Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-10 17:03:54    
Mchina wa kwanza anayewahudumia watalii wa China waliokwenda kutalii nchini Kenya

cri

Bw. Yang Che

Kenya ni nchi yenye vivutio vingi vya utalii, tokea Kenya itangazwe kuwa nchi inayowapokea watalii kutoka China mwishoni mwa mwaka 2003, idadi ya wachina wanaokwenda Kenya kutalii imeongezeka siku hadi siku.

Bwana Yang Che na mke wake Bi. Xue Wenying walikuwa wawili miongoni mwa Wachina wa waliotangulia kwenda barani Afrika kutafuta njia ya kujiendeleza baada ya China kufungua mlango kwa nchi za nje, waliwahi kuendesha zahanati ya kichina, mkahawa wa kichina na duka la kuuzia bidhaa za kichina nchini Kenya. Bw. Yang Che alisema:

"Tulipofika nchini Kenya hatukujua mambo yoyote kuhusu nchi hiyo, wala hatukufahamu lugha, lakini baada ya kuishi nchini Kenya kwa miaka miwili, kuanzia mwaka 1993 tulianza kufanya biashara kwa kuagiza bidhaa kutoka China."

Bw. Yang Che alikuwa Mchina wa kwanza aliyeuza wanasesere kutoka China, aliwahi kufanya biashara ya tai, magari, kompyuta, nguo na bidhaa za matumizi ya kila siku, yeye pia alikuwa Mchina wa kwanza aliyesajili kampuni ya utalii nchini Kenya.

Miaka kadhaa kabla ya China kuwaruhusu Wachina kutalii nchini Kenya, Bwana Yang Che aliona kuwa, kutokana na kuinuka kwa kiwango cha maisha ya Wachina, idadi ya Wachina waliokwenda nchi za Asia kusini na nchi za Ulaya kwa utalii imeongezeka mwaka hadi mwaka, akafahamu kuwa iko siku ambapo Wachina wataanza kutalii katika nchi za Afrika, alisajili kampuni ya utalii ya Longren ya Kenya mwaka 1998. Mwanzoni kampuni yake iliwapokea Wachina waliokwenda Kenya kufanya ukaguzi wa soko, na Wachina wote waliotembelea Kenya walisifu sana mandhari nzuri ya kimaumbile na kuwepo kwa wanyama wengi wa aina mbalimbali nchini Kenya. Bw. Yang Che ametoa mchango mkubwa katika kuhimiza Wachina waruhusiwe kuanza kufanya utalii nchini Kenya. Akisema:

"Waziri wa utalii wa wakati huo wa Kenya Bwana Kalonzo Musyoka ni rafiki yangu mkubwa. Nilimfahamisha mara nyingi hali ya maendeleo ya kiuchumi ya China na hali ya kupanuka mwaka hadi mwaka kwa soko la watalii wa China."

Wakati huo, kutokana na ofisi za ubalozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania kukumbwa milipuko ya kigaidi kwa wakati mmoja, na tukio la "Septemba 11", nchi za magharibi ziliwaonya raia wao wasiende katika nchi za Afrika mashariki kwa utalii kutokana na hofu ya kushambuliwa na magaidi, hivyo sekta ya utalii ya Kenya iliyotegemea sana watalii kutoka nchi za magharibi ilizorota mara moja. Baada ya kusikiliza maelezo ya Bw. Yang Che kuhusu soko la watalii nchini China, Bwana Musyoka alifurahi sana akijaribu chini juu kueleza matakwa ya Kenya kupewa hadhi ya kutembelewa na watalii wachina na serikali ya China. Mwezi Desemba mwaka 2003 wakati wa mkutano wa pili wa mawaziri wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, Kenya na nchi nyingine 7 za Afrika zilitangazwa rasmi kuwa nchi zitakazoweza kupokea watalii kutoka China.

