Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-10 17:00:53    
Nchi za Afrika zakaribisha waraka wa sera ya China kwa Afrika

cri

Tarehe 12 Januari, serikali ya China ilitoa waraka wa sera ya China kwa Afrika, ambao unaeleza malengo ya sera ya China kwa Afrika, kuweka mipango kuhusu ushirikiano kati ya pande hizo mbili katika sekta mbalimbali katika siku za usoni, na kuhimiza uhusiano kati ya China na Afrika kupata maendeleo yenye utulivu na ya muda mrefu. Waraka huo umekaribishwa na nchi mbalimbali za Afrika.

Tarehe 19 wataalamu, wasomi, wanadiplomasia na wahusika wa vyombo vya habari vya nchi za Afrika walikusanyika pamoja huko Pretoria Afrika ya kusini, wakikaribisha kwa shangwe kutolewa kwa waraka wa sera ya China kwa Afrika. Waliona kwa kauli moja kuwa, waraka huo utaimarisha zaidi uhusiano kati ya China na nchi za Afrika, na kusukuma mbele ushirikiano kati ya pande hizo mbili uingie katika kipindi kipya katika karne mpya.

Kaimu wa mkurugenzi wa taasisi ya utafiti wa masuala ya Afrika ya Afrika ya kusini Bwana John Tesa alisema, waraka wa sera ya China kwa Afrika umetolewa katika wakati mwafaka, ambao si kama tu umejumulisha uhusiano wa kirafiki kati ya China na Afrika uliokuwepo kwa miongo kadhaa, bali pia umesanifu ramani nzuri ya kukuza ushirikiano kati ya China na Afrika na ushirikiano kati ya kusini na kusini katika karne mpya.

Mkurugenzi wa taasisi ya mazungumzo ya duniani Bwana John Leper alisema, waraka wa sera ya China kwa Afrika ni waraka wa mwongozo kwa ushirikiano wa kimkakati kati ya Afrika na China katika siasa, uchumi, utamaduni na maeneo mengine.

Bwana Endumisou Entesinga wa Afrika ya kusini atakayekuwa balozi wa Afrika kusini nchini China alisema, katika miaka zaidi ya 50 iliyopita, China imetoa misaada mikubwa kwa nchi za Afrika, na kuziunga mkono nchi za Afrika bila kutafuta ubinafsi katika mapambano ya kujipatia uhuru na juhudi za ujenzi wa kiuchumi. Alisema ushirikiano kati ya Afrika na China utakuwa na mustakabali mzuri.

Balozi wa Zambia nchini Afrika ya kusini Bwana Senot Mubula alisema, Zambia na China zimedumisha uhusiano wa kirafiki kwa miaka zaidi ya 40, zamani China iliiunga mkono Zambia katika mapambano dhidi ya ukoloni, na kuisaidia kujenga reli ya TAZARA. China imetoa mchango mkubwa kwa nchi za Afrika na bila shaka imepata heshima kubwa kutoka kwa watu wa Afrika. Hivi sasa mabadiliko makubwa yametokea, katika zama hizi yenye utandawazi wa kiuchumi duniani, watu wa Zambia wanawakaribisha wachina kuwekeza vitega uchumi nchini Zambia.

Balozi wa Senegal nchini Afrika ya kusini Bwana Samba Mubup alisema, nchi za Afrika na China zina urafiki wa jadi tangu enzi na dahari, hivi sasa pande hizo mbili zitashirikiana kujiendeleza katika maeneo mbalimbali. Bara la Afrika ni chanzo cha ustaarabu wa binadamu, lina historia ndefu ya kiustaarabu. Nchi za Afrika zinahitaji msaada wa China, zinapaswa kuimarisha ushirikiano kati yake na China, ili kukuza zaidi ustaarabu wake.

Tarehe 4 Februari, waziri wa utalii wa Kenya Bwana Moris Delonzo alipohojiwa na mwandishi wa habari wa China huko Nairobi alisema, China siku zote iliziunga mkono nchi za Afrika katika mapambano yao ya kujipatia uhuru na juhudi zao za kujiendeleza, amefurahia juhudi zilizofanywa na China katika kuhimiza ushirikiano kati ya pande hizo mbili.

Bw. Delonzo alisema China siku zote inaheshimu uhuru na mamlaka ya nchi za Afrika, hata wakati huu ambapo China inastawi siku hadi siku, haina shauku ya kuingilia kati mambo ya nchi za Afrika kama baadhi ya nchi za magharibi zilivyofanya, bali ina msaada bila ya sharti lolote katika ujenzi wa nchi za Afrika.

Bw. Delonzo alipotembelea China mwaka jana akifuatana na rais Mwai Kibaki, alipata picha nzuri sana kuhusu mafanikio ya kiuchumi yaliyopatikana nchini China na sura nzuri ya watu wa China. Alisema maarifa ya China ya kujiendeleza kwa kujitawala na kujiamulia na kujitegemea kwa ukakamavu yanastahiki kuigwa na nchi za Afrika. China ni mfano mzuri wa kuigwa kwa nchi za Afrika katika kujiendeleza kiuchumi kwani zamani China ilikuwa nchi maskini kama ilivyo kwa nchi nyingi za Afrika.

Balozi wa China nchini Algeria Bw. Wang Wangsheng tarehe 6 huko Algiers alifanya mkutano na waandishi wa habari kuhusu waraka wa sera ya China kwa Afrika, akisema waraka wa sera ya China kwa Afrika utaimarisha urafiki na ushirikiano kati ya China na Afrika, kuihimiza jumuiya ya kimataifa kufuatilia zaidi nchi za Afrika, na kuhimiza maendeleo ya uwiano na masikilizano duniani.

Balozi Wang alisema huo ni waraka wa kwanza wa sera ya China kwa Afrika uliotolewa na serikali ya China, hasa ni hatua moja muhimu ya kidiplomasia ya China kwa nchi za Afrika.

Balozi Wang alisema serikali ya China siku zote inatilia maanani kukuza uhusiano kati yake na nchi za Afrika. Waraka huo umetoa malengo na hatua halisi za kuimarisha ushirikiano kati ya China na Afrika katika sekta zaidi ya 30 zikiwemo siasa, uchumi, elimu, amani na usalama na hatua za kutekeleza malengo hayo.

Idhaa ya kiswahili 2006-02-10