Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-08 20:43:09    
China kuanzisha mfumo kamili wa huduma za afya vijijini

cri

Watu zaidi ya milioni 750 wanaishi kwenye sehemu za vijijini nchini China, idadi hiyo inachukua asilimia 60 ya watu wote nchini China. Kutokana na sababu mbalimbali, hali ya huduma za afya vijijini bado iko nyuma sana ikilinganishwa na mijini. Nanma ya kuwasaidia wakulima kulinda afya zao na kutoa huduma za matibabu vijijini ni suala linalozingatiwa sana na serikali ya China. Hivi karibuni, serikali ya China imeweka mpango kuwa, katika miaka mitano ijayo China itajenga mfumo kamili wa huduma za matibabu kwenye sehemu za vijijini.

Takwimu husika zinaonesha kuwa, asilimia 80 ya raslimali za matibabu zimekusanyika mijini hasa kwenye hospitali kubwa. mfumo usiokamilika wa huduma za afya vijijini, vifaa vya matibabu vilivyopitwa na wakati na upungufu wa wataalamu wa utoaji wa matibabu kwenye sehemu za vijijini haviwezi kukidhi mahitaji ya huduma za afya vijijini. Aidha, wakulima wa China wanakosa uhakikisho wa kimsingi wa matibabu na kujilipia gharama za matibabu. Lakini kutokana na wakulima wengi wa China kuwa na mapato kidogo, ni sehemu ndogo tu ya mapato yao inaweza kutumika kwa ajili ya kugharamia matibabu. Hivyo kama wakulima wakipata magonjwa makubwa, watashindwa kumudu gharama kubwa za matibabu. Mwanakijiji mzee Zhang na familia yake wa wilaya ya Jianli mkoani Hubei alisema:

"hata yuan mia moja au mbili ni gharama kubwa kwa familia za sisi wakulima. Hivyo kama tukipatwa na magonjwa, lakini bado tunaweza kufanya kazi na kula chakula, hatutakwenda hospitali."

Ili kutatua suala hilo, kuanzia mwaka 2003 serikali ya China ilianza kujenga mfumo mpya wa ushirikiano wa matibabu vijijini, yaani serikali kuu, serikali za mitaa na wakulima wanatoa kiasi fulani cha fedha na kuanzisha mfuko wa matibabu, ili kuwalipia wakulima walioshiriki kwenye mfumo huo kiasi fulani cha gharama za matibabu. Hivi sasa, mfumo huo mpya umeanza kutekelezwa kwenye zaidi ya asilimia 30 ya sehemu za vijijini kote nchini China.

Bw. Ma Shichun ni mkulima wa kawaida wa wilaya ya Changyang mkoani Hubei, na alikuwa na tatizo la moyo la kuzaliwa nalo. Kutokana na mzigo mkubwa wa kiuchumi wa kumsomesha mtoto wake, hakuenda kupata matibabu ya upasuaji, hivyo afya yake ilikuwa ikiathiriwa siku hadi siku. Hadi kufikia mwaka 2003 ambapo mtoto wake alihitimu shule, na mfumo mpya wa ushirikiano wa matibabu ulianza kutekelezwa huko, aliamua kufanyiwa upasuaji.

Upasuaji huo na matibabu husika yaligharamu yuan elfu 60, na mfuko wa ushirikiano wa matibabu ulimlipia yuan elfu 10. Bw. Ma Shichun alisema:

"niliomba mkopo wa yuan elfu 10 kutoka benki kwa ajili ya kulipa gharama za matibabu, na nililipia mkopo huo kwa fedha nilizopewa na mfuko wa ushirikiano wa matibabu. Kwa kweli, mfuko huo ulisaidia kutatua tatizo kubwa."

Mji wa Dujiangyan mkoani Sichuan ni sehemu moja ambapo mfumo mpya wa ushirikiano wa matibabu unatekelezwa, ofisa mmoja wa mji huo Bw. Sen Lin alisema, wakulima wanaoshiriki kwenye mfumo huo wameanza kujipatia matibabu mara moja wakiwa wagonjwa, na wakulima wamepunguziwa kidhahiri mzigo wa gharama za matibabu. Alisema, tangu mji wa Dujiangyan uchaguliwe kuwa mji wa majaribio wa kutekeleza mfumo mpya wa ushirikiano wa matibabu mkoani Sichuan mwaka 2003, kiwango cha matibabu ya wakulima kimeinuka, na mfumo huo unakaribishwa na kuungwa mkono na wakulima.

Mfumo mpya wa ushirikiano wa matibabu si kama tu unawapunguzia wakulima mzigo wa kiuchumi, bali pia unaziongezea mapato idara za matibabu za ngazi ya shina vijijini. Vituo vya huduma za afya vya tarafa na wilaya vinatumia nyongeza ya mapato yaliyoongezeka kununua vifaa vya matibabu na kutoa mafunzo kwa madaktari na kuinua kiwango cha matibabu. Hali hiyo imesababisha mzunguko mzuri. Kuhusu hali hiyo, daktari wa kituo cha huduma za afya cha tarafa ya Moshi ya wilaya ya Changyang mkoani Hubei Bw. Hu Youxu alisema:

"zamani kituo chetu kilipokea wagonjwa 6 hadi 8 wa kulazwa kwa siku, hivi sasa ni wagonjwa 18 hadi 20 kwa siku, wakiwa wengi kabisa itafikia 30. mfumo huo mpya unawanufaisha wakulima na kusukuma mbele maendeleo ya hospitali, umeleta manufaa ya pande mbalimbali."

Kutokana na mafanikio ya mfumo huo mpya wa ushirikiano wa matibabu vijijini, serikali ya China imeamua kuongeza kiwango cha ruzuku kwa wakulima wanaoshiriki kwenye mfumo huo kuanzia mwaka huu, na kupanua hatua kwa hatua eneo la majaribio la kutekeleza mfumo huo na kuutekeleza rasmi mfumo huo kwenye sehemu zote za vijijini nchini China katika miaka mitano ijayo. Waziri wa afya wa China Bw. Gao Qiang alisema:

"idara za fedha za serikali kuu na serikali za mitaa zinapaswa kuongeza ruzuku kwa wakulima wanaoshiriki kwenye mfumo huo, ili kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya maendeleo ya mfumo huo mpya wa ushirikiano wa matibabu vijijini."

Hivi karibuni, wizara ya afya ya China ilitoa mpango wa maendeleo ya miaka mitano ijayo. Mpango huo umeagiza kuwa, katika miaka mitano ijayo, serikali ya China itatenga yuan zaidi ya bilioni 20 katika ujenzi wa miundombinu ya huduma za afya vijijini, hasa kuimarisha na kukamilisha mfumo wa huduma za afya vijijini za ngazi tatu yaani wilaya, tarafa na kijiji, na kuimarisha kazi ya kuwapa wataalamu wa huduma za afya vijijini na kutoa mafunzo kwa madaktari wa wilaya na vijiji, kuboresha miundo ya ujuzi na uwezo wa kutoa huduma wa watumishi wa huduma za afya vijijini, na kupeleka maelfu ya madakari hodari wa hospitali za mijini kwenda kufanya kazi kwenye idara za matibabu vijijini kila mwaka.

Idhaa ya Kiswahili 2006-02-08