhang Shuo ana imani kubwa na shughuli za utalii katika nchi za nje katika kipindi cha sikukuu ya Spring alisema,

"Hapo zamani, wachina walipenda kushinda nyumbani pamoja na watu wa familia zao katika mkesha wa sikukuu ya Spring, lakini mazoea hayo yamebadilika. Watu wengi wanachagua kutembelea nchi za Asia ya kusini mashariki kama Phuket na kisiwa cha Bali, hivi sasa mashirika yote ya utalii yamesimamisha uandikishaji wa watalii kutokana na wingi wa watu wanaotaka kuzitembelea nchi hizo. Kipindi cha siku kuu ya Spring kimekuwa nafasi nzuri kwa sekta ya utalii, ambayo inapata ufanisi na faida kubwa."

Takwimu zinaonesha kuwa watalii waliotembelea nchi za nje hususan walitoka miji miwili mikubwa ya China ya Beijing na Shanghai, na idadi ya watalii wa miji hiyo miwili zilifikia elfu 32 na elfu 28. Watu wa sekta ya utalii wamekisia kuwa idadi ya wachina wanaotembelea nchi za nje katika kipindi cha siku kuu ya Spring mwaka huu itavunja rekodi.

Sikukuu ya Spring inachukuliwa kuwa ni jadi ya kiutamaduni, lakini hivi sasa kitu kinachofuatiliwa zaidi na watu ni thamani ya kiuchumi inayotokana na sikukuu hiyo. Bw. Gao Debu ni profesa wa kitivo cha uchumi cha Chuo Kikuu cha Wananchi cha China, alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa hali ya ununuzi wa vitu katika kipindi cha sikukuu ya Spring kwa kiwango fulani inazidisha ongezeko la uchumi. Alisema, "ununuzi wa bidhaa" na matumizi ya huduma vinaongezeka kwa kiwango kikubwa katika kipindi cha sikukuu ya Spring, hali ambayo inachangamsha masoko yote ya China. Ununuzi wa bidhaa umebadilika kuwa matumizi ya huduma, hii ni mabadiliko makubwa yaliyotokea katika kipindi cha sikukuu ya Spring cha mwaka huu. Mabadiliko hayo yanaonesha kuinuka kwa kiwango cha maisha ya watu. Wafanyabiashara wanapaswa kuendeleza soko la kipindi cha siku kuu ya Spring kwa kutumia mabadiliko hayo."

Bw. Gao Debu alisema, kuongezeka kwa mfululizo kwa ununuzi katika kipindi cha sikukuu ya Spring kunatokana na ongezeko la kasi la uchumi wa China. Katika miaka ya karibuni, ongezeko la uchumi wa China lilikuwa linadumishwa katika zaidi ya 9%, pato la wakazi wa mijini na vijijini liliongezeka kwa kiasi kikubwa, na fedha za akiba walizoweka benki zinaongezeka kwa mfululizo. Habari zinasema hata katika sehemu za vijiji, ambazo ziko nyuma kiuchumi ikilinganishwa na sehemu za mijini, ununuzi wa vitu wa wakulima pia uliongezeka kwa kiasi kikubwa, wakulima wanapenda kununua vitu pamoja na chakula kinachotumika katika kipindi cha sikukuu ya Spring.

Mtaalamu wa uchumi ambaye ni profesa wa kitivo cha uchumi cha Chuo Kikuu cha Wananchi Bw. Gao Debu alisema, kuna tofauti kubwa katika matumizi ya fedha kati ya sehemu za mijini na sehemu za vijiji kutokana na tofauti ya mapato, hivi sasa wakazi wa mijini wanafikiria kutalii sehemu ya nje, wakati wakazi wa vijijini wananunua vitu na chakula. China ina idadi ya wakulima karibu milioni 900, hivyo soko la biashara nchini china bado lina nafasi kubwa ya kuendelea.

Idhaa ya kiswahili 2006-02-07