Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-15 16:15:32    
Mwanasayansi Ye Duzheng aliyepata tuzo ya taifa ya sayansi na teknolojia ya juu nchini China

cri

Siku chache zilizopita, sherehe ya kutoa tuzo ya taifa ya sayansi na teknolojia ya juu mwaka 2005 ilifanyika mjini Beijing. Katika sherehe hiyo Bw. Ye Duzheng na mwanasayansi mwingine walipata tuzo hiyo.

Bw. Ye Duzheng alizaliwa miaka 90 iliyopita mjini Tianjin. Katika mwaka alipozaliwa ndipo ripoti ya kwanza kuhusu hali ya hewa ya China ilipotolewa, ilikuwa ni kama ishara ya kwamba Bw. Ye Duzheng atahusika na metorolojia maishani mwake. Kadiri alivyokua, Bw. Ye Duzheng alikuwa na hamu kubwa zaidi na mambo ya metorolojia. Baada ya kuhitimu masomo ya chuo kikuu nchini China alikwenda Marekani kujiunga na Chuo Kikuu cha Chicago kusoma kozi ya metolojia na alipata shahada ya udaktari. Alirudi nyumbani China mwaka 1950 na akawa mmoja wa waanzilishi wa elimu ya metorolojia nchini China.

Katika utafiti wake alioufanya kwa zaidi ya miaka hamsini alipata mafanikio yaliyokuwa ya mwanzo kabisa katika nyanja za elimumwendo ya angahewa, mzunnguko wa angahewa na elimu ya metolojia. Siku kadhaa ziizopita, baada ya kupata tuzo ya taifa ya sayansi na teknolojia ya juu Bw. Ye Duzheng alieleza "siri" ya mafanikio yake. Alisema, "Kanuni yangu ya utafiti ni kutafuta ukweli, ukweli na ukweli, na kuwa makini, makini na makini. Naona kwamba kila mwanasayansi anapaswa kufuata kanuni hiyo."

Kutafuta ukweli na kuufanya utafiti kwa makini ni msimamo wa Ye Duzheng kutenda kazi. Ili kukusanya nyenzo, mara nyingi alikwenda kwenye nyanda za juu na jangwani ambapo mazingira ya kuishi ni magumu kufanya uchunguzi, na hatimaye alifanya utafiti kwa makini. Kutokana na uchunguzi na utafiti wake, alianzisha uwanja wa sayansi ya metorolojia kwenye nyanda za juu, amepata jawabu jinsi nyanda za juu za Qinghai-Tibet za China zinavyoathiri mzunguko wa angahewa na mabadiliko ya hali ya hewa ya Asia ya Mashariki, na amegundua jinsi mzunguko wa angahewa unavyoathiri upepo wa musimu wa Asia ya Mashariki.

Kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa duniani, Bw. Ye Duzheng ni mmoja wa wataalamu wachache wanaotetea kufanya utafiti huo. Bw. Ye Duzheng alihusisha shughuli za binadamu kama umwagiliaji, upandaji miti zilizosababisha mabadiliko ya sura ya dunia na mabadiliko ya hali ya hewa, ameweka msingi wa nadharia kuhusu uhusiano kati ya shughuli za binadamu na mabadiliko ya hali ya hewa.

Bw. Ye Duzheng aliwaambia waandishi wa habari kuwa, siku zote anafanya utafiti kwa kufuata mahitaji ya taifa. Alisema,

"Kazi lazima ilingane na mahitaji ya taifa, ili taifa linapohitaji niweze kutumia njia ya kisasa kufanya utafiti."

Kutokana na mafanikio yake makubwa, Bw. Ye Duzheng alichaguliwa kuwa mwanasayansi wa Taasisi ya Sayansi ya China, mwanasayansi wa heshima wa Royal Meteorological Society nchini Uingereza na mwanasayansi wa American Meteorological Society, na alisifiwa na ofisa mwandamizi wa Shirika la Metorolojia Duniani kuwa ni "mwanasayansi mashuhuri mwenye heshima duniani".

