Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-15 15:20:27    
Inasemekana kuwa Marekani na Israel zana njama ya kuupindua utawala wa Hamas

cri

Habari kutoka vyombo vya habari vya Marekani zinasema serikali za Marekani na Israel zimekuwa zikipanga haraka hatua za kuitenga na kuzingira kiuchumi Palestina ili kuulazimisha utawala wa Hamas uporomoke wenyewe.

Gazeti la the New York Times linasema, japokuwa kundi la Hamas lililoshinda kwenye uchaguzi wa bunge uliofanyika mwezi mmoja uliopita haijaunda rasmi serikali, viongozi waandamizi wa serikali ya Marekani wamekuwa wakijadiliana kisiri mpango wa kuulazimisha utawala wa Hamas kuporomoka, hatua muhimu zitakazochukuliwa ni kuikatia Palestina misaada yote kutoka nje na uhusiano wake na nchi za nje ili kuwachochea watu wa Palestina waipinge Hamas, na kupata lengo la "kuipindua serikali ya Hamas bila vita". Licha ya hatua hizo, Israel iko tayari kuchukua hatua nyingine za kuutikisa utawala wa Hamas zikiwa ni pamoja na kuzuia uhuru wa safari za watu wa Palestina, kukata maingiliano ya bidhaa kati ya ukingo wa magharibi wa mto wa Jordan na sehemu ya Gaza, kupiga marufuku watu wa Palestina kwenda Israel kufanya kazi. Inasemekana kwamba mstari wa mwisho wa Marekani kwa Hamas ni kuwa Hamas lazima itambue haki ya kuishi kwa Israel, iache silaha na vitendo vya nguvu na ikubali mikataba yote ya zamani iliyotiwa saini, vinginevyo Hamas itakabiliwa na utenge na utawala wake kuanguka. Habari kutoka vyombo vya habari vya Israel zinasema, waziri wa ulinzi wa Israel Bw. Shaul Mofaz tarehe 14 alisema kwa maneno makali, kwamba Israel ina nguvu za kutosha kupambana na "hali yoyote itakayotokea", ikiwa Hamas itaendesha utawala wa Palestina ikiwa "kundi la ugaidi", Israel "itakuwa na hatua za kutosha kupambana nayo."

Ingawa Marekani imekanusha habari zilizotangazwa kwenye gazeti la the New York Times, lakini kujaribu kuitiisha Hamas kwa hatua za kiuchumi ni ukweli usiofichika. Mapema kabla ya uchaguzi wa bunge wa Palestina kufanyika, Marekani na Israel zilikuwa zimeanza kuvumisha "fimbo za kiuchumi" kwa Hamas. Marekani iliwahi kutishia kwamba ikiwa Hamas itashiriki katika serikali ya mamlaka ya utawala wa Palestina, Marekani itasimamisha msaada wa kiuchumi kwa Palestina wenye dola za Kimarekani bilioni moja kwa mwaka. Israel pia ilitishia kwamba Itakataa kukabidhi mamlaka ya Palestina mapato ya kodi ya dola za Kimarekani milioni 50 kwa mwezi yaliyokusanywa na Israel kwa niaba ya mamlaka ya Palestina ili kulazimisha Hamas kubadilisha mipango wa kisiasa.

Palestina, nchi ambayo inategemea sana misaada kutoka nje hakika itakuwa tatizo kubwa iwapo Marekani ikiizingira Palestina kiuchumi. Takwimu zinaonesha kuwa hata kama Marekani itaendelea na msaada wake kwa Palestina, mamlaka ya Palestina pia ina upungufu wa dola za Kimarekani milioni 600, kama chanzo cha fedha likikabwa, sio tu shughuli za serikali ya Palestina zitashindwa kuendeshwa, lakini pia ahadi za kuboresha maisha ya watu wa Palestina zilizotolewa na Hamas wakati wa kampeni za kugombea uchaguzi zitakuwa ahadi hewa.

Msemaji mmoja wa kundi la Hamas tarehe 14 alisema, hatua za Marekani na Israel kulilazimisha liache utawala ni kuingilia kati mambo ya ndani ya Palestina na pia ni adhabu kwa "watu wote wa Palestina". Ili kuvunja njama za Marekani na Israel, Hamas inajitahidi kutafuta njia nyingine. Hivi sasa kiongozi wa kisiasa wa Hamas Khaled Mashaal akiongoza ujumbe wake kutembelea nchi za Kiarabu ili kupata misaada ya kiuchumi. Inasemekana kwamba Saudi Arabia na Katar zimeahidi kutoa msaada wenye dola za Kimarekani milioni kumi kadhaa kwa Palestina, isitoshe, Hamas inatumai kuwa nchi za Umoja wa Ulaya zilizokuwa zinatoa misaada mingi zibadilishe msimamo na kusaidia kwa ukarimu.

Wachambuzi wanaona hatua za Marekani na Israel zitachochea chuki za watu wa Palestina kwa nchi hizo. Zaidi ya hayo, rais wa Russia amemwalika kiongozi wa Hamas kufanya ziara nchini Russia, serikali ya Ufaransa pia inataka kufanya mazungumzo na Hamasi. Kwa hiyo, maofisa wa usalama wa Israel wanaona kuwa hatua za Marekani na Israel za kujaribu kuupindua utawala wa Hamas huenda hazitakuwa na matokeo kama yanayotarajiwa.

Idhaa ya kiswahili 2006-02-15