Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Russia Sergei Kiriyenko siku chache zilizopita alisema, Russia imeialika Iran kushiriki katika ujenzi wa kituo cha kwanza cha kimataifa cha kusafisha uranium nchini Russia, kutokana na hayo, Iran pengine itakuwa nchi ya kwanza kushiriki katika ujenzi wa kituo hicho.
Hii inamaanisha kuwa pendekezo la kujenga "mfumo wa kimataifa wa vituo vya nishati ya atomiki" lililotolewa na rais Vladimir Putin mwezi uliopita linatazamiwa kutekelezwa, na hivyo italeta tumaini finyu la kutatua suala la nyuklia la Iran ambalo linazidi kuwa na hali mbaya kila kukicha.
Kujenga "mfumo wa kimataifa wa vituo vya nishati ya atomiki" ni wazo lililotolewa na rais Putin wa Russia mwishoni mwa mwezi uliopita. Kutokana na wazo hilo, nchi husika zitaanzisha duniani mfumo wa huduma za kuendeleza nishati ya nyuklia kwa ajili ya matumizi ya amani, na kutoa huduma kwa nchi zote ikiwemo huduma ya kusafisha uranium chini ya uanglizi na udhibiti wa Shirika la Nishati ya Atomiki Duniani.
Naibu mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Russia Sergei Antipov mwanzoni mwa mwezi huu aliwaambia waandishi wa habari kuwa, kituo cha kwanza cha kimataifa cha nishati ya atomiki kitajengwa katika sehemu ya Siberia kwa sababu huko mazingira yanafaa kujenga kituo kama hicho. Tarehe 8 mkuu wa Shirika hilo Bw. Kiriyenko alisema, tarehe 16 ujumbe wa ngazi ya juu wa Iran utatembelea Russia, na yeye atafanya ziara ya kikazi nchini Iran mwishoni mwa mwezi huu.
Wachambuzi wanaona kuwa juhudi za Russia za kutaka kujenga kituo hicho zinatokana na sababu tatu: Kwanza, itasaidia kuhifadhi uhusiano kati ya Russia na Iran. Iran ni nchi mwenzi muhimu wa Russia katika uchumi, na pande mbili zina uhusiano wa karibu katika mambo ya viwanda vya silaha na safari za anga ya juu, katika wakati ambapo jumuyia ya kimataifa inataka Iran isimamishe shughuli za nyuklia ukiwemo utafiti wa nyuklia, ni vibaya kuendelea kuiunga mkono Iran wazi wazi, kama pendekezo la kuanzisha mfumo wa kimataifa wa vituo vya nishati ya atomiki ukikubaliwa, uhusiano mzuri kati ya nchi hizo mbili utaendelea. Pili, Iwapo pendekezo hilo likikubaliwa na kutekelezwa, basi Russia ikiwa ni mwanzishi na mwendeshaji wa mfumo huo itapata faida kubwa ya kiuchumi. Tatu na ni muhimu kwamba pendekezo hilo litaondoa nia ya Iran kuendeleza silaha za nyuklia na kuifanya Marekani ishindwe kupata kisingizio cha kuingilia kati mambo ya sehemu ya Caspian Sea na Iran, na usalama wa Russia utahakikishwa.
Hivi sasa Iran imefurahishwa na pendekezo hilo la Russia. Mwezi huu, pande mbili zilikutana mara nyingi kuhusu Iran kushiriki katika ujenzi wa kituo cha kwanza cha kimataifa cha nishati ya atomiki. Lakini kwa sasa bado ni vigumu kusema wazi kwamba Iran itakubali pendekezo hilo la Russia, kwa sababu siku zote Iran inataka haki yake ya kumiliki zana za nyuklia, na pendekezo la Russia haliwezi kukidhi haki yake hiyo.
Mpaka sasa Marekani haijasema lolote kuhusu pendekezo hilo la Russia, lakini rais Bush aliwahi kutoa pendekezo lake la kuanzisha "ghala la kimataifa la nishati ya nyuklia", kwa mujibu wa pendekezo hilo kila nchi inaweza kupata nishati ya nyuklia kwa ajili ya matumizi ya amani. Kutokana na kuwa pendekezo la Marekani na la Russia yanafanana, kwa hiyo pengine Marekani itakubali pendekezo la Russia.
Lakini "mfumo wa kimataifa wa vituo vya nishati ya atomiki" ni mradi kabambe, hauwezi kupatikana kwa urahisi na kusaidia utatuzi wa mgogoro unaozidi kuwa katika hali mbaya siku hadi siku, "maji ya mbali hayakati kiu mara moja", na kuanzishwa kwa mfumo huo hauwezi kukamilishwa na Russia peke yake. Kwa hiyo pendekezo la Russia likiweza kusaidia utatuzi wa suala la nyuklia la Iran, linategemea juhudi za pamoja za jumuyia ya kimataifa.
Idhaa ya kiswahili 2006-02-10
|