Bw. Ye Duzheng mbali na kufanya utafiti amewafundisha wanafunzi wengi, na licha ya kuwafundisha elimu ya sayansi, naye pia aliwalea kwa maadili mema ya mwanadamu. Kati ya wanafunzi wake, wengi wamekuwa uti wa mgongo katika nyanja ya metorolojia. Bw. Huang Ronghui mwenye umri wa zaidi ya miaka sitini alikuwa mwanafunzi wa Ye Duzheng, hivi sasa amekuwa mwanasayansi wa Taasisi ya Sayansi ya China, alisema, ufanisi wake unatokana na mafunzo kutoka kwa mwalimu wake, "Nimejifunza mengi kutoka kwa mwalimu wangu Ye Duzheng. Maendeleo niliyopata hivi sasa yote yanatokana na kufundishwa naye. Bwana Ye Duzheng ni mtu mwenye makini sana katika utafiti, na ni mtu mwenye msamaha mkubwa kwa wengine. Yeye sio tu mwalimu wa elimu bali pia ni mfano wa kuwatendea watu wema, moyoni mwangu yeye daima ni mtu mkubwa."

Ingawa Bw. Ye Duzheng amekuwa mzee sana, hata hivyo hakuacha kazi ya utafiti anayoipenda. Akiwa mkuu wa heshima wa kitengo cha fizikia ya angahewa katika Taasisi ya Sayansi ya China, kila siku anafanya kazi kwa muda wa saa nane. Alisema, ingawa maendeleo makubwa yamepatikana katika utafiti wa metorolojia, lakini ikilinganishwa na nchi zilizoendelea mafanikio hayo bado yako nyuma. Kwa mfano, nchi zilizoendelea zinaweza kutabiri vilivyo hali ya hewa katika wiki mbili zijazo, lakini China inaweza tu kutabiri siku nne zijazo.

Mkuu wa kitengo cha fizikia ya angahewa katika Taasisi ya Sayansi ya China Bw. Wang Huijun aliwaambia waandishi wa habari kuwa alipata msaada mkubwa kutoka kwa mzee Ye Duzheng katika muda wa miaka minne tokea aliposhika wadhifa wa uongozi wa kitengo hicho. Alisema, "Mzee Ye Duzheng huwa na fikra za kutangulia mbele katika utafiti kuliko wengine, tumeweza kuhisi kwamba kila wakati anajitahidi kuvumbua mbinu za kutatua matatizo. Mtindo mzuri wa kazi katika kitengo chetu unatokana na msingi uliowekwa na wanasayansi wazee kama Ye Duzheng, na kuibuka kwa wanasayansi vijana wengi katika kitengo chetu pia ni matokeo ya athari yake."

Bw. Ye Duzheng mwenye umri wa miaka tisini mwaka huu ana afya njema, alisema siri yake ya kuwa na afya njema ni kufanya mazoezi. Anashikilia kwenda kazini na kurudi nyumbani kwa miguu katika miaka mingi, kila siku anatumia dakika 50 hadi 60 njiani. Ye Duzheng alisema, furaha yake maishani mwake ni kufanya utafiti na kusoma vitabu vya burudani. "Ninaposikia uchovu napumzisha akili yangu kwa kusoma vitabu vya burudani, yaani riwaya. Napenda sana kusoma vitabu vya riwaya za gonfu, nimewahi kusoma karibu vitabu vyote vya riwaya za gonfu vilivyoandikwa na mwandishi mashuhuri Jin Yong."

Aidha, Bw. Ye Duzheng alisema, yeye ni mpenzi wa chakula, anapenda kula chakula cha baharini. Siku chache zilizopita alikula kaa watatu na akawa mgonjwa, lakini hakujuta, alisema, chakula kitamu ni aina ya furaha ya maisha.

Idhaa ya kiswahili 2006-02-15