Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-14 16:10:45    
Barua 0212

cri

Msikilizaji wetu Zipporah Anari wa Shule ya Upili ya Mokwerero S.L.P 2995, Kisii, Kenya anaanza barua yake akitoa salamu kwa wafanyakazi wa Radio China Kimataifa, pia anatoa shukrani kutokana na barua tuliyomwandikia. Anasema matangazo ya Radio China kimataifa kwake ni kama kifungua kinywa., na anasema anaamini kuwa idadi ya wasikilizaji wa Radio China kimataifa huko Kisii imeongezeka kwa sababu matangazo yanasikika vizuri na yanaburudisha na kuelimisha.

Katika barua yake anauliza kuwa kama kuna vitabu vya historia ya Radio China kimataifa pamoja na stika zetu angependa tumtumie, kwani anapenda kujifunza mambo mengi zaidi kuhusu China. Anasema wasikilizaji wa Radio China Kimataifa wanaendelea kuongezeka kila siku, na hivi karibuni watu kadhaa wamejiunga na klabu ya wasikilizaji, wanachama hao wapya ni pamoja na Roseline, Charles, Vivian, Grace, Jane, Vencian, Amborze, Gaspar, Walter, na Bilgate.

Tunamshukuru Zipporah Anari kwa barua yake na wenzake wa klabu yao ya wasikilizaji, ni matumaini yetu kuwa mtaendelea kusikiliza matangazo yetu, na ikiwezekana mtuletee barua kutoa maoni na mapendekezo yenu mara kwa mara.

Msikilizaji wetu Ibrahim. Kirusha wa S.L.P 111, Ulyankulu, Tabora, Tanzania anasema katika barua yake kuwa, amepokea barua yetu, na anatoa shukrani kwa kuweza kulipokea ombi lake. Ana uhakika kuwa atapata mafunzo mengi zaidi kupitia majarida na vipindi mbalimbali vya Radio China Kimataifa, kwani mpaka sasa amejifunza mengi ikiwa ni pamoja na aina 12 za wanyama na mwaka wa kuku, vilevile kuhusu chai ya Longjing na mapishi ya vipande vya nyama ya kuku vilivyo kaangwa pamoja na karanga na pilipili, na anasema kuwa anatumai atapata mafunzo mengi zaidi katika siku zijazo.

Vilevile anasema kuwa usikivu wa vipindi vya Radio China Kimataifa katika maeneo anayoishi, si nzuri sana. Hali inayofanya baadhi ya vipindi kutopatikana kwa ufasaha, hivyo anapendekeza kuiboresha mitambo ya Radio China Kimataifa ili wasikilizaji wapate matangazo yake vizuri na kwa ufasaha zaidi.

Anasema atatutumia makala ambayo itaeleza kwa kifupi hali halisi ya mazingira yao anayoishi kwa ujumla ikiambatana pamoja na picha zenye mandhari mbalimbali, ili tuweze kuzitoa katika jarida la urafiki litakalofuata, na wasikilizaji wenzake wataweza kuona mandhari ya huko anakoishi, na anaahidi kuwa atashirikiana nasi kwa lolote lile, ikiwa ni pamoja na kufikisha habari za Radio China Kimataifa katika jamii anayoishi, ili watu wengine waweze kunufaika na matangazo yanayorushwa na Radio China Kimataifa.

Tunamshukuru sana Bwana Ibrahim S.J. Kirusha kwa barua yake na maelezo yake juu ya usikivu wa matangazo yetu kwenye sehemu anayoishi, kuhusu hali hiyo Radio China kimataifa inafanya juhudi siku zote, tuna imani kuwa siku zijazo hali ya usikivu wa matangazo ya Radio China kimataifa popote wasikilizaji wanapoishi itaboreshwa kuwa vizuri.

Msikilizaji wetu Yakobo Muanga wa shule ya seminari Makoko, S.L.P 283, Musoma, Tanzania anasema katika barua yake kuwa, yeye ni mwanafunzi wa kidato cha pili wa shule ya seminari Makoko, na ana umri wa miaka 17. Anapenda kutoa shukrani kwa matangazo yetu. Amekuwa akivifuatilia barabara vipindi vyetu wakati wa likizo yake nyumbani, na amejifunza mengi sana kuhusu China kutoka vipindi vyetu.

Katika barua yake anauliza kuwa, kipindi cha lugha ya Kichina kitamsadiaje kufahamu lugha hiyo pasipo kufahamu hata maneno yake yanavyoandikwa? Na Radio China Kimataifa ina ofisi nchini Tanzania au Afrika Mashariki kwa ajili ya kukusanya habari na huduma kwa wasikilizaji?

Suala hilo kweli ni ngumu kujibu, tuseme kweli tulianzisha kipindi cha kujifunza kichina kwa ajili ya kuwasaidia wasikilizaji wenye hamu ya kujifunza kichina, lakini kutokana na kukosa kitabu kinachohusika, na ni vigumu kwa wasikilizaji wetu kuelewa kichina yenyewe ama kujua maandiko ya kichina, kweli ni vigumu kujifunza, wasikilizaji wetu wakijitahidi wataweza tu kuongea kidogo, lakini itakuwa ni vigumu kuandika.

