Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-09 16:11:23    
Msanifu wa mavazi ya kabila la Wahui Bi. Ma Shumin

cri

Kabila la Wahui ni moja ya makabila madogo madogo yenye idadi kubwa ya watu nchini China, walienea katika sehemu mbalimbali nchini China. Kutokana na kuishi pamoja na makabila mengine kwa muda mrefu, umaalum wa mavazi yao umekuwa ukififia siku hadi siku. Mavazi ni alama muhimu inayotofautisha utamaduni wa makabila mbalimbali, hivyo kila kabila linaona fahari kwa kuwa na utamaduni wa mavazi yao maalum.

Katika mashindano ya usanifu wa mavazi ya kabila la Wahui, mavazi yaliyosanifiwa na Bi. Ma Shumin yalisifiwa zaidi na watazamaji, na yalipewa karibu medali zote kwenye mashindano hayo. Kati ya mavazi aliyosanifu, kuna mavazi yanayovaliwa wakati wa kufanya kazi, mavazi ya kushiriki katika tafrija za usiku, mavazi ya kidini, na mavazi ya vijana wanaocheza ngoma za mitaani. Mavazi hayo yote yanaonesha umaalum wa kabila la Wahui katika rangi, mapambo na sifa ya vitambaa.

Mvulana wa kabila la Wahui Bw. Xu Jie alisema, mavazi yaliyosanifiwa na Bi. Ma Shumin yanaweza kuonesha tabia ya watu wa kabila la Wahui ya kujizuia na kupenda kufanya mambo kufuata mtazamo wake, akisema:

"Naona Bi. Ma Shumin si kama tu ni msanii maarufu wa kabila la Wahui, bali pia ni wa waislamu wote nchini China. Amefanya utafiti kuhusu utamaduni wa mavazi ya kabila la Wahui kwa miaka mingi na kusanifu aina nyingi za mavazi yanayowafaa waislamu wengi."

Shughuli za dini zinachukua sehemu muhimu ya maisha ya watu wa kabila la Wahui wanaoamini dini ya kiislamu. Wanaswali mara tano kwa siku moja nyumbani, na wanakwenda kuswali msikitini kila Ijumaa, na kufunga kwa mwezi mmoja kila mwaka, shughuli za dini zinahusiana na mambo yote ya waislamu. Bi. Ma Shumin aliyezaliwa katika familia ya kabila la Wahui alifanya usanifu wa mavazi kufuatana na hali halisi ya maisha ya waislamu.

Bi. Ma Shumin alisema, anaposanifu mavazi ya aina mbalimbali, anazingatia vya kutosha upendo na umaalum wa kabila la Wahui. Akisema:

Sauti

"Watu wa kabila la Wahui wanapenda rangi nyeupe, kijani na buluu, hivyo mimi huchagua vitambaa vyenye rangi hizo wakati wa kusanifu mavazi yanayovaliwa baada ya kuoga, ya swala na ya wakati wa mfungo wa ramadhani. Wahui wanapenda kutarizi, hivyo napamba mavazi kwa michoro ya kutarizi."

Kabila la Wahui nchini China lilianzishwa rasmi katika karne ya 13, ambapo watu wengi kutoka Asia ya kati, waarabu na waajemi walikuja China wakijichanganya na watu wa kabila la Wahan na la Wauygur, na siku hadi siku kabila la Wahui likaundwa. Hivi sasa watu wa kabila hilo wameenea katika sehemu mbalimbali nchini China, lakini hawana lugha wala maandishi. Na mavazi ya Wahui hayana mtindo maalum kama makabila madogo madogo mengine nchini China, ila tu wanaume huvaa kofia nyeupe na wanawake huvaa hijabu wakati wa kuswali. Hivyo Bi. Ma Shumin anataka kutoa mchango wake kuyafanya mavazi ya kabila la Wahui yawe na mtindo wake pekee. Akisema:

"Natumai kuwa, watu wa kabila la Wahui watakuwa na mavazi yao maalum kwa ajili ya sherehe au tafrija maalum ya kikabila. Mavazi ni lugha ya kabila moja, lakini hivi sasa mavazi maalum ya kabila la Wahui bado hayajaanza kushonwa, nasikitishwa sana."

Bi. Ma Shumin aliwahi kusanifu sura za wahusika wengi wa filamu au filamu za telivisheni. Sasa amekaribia kufika umri wa miaka 60, lakini anaendelea kufundisha katika chuo kikuu akiwa profesa.

Aliposanifu mavazi yanayovaliwa kazini au wakati wa kupumzika, Bi. Ma Shumin alizingatia desturi ya kuvaa ya Wahui, kwa mfano, vijana wa kabila la Wahui wanapenda kuvaa vizibao, Bi. Ma Shumin alisanifu aina nyingi za vizibao vyenye mitindo ya kisasa. Aliposanifu mavazi ya vijana wanaopenda kucheza ngoma za mitaani, mavazi ya juu yana kola ya kusimama, kitambaa kinang'ara, na kuweka vishikizo vyenye rangi ya fedha kwenye mkanda wenye rangi nyeusi, suruali za wavulana zina urefu wa asilimia 70 tu wa kawaida, na wasichana wanasanifiwa suruali za sketi, wanapocheza ngoma wanaonekana maridadi sana.

Mume wa Ma Shumin Bwana Ma Weili pia ni wa kabila la Wahui, wanafanya kazi katika chuo kikuu kimoja. Bwana Ma Weili alimwunga mkono mke wake kwa juhudi katika usanifu wa mavazi. Inasemekana kuwa katika mkoa unaojiendesha wa kabila la Wahui wanakoishi watu wengi wa kabila la Wahui, baadhi ya wafanyabiashara wanatumai kuwa mavazi aliyoyasanifu Bi. Ma Shumin yatangenezwa kwa wingi. Bw. Ma Weili alisema:

"Mavazi ya kikabila yanapaswa kuvaliwa na watu wengi, ama sivyo hayawezi kuitwa mavazi ya kikabila. Mchakato wa kuunda utamaduni wa mavazi ya kikabila unahitaji juhudi za watu mbalimbali, pamoja na wasanifu na wafanyabiashara kuhimiza uuzaji, pia unahusiana na kiwango cha elimu cha vijana."

Bw. Ma Weili alisema japo si rahisi kuanzisha utamaduni wa mavazi ya kabila la Wahui, lakini watu hawataacha juhudi hizo.

Idhaa ya kiswahili 2006-02-09