Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-13 20:04:52    
Lengo la kimkakati la safari ya waziri wa ulinzi wa Marekani katika nchi za Afrika kaskazini

cri

Waziri wa ulinzi wa Marekani Bwana Donald Rumsfeld tarehe 11 alianza ziara rasmi katika nchi tatu za Afrika kaskazini za Tunisia, Algeria na Morocco. Hii ni mara ya kwanza kwa Bwana Rusmfeld kuzitembelea nchi za Afrika kaskazini tangu ashike madaraka ya waziri wa ulinzi wa nchi hiyo, hivyo safari yake hii imefuatiliwa sana na vyombo vya habari duniani.

Mkurugenzi wa shirikisho la upelelezi la Marekani FBI Bwana Robert Mueller alifanya ziara katika sehemu ya Afrika kaskazini muda si mrefu uliopita, Bw. Rumsfeld baada ya kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa mkataba wa NATO uliofanyika nchini Italia aliitembelea tena sehemu hiyo. Wachambuzi wameona kuwa, kwa juu juu safari hiyo ya Rumsfeld katika sehemu ya Afrika kaskazini inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Marekani na nchi hizo tatu katika mapambano dhidi ya ugaidi, na kukuza uhusiano wa kiwenzi na nchi hizo tatu katika sekta ya kijeshi na usalama, lakini lengo lake hasa ni kuifanya sehemu hiyo iwe eneo la mikakakti yake ya kijeshi na usalama.

Tarehe 11 Bw. Rumsfeld baada ya kufanya mazungumzo na rais Ben Ali wa Tunisia na waziri wa ulinzi wa nchi hiyo alisema kwenye mkutano na waandishi wa habari kuwa, Marekani inazipongeza Tunisia, Algeria na Morocco kwa juhudi zao katika kupambana na ugaidi, na kuzitaja nchi hizo tatu ziwe washirika wa Marekani  wa kijeshi katika kupambana na ugaidi, na kutumai kuzidisha ushirikiano kati ya Marekani na nchi hizo tatu katika mapambano dhidi ya ugaidi na usalama.

Kuimarisha na kupanua ushirikiano wa kijeshi kati ya Marekani na nchi tatu za Afrika kaskazini ni lengo moja kubwa la ziara ya Bw Rumsfeld. Ili kukabiliana na changamoto ya ugaidi, Marekani inatumai kuandaa kikosi cha kupambana na ugaidi cha nchi hizo tatu za Afrika kaskazini, na kuongeza mazoezi ya kupambana na ugaidi. Marekani inaona kuwa, watu wa kundi la al-Qaeda huenda wanajificha katika sehemu ya kusini mwa Sahara au sehemu ya kusini mwa Afrika kaskazini. Bw. Rumsfled alisema, ameshajadiliana na viongozi wa Tunisia kuhusu kusaini makubaliano ya majeshi ya Marekani na Tunisia kupanua mazoezi ya kijeshi.

Mwito wa Rumsfeld wa kuimarisha ushirikiano wa mapambano dhidi ya ugaidi limeitikiwa na Tunisia. Rais Ben Ali alieleza nia ya kushirikiana na Marekani katika kupambana na ugaidi, na kusisitiza kupiga vita kithabiti vitendo vyovyote vya ugaidi na wenye siasa kali, na kuitaka jumuiya ya kimataifa ziongeze juhudi kuratibu msimamo ili kupambana kwa pamoja dhidi ya ugaidi utakaoleta madhara kwa jamii nzima ya binadamu.

Rais Ali wa Tunisia pia alizitaka nchi zenye ustaarabu tofauti ziimarishe mazungumzo, na kuondoa tofauti kati yao kwa njia ya amani. Bw. Rumsfeld alisema, Marekani itaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika sekta mbalimbali, na kutimiza malengo ya uhusiano wa kimkakati na kiwenzi kati ya nchi hizo mbili.

Wanadiplomasia na wataalamu wa kijeshi wanachukulia kuwa, kusudi lingine la Marekani kuingia katika sehemu ya Afrika kaskazini kwa kisingizio cha sehemu hiyo kukabiliwa na tishio la kundi la al-Qaeda, ni kuimarisha kuwepo kwa jeshi la Marekani katika sehemu ya bahari ya Mediterranean, na kugombea eneo linalodhibitiwa na nchi za Ulaya hasa Ufaransa. Inasemekana kuwa, Marekani inawezekana kujenga kituo cha kijeshi nchini Mauritania, na kuongeza athari yake katika sehemu ya Maghreb na Afrika nzima.

Idhaa ya Kiswahili 2006-02-13