Lakini tunafanya juhudi kutafuta njia mwafaka kwa kuwasaidia wasikilizaji wenye hamu ya kujifunza kichina. Mwaka jana chuo cha Confucius cha China kilianzishwa katika Chuo kikuu cha Nairobi Kenya, ambapo kuna walimu wanaofundisha kichina, ambao wanapenda kuwasaidia waafrika wengi kujua kichina, ikiwezekana tutashirikiana nao katika kutimiza lengo hilo. Na hatua ya kwanza huenda wasikilizaji wetu walioko Nairobi watapata manufaa kwanza, siku hadi siku, labda tutaweza kuandaa vizuri zaidi kipindi chetu cha kujifunza kichina.

Msikilizaji wetu huyo Bwana Yakobo Muanga anasema amekuwa akisikia sauti zetu mara kwa mara redioni japo hatufahamu hata kwa sura, hivyo anatumai atasoma historia fupi ya kituo cha matangazo, ili afahamu mengi kutoka huku, kwani ameyafahamu baadhi ya mambo na hali ya China kutokana na somo la jiografia na historia. Tena anauliza kuwa, kuna vijana wengi wanaofahamu lugha ya Kiingereza na Kiswahili nchini China? Anapenda kutafuta marafiki wa kalamu kama inawezekana.

Kuhusu suala hilo tunapenda kumwambia kuwa, nchini China wanaojifunza lugha ya kiingereza ni wengi, kwani wanafunzi wanaosoma shule za sekondari na hata siku hizi shule za msingi, wanaanza kujifunza lugha ya kiingereza, lakini kiingereza siyo somo kubwa, kila wiki wanasoma kidogo tu. Na wanafunzi wanaojifunza Kiswahili siyo wengi, kila awamu ya masomo ni wanafunzi wachache wapatao 20 au 40 tu wanaojifunza Kiswahili katika chuo kikuu cha radio cha Beijing au chuo kikuu cha lugha za kigeni cha Beijing. Kujifunza Kiswahili ni chaguo la wanafunzi wachache ambao wanapenda kuijua zaidi hali ya Bara la Afrika.

Lakini tokea reli ya TAZARA ijengwe mpaka sasa, wanafunzi waliowahi kujifunza Kiswahili siyo wachache sana, miongoni mwao wengi waliojifunza Kiswahili walishiriki kwenye ujenzi wa reli ya TAZARA, ama walikuwa wakalimani wa wizara ya mambo ya nje, wizara ya utamaduni, wizara ya biashara au shirika la habari la Xinhua, na wengine ni kama sisi watangazaji na watayarishaji wa vipindi idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa, hata miongoni wetu, watangazaji wazee kadha wa kadhaa wameshastaafu. Na idara yetu siku hizi kuna vijana wengi waliohitimu katika miaka ya hivi karibuni.

Msikilizaji wetu Philip Machuki wa klabu ya wasikilizaji ya Nyankware P.O. Box 646 Kisii, Kenya anasema katika barua yake kuwa, Radio China Kimataifa imepiga hatua mbele sana katika kuwahudumia wasikilizaji wake katika mwaka 2005. Anasema kitu cha kwanza ambacho wasikilizaji wanaweza kujifunza katika mwaka 2005 ni kuchapishwa kwa Jarida la Daraja la Urafiki, ambalo kwa kweli wasikilizaji wengi wanalipenda. Na ni furaha yao kuona ya kwamba barua nyingi za wasikilizaji pia zinatumika katika jarida hili.

Anapendekeza kuwa, kama ikiwezekana tunaweza kujumuisha yafuatayo katika jarida hilo, kwa mfano, anuani na majina ya wasikilizaji wa idhaa ya Radio China Kimataifa; chemsha bongo; watangazaji wa Radio China Kimataifa, washindi wa chemsha bongo; barua, mashairi pamoja na picha za wasikilizaji.

Anasema kitu cha pili katika mwaka 2005 ni wakuu wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa kuongeza muda wa matangazo kutoka nusu saa hadi saa nzima. Anaeleza kuwa kwa kweli kuongezwa kwa muda wa matangazo kumewasaidia sana kusoma, kufahamishwa na kuelewa mengi kuhusu taifa la China ambalo sasa linakua zaidi kwa uchumi. Mwishowe anaitakia idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa iwe na maendeleo makubwa zaidi katika mwaka 2006 kuliko mwaka jana.

Tunamshuruku msikilizaji wetu Philip Machuki kwa barua yake na matumaini mazuri, pia tunamshukuru kwa juhudi anazofanya siku zote za kutusaidia. Kweli juhudi zetu za kuandaa vipindi haziwezi kutengana na uungaji mkono wa wasikilizaji wetu wengi, kila tukipata barua kutoka kwa wasikilizaji wetu, tunaona tunatiwa moyo wa kuchapa kazi zaidi.

Na tukiwa tunakaribia kukamilisha kipindi hiki cha leo, tunatoa maswali mawili kwa wasikilizaji wetu wanaosikiliza matangazo kwenye 91.9 FM huko Nairobi Kenya ili wajibu.

Swali la kwanza, Kituo cha 91.9 FM cha Radio China kimataifa kilichozinduliwa rasmi tarehe 28 Januari huko Nairobi Kenya kila siku kinatangaza kwa lugha gani? Taja lugha tatu?

Swali la pili, matangazo ya Kiswahili kwenye 91.9 FM yanasikika kwa saa ngapi kwa siku ?

Ni matumaini yetu kuwa wasikilizaji mtajibu vizuri maswali haya na kututumia majibu haraka iwezekanavyo, ili waweze kupewa zawadi.

Idhaa ya kiswahili 2006-02-14