Maambukizi ya homa ya mafua ya ndege yaliibuka ghafla hivi karibuni kwenye nchi za Ulaya, ambazo zilikuwa na tahadhari kubwa juu ya maradhi hayo. Katika nchi nyingi za Ulaya, kulikuwa na sehemu kadhaa ambazo bata maji, kuku na mabata walikufa kutokana na kuambukizwa virusi vya homa ya mafua ya ndege. Hali halisi inaonesha kuwa nchi za Ulaya pia zinakabiliwa na changamoto ya maambukizi ya ugonjwa wa aina hiyo.
Wizara ya afya ya Slovenia tarehe 12 iliwasilisha taarifa kwa kamati ya Umoja wa Ulaya ikisema, maabara kuhusu maambukizi ya virusi vya homa ya mafua ya ndege ya nchi hiyo imethibitisha kuwa bata maji mmoja alikufa kutokana na homa ya mafua ya ndege, mwili wa bata huyo hivi sasa umepelekwa katika maabara ya Umoja wa Ulaya iliyoko nchini Uingereza kwa utafiti zaidi.
Siku moja kabla ya hapo kulikuwa na nchi nne za Umoja wa Ulaya, ambazo zilitoa taarifa kuhusu maambukizi mapya ya ugonjwa huo katika nchi zao. Wizara ya afya ya Italia tarehe 11 ilithibitisha kwamba hivi karibuni katika nchi yao kulikuwa na bata maji watano kati ya zaidi ya 10 waliokufa ghafla, ambao wamethibitishwa walikufa kutokana na kuambukizwa virusi vya homa ya mafua ya ndege vya aina ya H5N1. Taarifa hiyo imesema ndege hao walitoka sehemu ya Balgan.
Siku hiyo wizara ya kilimo ya Ugiriki ilisema, maabara ya Umoja wa Ulaya iliyoko nchini Uingereza imethibitisha, bata maji watatu waliokufa siku 11 zilizopita walikufa kutokana na kuambukizwa virusi vya homa ya mafua ya ndege vya aina ya H5N1. Lakini bata hao walifia porini, na wala siyo sehemu ya vijiji. Mbali na hayo, uligunduliwa mwili wa bata pori mmoja aliyekufa kwenye kisiwa cha bahari ya Aegean, upimaji wa mwanzo unaonesha kwamba bata huyo aliambukizwa virusi vya homa ya mafua ya ndege vya H5N1. Hivi sasa serikali ya Ugiriki imechukua hatua ya usimamizi na udhibiti. Kwa bahati nzuri, katika siku 11 zilizopita baada ya kugundua kwa bata huyo aliyekufa, hakukuwa na kuku au mabata walioambukizwa virusi vya aina hiyo nchini Ugiriki.
Taarifa iliyotolewa siku hiyo na wizara ya kilimo na misitu ya Bulgaria ilisema, maabara ya Umoja wa Ulaya iliyoko Uingereza siku hiyo alasiri ilithibitisha kuwa swan waliokufa tarehe 3 nchini Bulgaria, wakufa kutokana na kuambukizwa virusi vya homa ya mafua ya ndege ya aina ya H5N1. Idara ya madaktari wa mifugo ya Bulgaria imepeleka kikundi cha wataalamu kufanya usimamizi mchana na usiku kwenye sehemu ya kaskazini magharibi ya nchi hiyo ambapo aligunduliwa bata maji aliyekufa, kwa makundi ya ndege waliotua huko pamoja na kuku na mabata wanaofugwa huko. Aidha wanakusanya sampuli za kuku na mabata wanaofungwa kwenye eneo karibu na ndege aliyekufa, na sampuli hizo zimepelekwa katika maabara za serikali kwa utafiti zaidi.
Idara za afya za Romania siku hiyo zilithibitisha, maambukizi ya virusi vya H5N1 yaliibuka kwenye kijiji kimoja kilichoko sehemu ya mashariki ya nchi hiyo, ambapo kuku 57 wamekufa, serikali ya huko imechukua hatua ya kukiweka kijiji hicho kwenye karantini, kuchinja kuku na mabata zaidi ya elfu 20 wanaofugwa katika kijiji hicho na kunyunyiza dawa ya kuua vijidudu. Hiyo ni sehemu ya nne yenye maambukizi ya homa ya mafua ya ndege tokea mwaka huu nchini Romania. Wizara ya ulinzi ya Romania imepeleka askari 50 kwenda kutoa msaada.
Ili kuzuia maambukizi mapya ya virusi vya homa ya mafua ya ndege, kamati ya Umoja wa Ulaya ilitoa mpango tarehe 10 kuhusu maambukizi ya virusi. Habari zinasema kamati husika ya Umoja wa Ulaya imeamua kuitisha mkutano tarehe 16 na 17 kujadili hali ya maambukizi ya virusi vya homa ya mafua ya ndege yaliyoibuka nchini Italia, Ugiriki na Slovenia na hatua za udhibiti. Wataalamu na maofisa husika wamesema, hivi sasa afya za watu wa nchi za Ulaya bado hazijatishiwa sana kutokana na kwamba bata maji waliokufa kutokana na kuambukizwa virusi vya aina ya H5N1 vya homa ya mafua ya ndege ni ndege pori.
Idhaa ya Kiswahili 2006-02-13
|