Ili kuwafahamisha wachina hali ya vivutio vya utalii vya Kenya, mwaka 2002 kampuni ya utalii ya Longren ya Kenya ilifungua ofisi yake mjini Beijing na kuchapisha vitabu vya picha. Bw. Yang Che mwenyewe alienda katika mashirika mbalimbali ya utalii ya Beijing kutoa mihadhara kuhusu vivutio vya utalii vya Kenya, zana na huduma za utalii nchini Kenya na kadhalika.

Chini ya juhudi za pande mbalimbali, watu wa China walianza kufahamu hatua kwa hatua kuhusu mazingira ya utalii nchini Kenya, na idadi ya watalii wa China wanaoenda kutalii nchini Kenya inaongezeka siku hadi siku. Katika mwaka huu mpya wa jadi ya kichina, watalii zaidi ya 1000 wa China walikwenda Kenya kutalii na kutazama wanyama pori.

Bw. Yang Che alisema:

"Vitu vya Kenya vinavyowavutia zaidi watalii wa China ni wanyama pori, mazingira ya kimaumbile, hali nzuri ya hewa, na maua yanayochanua wakati wote. Wachina wote waliowahi kufika nchini Kenya hawawezi kujizuia kuisifu Kenya kwa vivutio vya utalii. Hususan mashabiki wa kupiga picha wanaipenda Kenya sana kutokana na kuwepo kwa wanyama wengi."

Kampuni ya Bw. Yang Che ina mabasi madogo matatu na magari madogo kadhaa, pamoja na waongozaji wa utalii wa kichina, inaweza kuwapokea watalii kumi kadhaa kwa mara moja. Imefahamika kuwa, hivi sasa kampuni 4 zilizowekezwa na wachina zinashughulikia utalii nchini Kenya, pia zimeunda kikosi cha viongozi wa utalii wa Kichina. Lakini kutokana na sababu mbalimbali, hivi sasa idadi ya watalii wa China wanaokwenda Kenya kutalii bado ni ndogo. Bw. Yang Che akisema:

"Sababu ya kwanza, wachina wengi bado hawajafahamu hali halisi ya nchi za Afrika, wengi wao wanafikiri kuwa Afrika ni bara lililoko mbali sana na lenye maajabu. Ya pili, njia ya kuwasiliana na watalii bado haijakamilika, watu wengi bado hawajui namna ya kujiandikisha na ujumbe wa utalii wa kwenda Kenya. Na sababu nyingine ambayo pia ni muhimu zaidi ni gharama kubwa."

Bw. Yang Che alisema lengo la kutalii nchini Kenya ni kutazama wanyama pori, lakini tikiti za kuingia kwenye mbuga za wanyama pori ni dola za kimarekani 30 kwa siku kwa mtu mmoja, pamoja na gharama kubwa ya hoteli na mawasiliano ya barabara, ni vigumu kupunguza gharama za kutalii nchini Kenya. Hivi sasa gharama za kutalii nchini Kenya peke yake zinalingana na gharama ya kutalii katika nchi tano za Ulaya.

Bw. Yang Che aliyeishi nchini Kenya kwa miaka 15 anaipenda sana Kenya. Alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, anawakumbuka marafiki zake wa Kenya, anapenda mandhari nzuri ya Kenya, japokuwa hivi sasa yuko nchini China, lakini kila akifumba macho yake hujisikia kama amerudi nchini Kenya, anaweza kusikia herufi nzuri ya nyasi ndefu, na kuwaona wanyama pori wanaohamia kutoka Serengeti Tanzania hadi mbuga ya wanyama pori ya Masai Mara ya Kenya, Korongo wa ziwa la Nakuru na mlima Kenya.

Bw. Yang Che alieleza imani yake kuwa, Kenya ina vivutio vizuri vya utalii, kadiri siku zinavyokwenda ndivyo wachina wanavyofahamu zaidi kuhusu vivutio vya utalii vya Kenya, na idadi ya watalii wa China watakaokwenda Kenya kusafiri pia itaongezeka mwaka hadi mwaka.

Idhaa ya kiswahili 2006-02-10