Shirika la Afya ya Wanyama Duniani, tarehe 8 lilitoa taarifa ikisema homa ya mafua ya ndege ilizuka katika jimbo la Kaduna kaskazini mwa Nigeria. Hii ni mara ya kwanza kwa ugonjwa huo kutokea barani Afrika. Wataalamu wanaona kuwa kutokana na hali duni ya matibabu barani Afrika, kuibuka kwa ugonjwa huo ni changamoto kubwa kwa mfumo wa kinga na udhibiti wa ugonjwa huo barani humo. Hivi sasa tukio hilo limepewa uzito mkubwa na Shirika la Afya Duniani, WHO.
Taarifa ilieleza kuwa, ugonjwa huo umetokea kwenye kiwanja kimoja cha ufugaji wa kuku kijijini Jaji kwenye jimbo la Kaduna, kaskazini mwa Nigeria. Baadaa ya kuchunguza sampuli ya kuku waliokufa katika maabara nchini Italia, virusi vya H5N1 vya ugonjwa huo vimethibitishwa. Kisha serikali ya Nigeria ikatoa ripoti ya tukio hilo kwa Shirika la Afya ya Wanyama Duniani.
Waziri wa kilimo wa Nigeria Bw. Adamu Bello tarehe 8 kwenye mkutano wa baraza la serikali alisema, serikali ya Nigeria imechukua hatua za dharura kuchinja kuku wote, kusafisa kwa dawa na kuweka karantini kwenye kiwanja hicho, na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani na Shirika la Afya Duniani pia yatachukua hatua za dharura. Hivi sasa kikundi cha wataalamu kiko safarini kwenda kwenye sehemu ulipotokea ugonjwa ili kupima hali ilivyo na kutoa mapendekezo. Bw. Bello alisema, serikali ya Nigeria itatenga kiasi cha dola za Kimarekani milioni 13 hadi 15 ili kupambana na ugonjwa huo na kulipa hasara kwa watakaoathirika.
Aidha, Bw. Bello alitangaza kuwa hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyegunduliwa kuambukizwa ugonjwa huo, lakini uwezekano upo kutokana na hali duni ya matibabu.
Habari nyingine zinasema ugonjwa huo pia umetokea katika sehemu nyingine ya kaskazini ya Nigeria, na katika sehemu iliyo karibu na kijiji cha Jaji kuku pia wameanza kufa kwa wingi, lakini baada ya kufanya uchunguzi wa maabara imethibitishwa kuwa kuku hao walikufa kutokana na mdondo, lakini wataalamu wanasema kutokana na hali duni ya matibabu matokeo ya uchunguzi huo pengine hayaaminiki.
Kutokana na kuwa bara la Afrika ni eneo la wanyama wanaohama hama duniani, hivi sasa haijajulikana kama ugonjwa huo wa homa ya mafua ya ndege unahusiana na ndege hao. Bw. Bello anaona kuwa biashara ya magendo ya nyama ya ndege kutoka nchi za nje pengine ni chanzo cha ugonjwa huo.
Uchunguzi wa maabara umethibitisha kuwa virusi H5N1 vilivyotokea nchini Nigeria vinafanana na virusi vilivyotokea barani Asia. Kwa sababu virusi vya aina hiyo vinaambukiza kwa kasi, wataalamu wana wasiwasi kuwa virusi hivyo vitaenea haraka katika sehemu nyingine za Afrika endapo hatua za dharura hazitachukuliwa mara moja. Barani Afrika wafugaji wengi wanafuga kienyeji, hali hiyo imerahisisha maambukizi ya ugonjwa huo. Zaidi ya hayo, wafugaji wanaishi pamoja na mifugo na watu wanakaa na mifugo pamoja kwenye magari katika uchukuzi. Mazingira kama hayo ni hatari kwa binadamu kuambukizwa virusi.
Hivi sasa, ingawa hakuna ripoti kuhusu ugonjwa huo nje ya Nigeria barani Afrika, lakini kutokana hali duni ya mfumo wa kinga na udhibiti, kama ugonjwa huo ukitokea katika nchi nyingine hali itakuwa ya kutisha.
Katibu mkuu wa WHO alisema, shirika lake linatilia mkazo hali ya ugonjwa huo barani Afrika, ingawa serikali ya Nigeria haijawaalika wataalamu wa WHO kwenda kwenye sehemu yenye ugonjwa huo kufanya uchunguzi, lakini shirika hilo litaisaidia Nigeria kadiri iwezavyo katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Idhaa ya kiswahili 2006-02-09
|